Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya B.Maria wa Altagracian: 1922-2022: Ushuhuda wa Imani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria wa Altagracian, alipotangazwa rasmi kuwa ni Mama mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Wadominican, kunako tarehe 15 Agosti 1922, Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei hii, alimteuwa Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican kuwa mwakilishi wake maalum katika sherehe za kufunga mwaka wa Jubilei. Katika maadhimisho haya, Askofu mkuu Edgar Peña Parra, amepata nafasi ya kusali pamoja na mahujaji waliofika kwenye mkesha wa maadhimisho haya, tarehe 14 Agosti 2022, kwa kumwomba Bikira Maria kuwasindikiza Wadominican katika hija ya maisha yao hapa duniani, huku wakiendelea kuwasha moto wa imani, matumaini na mapendo. Askofu mkuu Edgar Peña Parra amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali na Kidini na hatimaye, akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kielelezo cha kufunga rasmi Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria wa Altagracian, alipotangazwa rasmi kuwa ni Mama mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Wadominican, kunako tarehe 15 Agosti 1922. Amewaalika watu watakatifu na wateule wa Mungu Jamhuri ya Wadominican, kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwasindikiza katika hija ya maisha yao ya kiroho kwa kujikita katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa hususan Ekaristi Takatifu ili kuweza kukabiliana kikamilifu na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza katika maisha yao.
[ Photo Embed: Watu wa Mungu Jamhuri ya Wadominican iwe ni shuhuda wa imani na mapendo]
Wadominican wawe ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika moto wa huruma na upendo wa Mungu uliowashwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, chimbuko la msamaha wa dhambi, maisha na uzima wa milele. Ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni mapambano endelevu na fungamani yanayohitaji nguvu ya upendo na huruma ya Mungu. Ni mwaliko wa kukesha na kuomba, ili wasitumbukie kwenye majaribu, kwa kuwa karibu na Kristo Yesu katika: Sala, Neno, Sakramenti na huduma makini kwa jirani. Waamini waendelee kumwomba Bikira Maria ili katika umaskini, unyonge na udhaifu wao wa kibinadamu, awaombee na kuwategemeza katika uvumilifu, utii, unyenyekevu na huduma makini kwa maskini na wahitaji zaidi. Awaombee neema ya kuendelea na hija hii ya maisha ya kiroho, kwa kutambua na kuhisi uwepo wa Kristo Yesu na Bikira Maria katika maisha na utume wao, ili waweze kushikamana katika umoja, ushiriki na utume wa Mama Kanisa.
Askofu mkuu Edgar Peña Parra Amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali na Kidini, pamoja na mambo mengine, amekazia umuhimu wa Ibada kwa Bikira Maria wa Bikira Maria wa Altagracian anayeheshima sana nchini humo na ambaye amekuwa mhimili mkuu katika ujenzi wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kumekuwepo na mifumo mbalimbali ya ukoloni hadi wakati huu ambapo ukoloni wa kiitikadi unaendelea kushamiri, Mama Kanisa anasema kwamba, huu ni ukiukwaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Yote hii ni mifumo inataka kudhohofisha mshikamano na mafungamano ya watu asilia; kanuni maadili na utu wema, hali ambayo inataka kuwang’oa watu kutoka katika mila, desturi na tamaduni zao njema. Watu wa Mungu Amerika ya Kusini wanapaswa kuwa macho dhidi ya Ukoloni wa Kiitikadi unaotaka kumeng’enyua utakatifu wa maisha kwa kupandikiza utamaduni wa kifo; kwa kuvunjilia mbali tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, mambo ambayo ni msingi wa jamii, ukuaji na afya ya binadamu. Ukoloni wa kiitikadi unataka kupoka matumaini ya vijana wa kizazi kipya, kwa kuwatumbukiza katika ulaji wa kupindukia na mambo mpito!
Askofu mkuu Edgar Peña Parra katika maadhimisho ya ibada ya Misa Takatifu kama kielelezo cha kufunga rasmi Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria wa Altagracian, alipotangazwa rasmi kuwa ni Mama mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Wadominican, kunako tarehe 15 Agosti 1922 amewasilisha: baraka, salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni siku ya kumshukuru, kumwabudu na kumtukuza Mwenyezi Mungu, ili kuendelea kujizatiti ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ni wakati wa kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya sera na mikakati ya ukoloni mamboleo. Watu wateule na watakatifu wa Mungu watambue kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Waamini wajitahidi kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.
Hapa ni mahali pa kukaribisha zawadi ya maisha, kuadhimisha na kutangaza Habari Njema ya Wokovu ili kuchochea na kukoleza utakatifu wa maisha, tayari kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii kwa kizazi cha sas ana vile vijavyo, kwa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Askofu mkuu Edgar Peña Parra amewataka vijana kufanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa. Wasimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wajenge na kuimarisha dhamiri adili itakayowasaidia kuchagua mema dhidi yam abaya. Vijana wasipende kula raha kupita kiasi, bali wajijengee utamaduni wa kuwa na kiasi, ujasiri wa kusonga mbele, wastahimilivu na wavumilivu katika mchakato wa kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku. Vijana wajiepushe na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; tabia ya kutaka kujimwambafai na mambo kama hayo. Wajijengee utamaduni wa kuwajibika katika mifumo mbalimbali ya maisha: kiroho, kijami, kiuchumi, kitamaduni na Kikanisa, ili hatimaye, kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waendeleze na kudumisha: tamaduni, mila na desturi njema kutoka kwa wazazi wao, wawe wajasiri na vyombo vya matumaini. Wazazi na walezi watekeleze dhamana na wajibu wao kikamilifu, ili waendelee kuwa ni watu wenye furaha, ukarimu, uaminifu pamoja na kujitoa. Watu wa Mungu Jamhuri ya Wadominican, iwashe moto wa: Ushirika, upendo, ukarimu na mshikamano wa kidugu.