Tafuta

Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu, Jimbo kuu la Roma kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 24 Julai 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Siku ya Wazee na Wajukuu 2022. Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu, Jimbo kuu la Roma kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 24 Julai 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Siku ya Wazee na Wajukuu 2022. 

Siku ya Wazee na Wajukuu Kwa Mwaka 2022: Mashuhuda wa Huduma ya Upendo na Sala

Kardinali Angelo De Donatis, amekazia umuhimu na udumifu katika maisha ya sala, kwa ajili ya kuombea: haki na amani duniani; afya njema, maridhiano kati ya watu wa Mataifa bila kusahau kujiombea wao wenye na mahitaji msingi ya familia zao. Wazee wengi ni wale waliozaliwa mara baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kumbe ni watu walioshuhudia madhara ya vita katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Pili ya Wazee na Wajukuu Duniani, tarehe 24 Julai 2022 anawaalika wazee kutoogopa uzee na kudhani kwamba, uzee ni ugonjwa na kamwe wasielemewe na utamaduni wa kutupa, usiojali utu, heshima na haki msingi za binadamu. Bali watambue kwamba, maisha marefu kadiri ya Maandiko Matakatifu: wazee ni baraka, ishara hai ya wema na huruma ya Mungu ambaye ni chemchemi ya maisha. Heri nyumba anamoishi mzee na heri kwa familia inayotunza na kuwaheshimu wazee. Jamii inapaswa kuhakikisha kwamba, sera na mikakati kwa ajili ya huduma kwa wazee, zinawajengea matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwani hata katika uzee wao wataendelea kuzaa matunda. Katika uzee, watu wanatambua kwamba, nguvu zinapungua na afya inaanza kudhohofu kiasi cha kuanza kujihisi kwamba, “si mali kitu katika jamii inayowazunguka.” Ikumbukwe kwamba, uzee si hukumu ya kifo, bali ni chemchemi ya baraka na neema. Ni mwaliko wa kuendelea kuboresha hata maisha ya kiroho kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu; kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa sanjari na kuendelea kuboresha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na huduma makini kwa jirani, wanaohitaji sala, sadaka na uwepo wao angavu!

Wazee waboreshe maisha yao ya kiroho kwa sala, Neno la Mungu na huduma
Wazee waboreshe maisha yao ya kiroho kwa sala, Neno la Mungu na huduma

Baba Mtakatifu anawataka wazee wawe ni baraka na neema kwa jirani zao wanaowazunguka. Uzee si wakati wa kutaka wala kukatishwa tamaa na wala wazee hawapaswi kuelemewa na mawazo wala hofu zisizo na miguu wala kichwa! Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee.” Zab 92:15. Wakati huo huo, Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu, Jimbo kuu la Roma kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 24 Julai 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Wazee na Wajuu Duniani. Amewakumbusha wazee na wajukuu wao waliohudhuria Ibada hii ya Misa Takatifu kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa yuko nchini Canada kama hujaji wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, ndiye aliyetia nia ya kuanzishwa kwa siku hii malum, ili kuwaenzi wazee wanaopaswa kuendelea kuzaa matunda ya hekima, imani thabiti na upendo kama kielelezo makini cha imani tendaji.

Kardinali Angelo De Donatis, amekazia umuhimu na udumifu katika maisha ya sala, kwa ajili ya kuombea: haki na amani duniani; afya njema, maridhiano kati ya watu wa Mataifa bila kusahau kujiombea wao wenye na mahitaji msingi ya familia zao. Wazee wengi ni wale waliozaliwa mara baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kumbe ni watu walioshuhudia madhara ya vita katika maisha ya mwanadamu, wakajitahidi kujenga urafiki na muungano na Mwenyezi Mungu, ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa amani duniani. Sala inapaswa kujengeka katika mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu yanayoshuhudiwa katika upendo. Waamini wajitahidi kujenga maisha ya sala katika msingi wa imani na kamwe wasikate tamaa bali waendelee kuwa wabunifu na wadumifu katika maisha ya sala. Mwenyezi Mungu ameonesha upendo wa hali ya juu sana kwa binadamu kiasi cha kuwakirimia Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili amkomboe mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Akawajalia pia Roho Mtakatifu anayeliongoza na kulitakatifuza Kanisa.

Wazee ni baraka na ishara ya wema na huruma ya Mungu
Wazee ni baraka na ishara ya wema na huruma ya Mungu

Wajukuu na vijana wawe ni mashuhuda wa Injili ya upendo na huduma hasa kwa kuwatembelea wazee kwani kwa kufanya hivyo, wanatekeleza matendo ya huruma. Waamini watambue kwamba, Sala kuu ya Baba Yetu Uliye Mbinguni, ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, inayokazia ushirika wa watoto wa Mungu. Kadiri ya Mwinjili Luka, ushirika huu unasimikwa katika: mahitaji msingi ya binadamu; msamaha na mapambano dhidi ya dhambi na Shetani, Ibilisi, ili kujengha ushirika thabiti kati ya Mungu na jirani. Mwenyezi Mungu amejifunua kama rafiki ya binadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani, kumbe, waamini wajenge ujasiri wa kukutana na Mwenyezi Mungu katika: Sala, Neno na Sakramenti za Kanisa, mambo msingi yanayomwilishwa katika Injili ya huduma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Waamini watambue kwamba, wote ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi. Wajitahidi kumwomba Bikira Maria ili awafundishe kuwa na huruma sawa sawa na wazazi wake, yaani watakatifu Joakim na Anna.

Wazee na Wajukuu

 

24 July 2022, 15:33