Tafuta

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican mwezi Septemba 2022 inaadhimisha Kumbukizi la Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake. 7 Julai 2022 Ni Siku ya Kiswahili Duniani. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican mwezi Septemba 2022 inaadhimisha Kumbukizi la Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake. 7 Julai 2022 Ni Siku ya Kiswahili Duniani. 

Siku ya Kiswahili Duniani: Miaka 30 ya Idhaa ya Kiswahili Radio Vatican

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican mwezi Septemba 2022 inaadhimisha Kumbukizi la Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, kiungo muhimu katika mchakato wa uinjilishaji miongoni mwa watu wa Mungu wanaozungumza Lugha ya Kiswahili. UNESCO tarehe 23 Novemba 2021 ilitangaza kwamba, kila mwaka tarehe 7 Julai ni Siku ya Kiswahili Duniani. Vatican inaendelea kukipatia msukumo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Lugha ni chombo muhimu sana cha mawasiliano kilichoundwa na sauti za nasibu za kusemwa na kutumiwa na jamii ya utamaduni fulani. Jinsi ambavyo zipo jamii nyingi za tamaduni mbalimbali duniani, vivyo hivyo ziko lugha mbalimbali zilizoundwa kukidhi haja ya mawasiliano ya tamaduni mbalimbali. Maingiliano ya jamii zenye tamaduni na lugha mbalimbali yanayotokana na mashirikiano katika shughuli za biashara na nyinginezo za kijamii, huzusha haja ya kuwepo kwa lugha moja itakayoweza kuwaungaanisha watu hao wenye tamaduni na lugha mbalimbali. Maingiliano kama hayo yanaweza kuwa katika viwango mbalimbali. Kiwango cha kwanza ni kile cha mtu binafsi ambapo mtu hutoka kwenye jamii yake na kwenda kuishi kwenye jamii inayozungumza lugha tofauti na ile ya kwao. Katika hali kama hiyo, mtu huyo itabidi ajifunze lugha ya jamii ile ya pili ili aweze kuwasiliana nao. Kiwango cha pili ni kile kinachohusisha mkusanyiko wa watu waliotoka kwenye tamaduni mbalimbali na hawana hata lugha moja ya kuwaunganisha. Watu kama hawa wakikaa pamoja huweza kuzusha lugha ya kati ambayo katika hatua za mwanzo itajulika nazo kama Pijini na baadaye kama Krioli. Kiwango cha tatu ni kile ambacho maingiliano ya watu wenye tamaduni na lugha mbalimbali husababisha kuteuliwa kwa lugha moja miongoni mwa lugha zao na kutumika kama chombo cha mawasiliano na cha kuziunganisha jamii zote husika. Kiwango hiki chaweza kujitokeza katika ngazi ya wilaya, mkoa, nchi, kanda, bara na hata ulimwengu mzima.

Katika mchakato wa kukuza na kudumisha Lugha ya Kiswahili kwa upande wa Vatican, hadi sasa jitihada kubwa zimekwisha kufanywa, ili kutafsiri nyaraka mbalimbali za Kanisa hasa tangu maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican hadi wakati huu katika lugha ya Kiswahili. Nyaraka hizi zinapatikana kwenye Tovuti rasmi ya Vatican: www.vatican.va. Mababa wa Kanisa wanasema, Liturujia ni kilele ambapo kazi za Kanisa inaelekea, na papo hapo ni chemchemi zinamotoka nguvu zake zote. Maana, bidii zote za kazi za kitume hukusudiwa ili wote, waliofanywa watoto wa Mungu kwa njia ya Imani na Sakramenti ya Ubatizo, wakusanyike pamoja, wamtukuze Mwenyezi Mungu katika Kanisa, washiriki sadaka na kuila karamu ya Bwana, Rej. SC 10. Kiswahili ni kati ya lugha zinazolitambulisha Bara la Afrika katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa zinazoadhimishwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni katika muktadha huu, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican mwezi Septemba 2022 inaadhimisha Kumbukizi la Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, kiungo muhimu katika mchakato wa uinjilishaji miongoni mwa watu wa Mungu wanaozungumza Lugha ya Kiswahili. Bado kuna changamoto pevu zinazopaswa kuvaliwa njuga.

Ni katika muktadha huu, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO katika mkutano wake wa 41 uliofanyika mjini Paris, Ufaransa, tarehe 23 Novemba 2021 uliamua kwamba, tarehe 7 Julai ya kila mwaka itakuwa ni Siku ya Kiswahili Duniani. Azimio hili lilipitishwa na wanachama wote wa UNESCO bila kupingwa. Waswahili kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wakafurahia sana tamko hili, kwa Umoja wa Mataifa kuamua kutoa kipaumbele cha pekee kwa Lugha ya Kiswahili. Hii ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kutoka Barani Afrika kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na kutengewa siku maalum ya kuadhimishwa Kimataifa. Kiswahili kinatambulikana kuwa ni lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Bunge la Afrika. Lakini, ikumbukwe kwamba, Kiswahili ni kati ya lugha zinazozungumzwa na watu wengi duniani.

Lugha ya Kiswahili imekuwa ikitumika pia kama utambulisho wa watu wa Mungu Barani Afrika
Lugha ya Kiswahili imekuwa ikitumika pia kama utambulisho wa watu wa Mungu Barani Afrika

Profesa John G. Kiango kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania anasema, dhima kuu ya lugha yoyote ni kukidhi haja ya mawasiliano katika jamii yenye utamaduni mmoja. Pamoja na dhima hiyo muhimu, lugha hutumika pia kama kitambulisho cha jamii fulani na vilevile kama njia mojawapo ya kuelezea na kuhifadhia utamaduni wake. Hata hivyo, kutokana na maingiliano ya watu, zipo lugha ambazo zimevuka mipaka ya jamii zao husika na kutumika kama vyombo vya mawasiliano katika jumuiya kubwa zaidi zenye watu wenye lugha na tamaduni tofauti. Lugha kama hizo hazikidhi haja ya mawasiliano ya jamii zao tu, bali hukidhi haja ya mawasiliano katika jamii pana zaidi katika nchi, kanda, au dunia nzima. Lugha zenye dhima kama hii, hujulikana kama lugha-mawasiliano (lingua franca). Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, lugha inayoweza kuchaguliwa kama lugha ya kuzitambulisha na kuziunganisha jamii katika nchi hizi ni Kiswahili. Kiswahili kimevuka mipaka ya nchi zao asilia yaani Tanzania na Kenya na kuenea karibu kwenye nchi zote Afrika Mashariki na Kati japo kwa viwango tofauti. Hakuna lugha nyingine ya Kiafrika katika nchi hizi za Afrika Mashariki yenye sifa kama hiyo. Kwa hiyo, Kiswahili kinafaa kuchukuliwa kama lugha ya utambulisho wa wananchi wa Afrika Mashariki na vilevile lugha ya kuwaunganisha.

Katika nchi za Afrika Mashariki, lugha za Kiingereza na Kiswahili zinatumika sana katika mawasiliano. Nchini Tanzania, Kiswahili hutumika kama lugha ya Taifa, lugha rasmi katika shughuli za serikali na bunge, lugha ya mawasiliano katika shughuli za biashara za nchini, na baina yake na nchi jirani, lugha inayotumika katika vyombo vya habari na vilevile lugha ya kufundishia katika shule za msingi. Nchini Kenya, Kiswahili hutumika kama chombo cha mawasiliano baina ya watu wa makabila mbalimbali, katika mikutano ya kisiasa na wananchi, katika shughuli za biashara za nchini na baina yake na nchi jirani, na hufundishwa kama somo katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu. Nchini Uganda, Kiswahili hutumiwa zaidi na askari na katika kufanya mawasiliano na wageni kutoka nchi jirani za Afrika Mashariki hususani katika biashara, shughuli za kijamii n.k.

Siku ya Kiswahili Duniani 2022 Kitaifa Dar es Salaam
Siku ya Kiswahili Duniani 2022 Kitaifa Dar es Salaam

Tarehe 30.11.2001, Serikali za Tanzania, Kenya na Uganda, zilitiliana saini mkataba wa ushirikiano mpya wa Afrika Mashariki. Ushirikiano huu mpya umeanzishwa kwa tahadhari kubwa ili usikumbwe na matatizo yaliotokea kwenye ushirikiano wa awali, matatizo yaliyosababisha kuvunjika kwa ushirikiano huo. Ushirikiano mpya wa Afrika Mashariki umefungua milango mingi ya ushirikiano katika nyanja za biashara, elimu, uchumi, kijamii na kisiasa. Iko azma ya kuwa na mipaka huru baina ya nchi husika, soko la pamoja la bidhaa za biashara baina ya nchi hizo, sarafu moja n.k. Mazingira kama hayo yatafanya maingiliano baina ya watu wa Afrika Mashariki kuwa makubwa zaidi hususani kwenye nyanja za kiuchumi, kielimu na kijamii. Mazingira kama hayo yatanufaika zaidi kama Kiswahili kitatiliwa maanani katika nchi hizi. Katika kufikiria kwa dhati dhima ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano, utambulisho na kiunganishi cha watu wa Afrika mashariki, kuna haja ya kuwa na mikakati bayana ya kufikia lengo hilo.

Profesa John G Kiango anasema Malengo ya Kimkakati na Dira ya Kimkakati itaielekeza Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye kuunda na kuendeleza asasa za Kiswahili katika Afrika Mashariki, na kutilia mkazo mafunzo ya Kiswahili kwa watu wake. Katika kufanikisha hilo, malengo ya kimkakati yawe ni pamoja na uundaji na ukuzaji wa asasi za kukuza na kusimamia maendeleo ya Kiswahili, kuhimiza na kusimamia matumizi ya Kiswahili katika vyombo vyake kama vile redio, magazeti, mabunge n.k., na kuhimiza mafunzo ya Kiswahili katika nchi husika kwa kubadilishana walimu, vitabu na uzoefu. Nchini Tanzania, katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, yanayofanyika kitaifa Jijini Dar es Salaam, tarehe 7 Julai 2022, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho haya. Rais Mstaafu Joachim Chisano wa Msumbiji, aliyewahi kutoa hotuba yake kwenye Umoja wa Afrika kwa lugha ya Kiswahili yuko tayari nchini Tanzania kushiriki katika maadhimisho haya. Wengine ni Mheshimiwa Sam Nujoma, Rais Mstaafu wa Namibia. Hawa wanatambua fika mchako wa lugha ya Kiswahili katika harakati za ukombozi Kusini mwa Bara la Afrika. Wakati huo huo, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia anawaalika watanzania na wapenzi wa Lugha ya Kiswahili, kuungana na watanzania tarehe 9 Julai 2022 kuanzia asubuhi hadi “Lyamba lya Mfipa” kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani. Waswahili nchini Italia wanatakiwa kujipanga kisawasawa, kwani hii ndiyo Siku ile iliyokubalika!

Siku ya Kiswahili Duniani

 

 

06 July 2022, 14:42