Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA: Umuhimu wa Mawasiliano ya Jamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tanzania ni mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA uliofunguliwa rasmi Dominika tarehe 10 Julai 2022 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali John Njue, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Nairobi, Kenya na mahubiri kutolewa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam. Mkutano unanogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui na utajiri wake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ni kati ya wajumbe wa ngazi za juu kutoka Vatican wanaohudhuria mkutano wa AMECEA ambaye tarehe 11 Julai 2022 ametoa hotuba kwa wajumbe wanaohudhuria mkutano huu. Katika hotuba yake amejielekeza zaidi kuonesha umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, unavyoingiliana na mawasiliano, kwa ajili ya ujenzi wa ushirika, mahusiano na mwingiliano kati ya watu na mazingira.
Kimsingi Waraka “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni nyenzo ya nguvu katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na mawasililiano kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto za kiikolojia zinazomwandama mwanadamu. Katika Waraka huu wa Kitume, Baba Mtakatifu Francisko kwa muhtasari anagusia mambo yanayotokea katika mazingira; Umuhimu wa kuenzi Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa kiikolojia vinavyohusiana na watu pamoja na Ikolojia msingi. Baba Mtakatifu anagusia njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni umuhimu wa elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho. Inaweza kusemwa kwamba, matatizo na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo ni kutokana na tabia ya kujenga mbinu na malengo ya sayansi na teknolojia kama mfumo wa elimu ya ufahamu ambao unaunda maisha ya watu na shughuli za kijamii.
Kushinikiza mfumo huu katika maisha ya watu kuna madhara yake, jambo la msingi ni kukubali kwamba, bidhaa za kiteknolojia zina nguvu kwa sababu hujenga mfumo unaoidhibiti mitindo ya maisha na hivyo kutengeneza fursa katika jamii sanjari na mitazamo ya maslahi ya makundi fulani fulani yenye nguvu. Maamuzi ambayo yanaonekana kufaa kiuhalisia ni yale maamuzi kuhusu aina ya jamii tunayotaka kujenga. Rej Laudato si 107. Dr. Paolo Ruffini anasema, tasnia ya mawasiliano ya jamii inayo dhamana kubwa ya kuwakumbusha walimwengu mwingiliano uliopo kati ya hatima ya maisha ya mwanadamu na mazingira, ili kujenga kizazi kinachowajibika zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote badala ya kuzalisha walaji wa kupindukia. Mawasiliano yasaidie kuimarisha kanuni maadili za kiikolojia, kwa kuwajengea watu ufahamu wa kiikolojia kama unavyofundishwa na kufafanuliwa na Maandiko Matakatifu na Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kutambua mwingiliano uliopo ili kutenda kwa haki na busara. Watu wa Mungu wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini kwa kutambua kwamba, njia halisi ya ikolojia daima ni njia ya jamii inayopaswa kuunganisha masuala ya haki katika majadiliano mintarafu mazingira, ili kusikiliza kilio cha maskini na kilio cha Dunia mama.
Mawasiliano yanapaswa kuwa ni kiini cha majadiliano mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Vyombo vya mawasiliano ya jamii, viwasaidie watu kufikiri na kutenda kwa busara, hekima na upendo; viwe ni vyanzo vya maendeleo fungamani ya binadamu vinavyokazia mahusiano mema na adili; kwa kuwashirikisha watu elimu na ujenzi wa urafiki wa kibinadamu. Hii ndiyo dhima kubwa ya Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii. Maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Barani Afrika kunako mwaka 1994, yamekuwa ni chachu ya mawasiliano kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Huu umekuwa ni mwanzo wa kuanzisha njia mbalimbali za mawasiliano ya jamii, ambazo zinaendelea kujenga mahusiano ya karibu na Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kuchota na kurusha habari na matangazo mbalimbali yanayotolewa na Mama Kanisa kutoka mjini Vatican. Katika kipindi cha takribani miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Idhaa ya Kiingereza ya Radio Vatican na Miaka 30 ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, bila kusahau mchango unaotolewa pia kwa lugha nyingine zinazozungumzwa Barani Afrika, Radio Vatican imekuwa ni daraja linalounganisha watu wa Mungu Barani Afrika na Kanisa la Kiulimwengu, Baba Mtakatifu pamoja na Mabaraza mbalimbali ya Kipapa, katika ulimwengu wa mawasiliano ya jamii.
Ushirika huu unapaswa kunogeshwa zaidi na zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika amesema Dr. Paolo Ruffini. Taasisi mbalimbali za mawasiliano ya jamii zinazoendeshwa na kusimamiwa na Vatican, vinalenga kunogesha maboresho, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; kwa kutangaza na kushuhudia ukweli. Kanisa Barani Afrika, linaalikwa kuchangia pia habari za maisha na utume wa Makanisa mahalia, ili ziweze kufahamika na wengi. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kuwa na waandishi wa habari watakaoliwezesha Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii kutekeleza vyema dhamana na utume wake, kwa kutambua kwamba, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Huu ni mwaliko wa kujenga jukwaa litakaloweza kukusanya, kuchakata na hatimaye, kutangaza na kushirikisha, ukweli, wema na uzuri. Mawasiliano ya dhati yanafumbatwa katika ukweli na mahusiano, kwa kutambua nguvu na udhaifu wao kama ndugu wamoja, kwani wote wanategemeana na kukamilishana.