Tafuta

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu tarehe 11 Julai 2022 alipata nafasi ya kutembelea Kanisa la Parokia ya Mt. Yohane Bosco, Jimbo kuu la Dar es Salaam Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu tarehe 11 Julai 2022 alipata nafasi ya kutembelea Kanisa la Parokia ya Mt. Yohane Bosco, Jimbo kuu la Dar es Salaam  

Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA: Kardinali Tagle: Parokiani Kibaha

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle tarehe 11 Julai 2022 alipata nafasi ya kutembelea Kanisa la Parokia ya Mt. Yohane Bosco, Jimbo kuu la Dar es Salaam ambalo hivi karibuni lilitabarukiwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi katika mkesha wa Sikukuu ya Mtakatifu Yohane Bosco, Mlinzi na Mwombezi wa Parokia ya Kibaha, Jimbo kuu la Dar Es Salam tarehe 30 Januari 2022.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA, linaloundwa na Nchi 8 ambazo ni: Zambia, Malawi, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Eritrea, kuanzisia tarehe 10-18 Julai 2022 linaadhimisha mkutano wake mkuu wa 20 Jijini Dar es Salaam. Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji. Mkutano huu unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui na utajiri wake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote ndiyo mada kuu inayoongoza mkutano wa AMECEA kwa mwaka 2022. AMECEA inasema, Mambo makuu matatu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Anahimiza umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anitaka jamii kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa.

Mababa wa AMECEA wamepata nafasi kushuhudia uhai wa Kanisa la Tanzania
Mababa wa AMECEA wamepata nafasi kushuhudia uhai wa Kanisa la Tanzania

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote"  anapembua kwa kina mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiikolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya mafao ya watu wote duniani. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumatatu tarehe 11 Julai 2022 alipata nafasi ya kutembelea Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yohane Bosco, Jimbo kuu la Dar es Salaam ambalo hivi karibuni lilitabarukiwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam katika mkesha wa Sikukuu ya Mtakatifu Yohane Bosco, Mlinzi na Mwombezi wa Parokia ya Kibaha, Jimbo kuu la Dar Es Salam tarehe 30 Januari 2022.  Kardinali Tagle katika hija hii ya kichungaji alikuwa ameandamana na Maaskofu wakuu kutoka Jimbo kuu la Khartoum, Sudan Kongwe na Jimbo kuu la Lusaka, Zambia na mwenyeji wao alikuwa ni Askofu mkuu Ruwaichi. Padre Beno Kikudo aliwatembeza wageni wa Parokia ili kujionea maendeleo ya Parokia sanjari na ujenzi wa nyumba ya Mapadre! Waswahili husema, nyota njema......! 

Waamini watambue na kukumbuka kwamba, Kristo Yesu ndiye Jiwe kuu la pembeni na kila mwamini anapaswa kujengeka na kuwa ni jiwe hai, ili waamini wote waweze kutembea kwa pamoja katika umoja, ushirika na utume, kama sehemu ya mchakato wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Bila uwepo wa Kristo Yesu kati yao, Kanisa kama Jengo litageuka na kuwa ni uwanja wa fujo, “patashika nguo kuchanika” aliwahi kusema Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, ambaye anawataka waamini kuwa mawe hai katika Kanisa kwa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha, kwa kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayezungumza pamoja nao kutoka katika undani wa nyoyo zao, yaani dhamiri nyofu. Mababa wa AMECEA katika mkutano wao wa 20 Jijini Dar es Salaam, wanaendelea kukazia umuhimu wa majiundo ya dhamiri adilifu, kanuni maadili na utu wema ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni mwaliko wa kutafuta na kutibu mambo yanayopelekea uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote.

Mababa wa AMECEA wanakazia ujenzi wa dhamiri adilifu, kanuni maadili na utu wema
Mababa wa AMECEA wanakazia ujenzi wa dhamiri adilifu, kanuni maadili na utu wema

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha upendo wa udugu kwa jirani, ili kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, utunzaji bora wa mazingira ni chachu ya amani na utulivu. Uchafuzi wa mazingira unasababishwa na uchu wa mali, madaraka na tabia ya kutaka kuwatala na kuwakandamiza wengine. Ikumbukwe kwamba, utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anapenda kuwaalika Mababa wa AMECEA kufanya tafakari ya kina kuhusu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Hizi ni nyaraka mbili muhimu zinazofungamanishwa na maendeleo fungamani pamoja na udugu wa kibinadamu. Lengo ni kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kupambana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika ulimwengu mamboleo kama ilivyo kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Utunzaji bora wa mazingira uzingatie pia haki jamii, utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” katika Sura ya nne anasema kwamba, mazingira ni chanda na pete na mafao ya wengi na kwamba, hii ni sehemu ya haki kwani mwanadamu ana mwingiliano wa pekee na mazingira na kwamba, hii ni sehemu inayozunguka maisha yake. Athari za mazingira na maisha ya kijamii zinakwenda sawa sawa na wala haziwezi kutenganishwa, kumbe hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha urafiki wa kiraia na mshikamano kati ya vizazi na vizazi ili kulinda na kutunza mazingira. Utunzaji mkamilifu ni sehemu ya mafao ya wengi, changamoto ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anasema kuna haja pia ya kuhakikisha kwamba, Jamii inalinda na kudumisha utajiri wa tamaduni za binadamu kama vile za jamii ya Waborigini na mazingira ya mijini, ili kufanya maboresho ya maisha ya binadamu, kwa kuheshimu pia maeneo ya wazi, makazi ya watu na usafiri mijini mambo ambayo wakati mwingine yanaathari kubwa kwa maisha ya watu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, mwili wa mwanadamu unathaminiwa kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kuipokea dunia kama nyumba ya wote na hivyo kushinda kishawishi cha mantiki ya kutawala.

Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa kimaadili na kiutu
Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa kimaadili na kiutu

Wakati huo huo, Askofu Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu tamaduni za watu na mazingira anawasihi watu wa Mungu Afrika Mashariki na Kati kuheshimu mila na tamaduni njema kama njia ya kuenzi kazi ya uumbaji na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

AMECEA Tagle

 

14 July 2022, 16:10