Utoaji Mimba Ni Kinyume Cha Haki Msingi, Utu na Heshima ya Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Utoaji mimba si sehemu ya haki msingi za binadamu bali ni kwenda kinyume cha Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mwelekeo wa jamii kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha uhuru wa wanawake kuamua wanavyotaka kuhusiana na miili yao! Kanisa linasema ni vigumu kuonesha kwamba, utoaji mimba ni sehemu ya haki msingi za binadamu wakati unapelekea mauaji ya kiumbe kisichokuwa na hatia. Harakati za kutaka kukuza na kudumisha uhuru na usawa kati ya wanawake na wanaume ni mambo mazuri katika jamii, lakini usawa unaotoa fursa na haki ya mtu kushiriki katika mauaji ya watoto wasiokuwa na hatia hapa ni kwenda kinyume kabisa cha: Utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kuwasababishia mateso na mahangaiko makubwa wanawake wanaoshiriki katika zoezi la utoaji mimba. Kuna kundi kubwa la wanawake linaloendelea kuteseka kisaokolojia kwa vile waliwahi kushiriki katika zoezi la utoaji mimba, lakini ni mateso na mahangaiko ambayo hayazungumziwi. Uhuru ni jambo jema sana katika kukuza na kuendeleza mahusiano kati ya mwanaume na mwanamke, wanaotambua dhamana na wajibu wao unaowashirikisha katika kazi ya uumbaji.
Huu ni uhuru unaowajibisha na kuhamasisha majadiliano ya kina. Kumbe, kuna haja ya kimaadili na kiutu kwa jamii kuangalia kwa makini kwamba, mimba isionekane kuwa ni jambo ambalo halitakiwi na inaweza kunyofolewa wakati wowote ule, kwani mtoto aliyeko tumbani mwa mama yake ana haki ya kuzaliwa, kukua na kukomaa hadi mauti yatakapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ni katika muktadha huu, Vatican inaungana na wapenda amani duniani, kuunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu ya Marekani uliobatilisha maamuzi ya Kesi ya Roe V. Wade iliyohalalisha Sheria ya Utoaji Mimba kwa Takribani miaka 50 iliyopita. Hii ni sheria iliyopitishwa kunako mwaka 1973 ikiwaruhusu wanawake wenye ujauzito katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza, nchini Marekani kuweza kunyofoa mimba. Uamuzi huu mpya unatoa haki kwa Majimbo nchini Marekani kubatilisha sheria hiyo ambayo imedumu kwa takribani miaka 50 kwa kisingizio cha uhuru wa wanawake kuhusiana na miili yao.
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, linasema, kwa sasa hiki ni kipindi cha kuganga na kuponya madonda yaliyojitokeza baada ya kupitisha Sheria ya Utoaji Mimba nchini Marekani. Ni fursa ya kutafakari, ili hatimaye, kujenga umoja, upendo na mshikamano wa kijamii; kwa kuweka sera na mikakati itakayosaidia kuwajengea wanafamilia uwezo wa kiuchumi ili kukabiliana kikamilifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia. Wanawake wapewe fursa za kiuchumi ili waweze kujitegemea na hatimaye, kuwalea Watoto wao kwa upendo. Huu ni wakati muafaka wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia hazina budi kulindwa, kudumishwa na hatimaye, kurithishwa ndani ya jamii.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na waandishi wa habari waliokuwa kwenye hija yake ya kitume nchini Hungaria na Slovakia mwezi Septemba 2021 alisema kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kama waamini wanaitwa na kuhamasishwa kulinda, kuitunza na kuidumisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango na mapenzi ya Mungu, hata pale watu wanapokumbana na magonjwa pamoja na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Hakuna mwenye haki ya “kufyekelea mbali zawadi ya maisha ya binadamu”. Kutoa mimba ni mauaji. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, uhai wa binadamu unaheshimiwa na kuthaminiwa na kwa njia hii, kuweza kutangaza na kushuhudi tunu msingi za maisha ya Kikristo katika mazingira ya kifamilia. Kila huduma ya matibabu inayotolewa kwa mgonjwa iwe ni chemchemi ya huruma na upendo kwa wagonjwa wanaoteseka. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya afya ya mwanadamu yanapaswa kuwa kweli ni chombo cha huduma kwa wagonjwa na wala si vinginevyo.
Kamwe mgonjwa asionekane kuwa ni mzigo mzito, kiasi cha kuanza kuhalalisha kisheria mchakato wa kifolaini. Kwa haraka haraka anasema Baba Mtakatifu, jambo hili linaweza kuonekana kuwa kama sehemu ya uhuru wa mtu binafsi; lakini ndani mwake, uhuru huu unafumbata ubinafsi unao thubutu kupima: haki, heshima na utu wa mtu kutokana na umuhimu wake. Kifolaini hakimsaidii mtu kumpunguzia maumivu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, umefika wakati wa kusimama kidete kupinga utamaduni na utandawazi usiojali utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utoaji mimba, kifo laini na adhabu ya kifo ni mauaji yanayokwenda kinyume cha haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Kwa zile nchi ambazo zimetunga Sheria ya kutoa mimba, zimejikuta zikiwa na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa na matokeo yake ni watu wenye umri mkubwa kuongezeka maradufu! Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Kanisa kujikita katika shughuli za kichungaji na wala si kuwahukumu wanasiasa wanaojihusisha na utamaduni wa kifo. Kanisa lijitahidi kujenga ujirani mwema, kwa kuwaendea kwa huruma na upole.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu Vincenzo Paglia, Rais Taasisi ya Kipapa ya Maisha anasikitika kusema kwamba, nchi za Magharibi zinaanza kupotesha ari na mwako wa Injili ya uhai, changamoto na mwaliko kwa jamii kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha, utu, na heshima ya binadamu. Lengo ni kuambata na kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kuwajibika kikamilifu kwani leo na kesho ya mwanadamu viko mashakani sana.