Tafuta

Ratiba ya Papa kwa Mwezi Juni na Julai Ratiba ya Papa kwa Mwezi Juni na Julai 

Ratiba ya Papa kwa mwezi Juni na Julai 2022

Ratiba ya mikutano ijayo ya Papa imechapishwa:miongoni mwa shughuli za mwezi huu ni Mkutano wa X wa Familia duniani,mwezi Julai ni ziara za kitume katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini na baadaye nchini Canada.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Ofisi ya Waandishi wa Habari Vatican imetangaziwa kuhusu maadhimisho ambayo Baba Mtakatifu Francisko atafanya katika mwezi wa  Juni na Julai.  Papa Francisko atakuwepo katika Mkutano wa X wa Familia Duniani utakaofanyika mjini Roma kuanzia tarehe 22 hadi 26 Juni 2022 na ambapo wajumbe wa Mabaraza ya Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za dunia na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa zinazohusika na uchungaji wa Kanisa watashiriki na familia nyingi kushiriki. Tamasha la Familia na Kongamano la Kitaalimungu-Kichungaji litafanyika katika ukumbi wa Paulo VI. Tarehe 25 Juni, saa 11.15 jioni, Papa Francisko ataadhimisha Misa Takatifu katika uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican.

Tarehe 29 Juni 2022, ni maadhimisho ya Watakatifu Petro na Paulo, wasimamizi wa  Roma, ambapo Papa Francisko ataongoza  saa 3.30, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Misa na kubariki Pali, ambazo zitawekwa kama ishara ya ushirika na Askofu wa Roma juu ya Maaskofu wakuu wapya wa miji mikuu.

Ziara barani Afrika na Canada

Mwezi Julai Papa atakabiliana  na ziara mbili za kitume, mwanzoni na mwisho wa mwezi. Kuanzia tarehe 2 hadi 7 atasafiri kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini. Hii itakuwa ni ziara ya 37 ya Kitume ambayo Papa Francisko atatembelea miji mitatu: Kinshasa, Goma na Juba na kukutana na mamlaka ya kiraia na kikanisa, vijana, watu waliokimbia makazi, waathirika wa ghasia. Hatimaye, kuanzia tarehe 24 hadi 30 Julai 2022, Papa  Francisko atakuwa tena  nchini  Canada akitekeleza azma aliyoitoa mara kadhaa ya kufikia nchi hiyo ambapo Kanisa linajishughulisha na mchakato muhimu wa upatanisho na wazawalia yaani watu wa Asilia. Kulingana na ajenda ya usafiri, Papa atasimama Edmonton, Québec na Iqaluit.

04 June 2022, 16:30