Tafuta

Mkutano wa X wa Familia duniani Mkutano wa X wa Familia duniani 

Kard.De Donatis:Mioyo ya familia imejeruhiwa na majaribu ya historia na dunia

Kardinali De Donatis,Makamu wa Papa kwa Jimbo la Roma ameongoza Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kwa ajili ya Washiriki wa Mkutano wa X wa Familia duniani unaonedelea jijini Vatican hadi 26 Juni.“Moyo wa Mchungaji hudunda kwa furaha ndani ya nyumba iliyojaa marafiki.Nyumba za wanaume na wanawake wa sasa,sio nyumba za siku kuu kila wakati.Mara nyingi ni sehemu za mgawanyiko na vurugu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Ijumaa tarehe 24 Juni, Kardinali Angelo de Donatis, Makamu wa Papa kwa Jimbo la Roma ameongoza Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kwa ajili ya Washiriki wa Mkutano wa X wa Familia duniani unaonedelea jijini Vatican hadi 26 Juni 2022. Katika mahubiri yake amesema, katika siku hii ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, siku  inaanza na furaha kubwa ya uwepo hapo kutoka sehemu mbali mbali za dunia kama vile zizi lililozunguka Mchungaji wake. Kardinali amebainisha jinsi ambavyo katika maandaki (Catacombs) ya kizamani yaliyo jaa jiji la Roma, walikuta alama za Kikristo, miongoni mwake ni maandishi na picha za kizamani. Katika kazi hizo picha ya Mchungaji inajitokeza, sura ambayo iliunganishwa na mifano iliyopo ya sanaa ya Kirumi. Ingawa kwa Warumi mchungaji kwa ujumla alikuwa kielelezo cha ndoto ya maisha ya amani na rahisi, ambayo watu katika machafuko ya jiji kubwa walitamani na kwa Wakristo picha hiyo ina maudhui ya kina.

Washiriki wa Mkutano wa X wa Familia duniani jijini Vatican
Washiriki wa Mkutano wa X wa Familia duniani jijini Vatican

Kardinali de Donatis amesema: “Mchungaji wa kweli ndiye anayejua pia njia ipitayo katika bonde la giza; yeye ndiye ambaye, hata kwenye barabara ya upweke wa mwisho, hutembea nasi, akituongoza na kutuvusha. Yeye mwenyewe aliitembea njia hiyo, hadi kufa kwake, akashinda na akarudi kutusindikiza sasa na kutupatia uhakika kwamba, pamoja naye, daima mapito yanapatikana”. Akiendelea Kardinali De Donatis  amesema picha hii inajaza mwanga zaidi kwa Mkutano wa X wa Familia Duniani wa Familia. Na katika siku kuu ya Moyo wa Kristo Mchungaji Mwema, mioyo ya ulimwengu wote inadunda, ina furaha kwa sababu wamejibu ‘Ndiyo’ kwa Mungu; ni mioyo iliyojeruhiwa na majaribu ya historia na dunia; ni mioyo iliyofunguka kwa upya wa Injili, ili kutoa ushuhuda wa uwepo wa daima wa Kristo Bwana-arusi katika historia yetu. Sio kweli kwamba familia kwa sasa imepotea, na kumalizika. Bado iko juu ya mabega ya Mchungaji ambaye kwa nguvu na huruma huvuka njia za ulimwengu na anatuita kugundua tena njia ya utakatifu.

Washiriki wa Mkutano wa X wa Familia duniani jijini Vatican
Washiriki wa Mkutano wa X wa Familia duniani jijini Vatican

Mfano wa Mchungaji unahitimishwa kwa karamu nyumbani kwake. Ni vyema kutambua mwelekeo huu wa ndani ambao kondoo hupata amani. Moyo wa Mchungaji hudunda kwa furaha ndani ya nyumba iliyojaa marafiki. Nyumba za wanaume na wanawake wa sasa, sio nyumba za siku kuu kila wakati. Mara nyingi ni sehemu za mgawanyiko, za ukimya, za wasiwasi, na  kwa bahati mbaya pia za vurugu. Badala ya kuwa makao ya amani, mara nyingi huwa kiota cha kujifungia ili kujilinda kutoka kwa wengine au hata kutoka kwa washiriki wa familia ya wenyewe binafsi. Ni mara ngapi, hata kuanzia kwa njia bora zaidi, baadhi ya wanandoa na familia wamejikuta wakiwa wageni majumbani mwao, kama mwili ambao moyo haupo tena, ambainisha Kardinali De Donatis. Kama  Wakristo haipaswi kuwa hivyo. Ikiwa imeeingiza katika nyumba kubwa zaidi ya Kanisa, ulimwengu unaweza kupata katika nyumba zetu siku kuu kwa  wale wanaoishi Furaha ya Upendo. Kwa  maana hiyo ni muhimu kuwa  na moyo kwa kuiga moyo wa Kristo. Ni kwa njia hiyo tu ndipo familia itakuwa Kanisa zaidi na Kanisa litakuwa familia zaidi. Ndipo mioyo yetu itakuwa kama bahari, ambapo Upendo unamiminwa bila kipimo, shukrani kwa Roho Mtakatifu ambaye anakuja kugusa mambo ya ndani ya mwanadamu na kumfanya amelemete kama kioo. Familia inayopokea upendo huo unaofurika kama zawadi inaweza kuwabadilisha na kuwabadilisha wale ambao, kwa Furaha ya Upendo (Amoris Laetitiae),  wanabaki wameambukizwa nayo.

Tazama mimi hapa kwa ajili ya kufungulia milango Bwana

Kardinalo De Donati, amependa kumshukuru Bwana pamoja nao na kwa ajili yao kwa uchangamfu wa familia ya Kikristo, kwa ajili ya mashuhuda wengi wajasiri na wenye furaha waliotawanyika ulimwenguni kote, ambao hutoa uhai na kuupatia ulimwengu uhai, wakirudia kusema ile “Ndiyo” pamoja na mambo yao yote kwa mioyo. Sio “Ndiyo” inayojumuisha maneno au hali ambazo zimezuiliwa kwa muda mfupi maishani. Hiyo ni Ndiyo  tazama mimi hapa” ya kila siku, inayojumuisha kuamka asubuhi kwenda kazini na kuwatayarisha watoto shuleni; ya kufanya ziara kwa madaktari, mahali ambapo sisi tunapeleka  wazee wetu; iliyofanywa na harufu ya kupika na ukimya wa huzuni; inayotengenezwa na utulivu wa jioni na usiku kucha bila usingizi, ; iliyotengenezwa na ndoto na matamanio, wasiwasi na shauku, kicheko na machozi, maisha na kifo. Ni moyo wa mama yangu, baba yangu, kaka na dada zangu, wanangu na binti zangu.

"Tumwombe Bwana kwamba Moyo wake uchukue mwelekeo katika nyumba zetu". ‘Ndiyo, tazama mimi hapa’  tunaitaka kwa kumfungulia milango yetu na tutagundua kwa upya sala ya familia, hata katika urahisi wa ishara ndogo za kila siku; tutajifungulia kwa jumuiya, kutoa ushuhuda wa upendo wa Mungu; tutakimbia ugumu wa moyo uliogandamana, ambao uthibitishwa tunapogeukia kwenye nafasi zetu na kuepuka kusikiliza, kuzungumza na kusamehe”. Kardinali De Donatis kwa kuhitimisha mahubiri yake amesema “Tutaelewa kwamba utakatifu sio lengo lisiloweza kufikiwa, wakati milango iliyofunguliwa ya nyumba zetu, kufanya siku kuu na marafiki, itatusaidia kwenda nje kusikiliza familia nyingine au wale ambao hawana au hawana tena familia. Kama mchungaji tutakwenda kuwatafuta wanaume na wanawake wa wakati wetu, si kwa macho ya kuhukumu na kuchambua, bali kwa moyo unaokaribia na kutembea pamoja nao, kwa moyo unaoona taabu ili kuona uzuri wa Huruma”.

24 June 2022, 15:52