Askofu Mkuu Gallagher huko Makedonia Kaskazini kwa ajili ya Jukwa la Prespa 2022
Vatican News
Katibu wa Vatican wa Mahusiano na ushirikiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa, Askofu Mkuu Gallagher Jumatano kupitia tweet yake alitangaza juu ya safari ya kwenda Makedonia Kaskazini kuanzia tarehe 16-19 Juni 2022 ili kushiriki sehemu ya Majadiliano ya Jukwaa la Prespa 2022, linalofanyika katika jiji la Ohrid.
Tukio hilo linashuhudia viongozi wa kisiasa wakijadili mustakabali wa Balkan Magharibi kabla ya mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) huko Brussels kuanzia tarehe 23 Juni 2022 juu ya mada hiyo hiyo. Viongozi wamejipanga kuzingatia mustakabali wa eneo hilo kuhusiana na hali ya sasa ya usalama ya Ulaya. Hata hivyo hivi karibuni mnano tarehe 25 Mei 2022, Bwana Dimitar Kovačevski Waziri Mkuu wa Makedonia ya kaskazini alitembelea Vatican na kufanya mkutano na Papa.
Askofu Mkuu Gallagher pia ataadhimisha Misa katika Kanisa Kuu la Skopje, ambalo Papa Francisko alitembelea mnamo Mei 2019. Wakati wa ziara hiyo ya Kitume, Papa alisali pia katika ukumbusho wa Mama Teresa, aliyezaliwa katika mji mkuu wa Albania mnamo mwaka 1910, na kushiriki katika mkutano wa kiekumene na wa kidini na vijana.