Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama, Tanzania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kigoma, kuwa ni Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kahama lililoko nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko alikuwa ni Makamu wa Askofu Jimbo Katoliki la Kigoma na Katibu mtendaji, Idara ya Kichungaji Jimbo Katoliki la Kigoma. Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko alizaliwa tarehe 25 Machi 1970 huko Kalinzi, Jimbo Katoliki la Kigoma. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi kutoka Seminari Ndogo ya Katoke kati ya mwaka 1986 hadi mwaka 1993; Seminari Ndogo ya Ujiji kati ya Mwaka 1993 hadi mwaka 1994. Aliendelea na masomo ya Falsafa, Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, kati ya Mwaka 1994 hadi mwaka 1996. Baadaye aliendelea na masomo ya Taalimungu, Seminari kuu la Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam kati ya mwaka 1996 hadi mwaka 1999. Kati ya Mwaka 1999 hadi mwaka 2000 alifanya mazoezi ya shughuli za kichungaji Seminari Ndogo ya Ujiji.
Hatimaye, tarehe 5 Julai 2001 akapewa Daraja takatifu ya Upadre kwa Jimbo Katoliki la Kigoma. Baada ya Upadrisho, amewahi kuhudumu kama: Paroko-usu Parokia ya Kasulu, Jimbo Katoliki la Kigoma, Mwalimu na Mlezi, Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora. Kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2008 alitumwa na Jimbo Katoliki la Kigoma, kwenda nchini Italia kujiendeleza zaidi kwa masomo na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Taalimungu Maadili. Alibahatika pia kufanya utume wake wa Kipadre katika Parokia ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, Jimbo Katoliki la Catania kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2008. Baada ya kurejea nchini Tanzania, alitumwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kufundisha Seminari Kuu la Kipalapala, Jimbo Kuu la Tabora.
Askofu mteule Christopher Ndizeye Nkoronko, amewahi pia kuwa Mkurugenzi wa Utume wa Walei, Jimbo Katoliki Kigoma, Paroko wa Parokia ya Kibondo, Dekano wa Dekania ya Kibondo na Rais wa Umoja wa Mapadre Wazalendo, Jimbo Katoliki la Kigoma. Kati ya Mwaka 2015 hadi mwaka 2016 alikuwa ni Katibu mkuu msaidizi wa UMAWATA, Taifa. Kati ya Mwaka 2016 hadi mwaka 2019 alikuwa Paroko wa Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Kigoma. Tangu mwaka 2011 aliteuliwa hadi wakati huu, amekuwa ni Mratibu wa UFATA, "Tanzania Family Strengthening" na Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa, PMS Jimbo Katoliki la Kigoma. Tangu mwaka 2016 hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Kigoma na Katibu mtendaji wa Idara ya Kichungaji Jimbo Katoliki la Kigoma.