Tafuta

Ikumbukwe kwamba, njia za asili za mawasiliano zitaendelea kutumika sanjari na mabadiliko makubwa ya teknolojia kwa njia ya kidigitali. Ikumbukwe kwamba, njia za asili za mawasiliano zitaendelea kutumika sanjari na mabadiliko makubwa ya teknolojia kwa njia ya kidigitali.  

Wadau Wa Tasnia ya Mawasiliano Iweni Vyombo na Mashuhuda wa Mafungamano Kijamii

Paolo Ruffini amekazia umuhimu wa waamini kuimarisha mitandao ya kijumuiya pamoja na kuendelea kuwa karibu na wasikilizaji na wasomaji wa njia za mawasiliano ya kidigitali, kwa kusoma alama za nyakati sanjari na kutambua lugha ya wasogozi wa mitandaoni. Njia za asili za mawasiliano zitaendelea kutumika sanjari na mabadiliko makubwa ya teknolojia kwa njia ya kidigitali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwa: ni wahudumu na vyombo vya ukweli, wema na uzuri, kwa kusimama kidete kutetea kile kilicho chema, kizuri na kitakatifu, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu. Mawasiliano ya jamii iwe ni chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu, ili kuganga na kuponya madonda yaliyosababishwa na habari potofu. Wadau wa tasnia ya mawasiliano wanapaswa kuendeleza kipaji cha ubunifu ili kuwaondoa watu jangwani na hivyo kuanzisha mchakato wa mawasiliano mubashara unaojenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Huu ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati, ili kuibua na kuendeleza maisha mapya. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni muda wa kujenga na kudumisha ujasiri unaofumbwatwa katika misingi ya ukarimu, udugu wa kibinadamu na mshikamano. Mtandao wa mawasiliano ya jamii hauna budi kuendelezwa katika ulimwengu wa utandawazi pamoja na kuzingatia mahitaji ya jamii mahalia. Huu ni mfumo wa kidigitali na unaozingatia ukweli, ili kuwaunganisha watu katika medani mbalimbali za maisha na kamwe si kuwatenganisha na kuwasambaratisha.

Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wawe ni mashuhuda wa mafungamano.
Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wawe ni mashuhuda wa mafungamano.

Maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii hayana budi kuwa na mwelekeo wenye mafao mapana zaidi kwa watu wote. Huu ni wakati wa kujikita katika mawasiliano dhidi ya virusi vya ubinafsi na uchoyo, ili kudumisha: umoja, mshikamano, ukweli na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana. Mahusiano na mafungamano yamwilishwe katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kujenga uchumi shirikishi, unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu. Watu wadumishe ushirikiano unaosimikwa katika tunu msingi za maisha ya kiutu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Wadau wa tasnia ya mawasiliano wanapaswa kujisadaka kwa kutoa muda wao, ujuzi, weledi, rasilimali fedha na sala zao. Ni wajibu na dhamana ya Kanisa kutoka kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Mama Kanisa hana budi kuhakikisha kwamba, anatumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mungu.

Gazeti la "Voz da Fatima" Linaadhimisha Miaka 100 ya huduma kwa watu wa Mungu
Gazeti la "Voz da Fatima" Linaadhimisha Miaka 100 ya huduma kwa watu wa Mungu

Vyombo vya mawasiliano ya jamii visaidie watu kugawana mambo ya kidunia, kufahamu yanayoendelea kujiri sehemu mbalimbali za dunia, lakini zaidi, viwe ni chemchemi ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano hivi karibuni ameshiriki katika kongamano la mawasiliano ya jamii, lililoandaliwa na Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Ujenzi wa Mitandao ya Kijamii Katika Mapinduzi ya Kidigitali Kwenye Tasnia ya Mawasiliano.” Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa waamini kujenga na kuimarisha mitandao ya kijumuiya pamoja na kuendelea kuwa karibu na wasikilizaji na wasomaji wa njia za mawasiliano ya kidigitali, kwa kusoma alama za nyakati sanjari na kutambua lugha ya wasogozi wa mitandaoni. Lakini, ikumbukwe kwamba, njia za asili za mawasiliano zitaendelea kutumika sanjari na mabadiliko makubwa ya teknolojia kwa njia ya kidigitali.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waandishi wa habari katika vyombo vya Kanisa wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa sera na mikakati inayowakutanisha na kuwafungamanisha watu. Kimsingi wawe ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ili kuondokana na utamaduni wa kifo. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kuanzia tarehe 1-6 Agosti 2023 huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno, iwe ni fursa ya kuwekeza katika mawasiliano yanayojikita katika matendo, mahusiano na mafungamano ya kijamii, daima mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Mwaka 2022 Gazeti la “Voz da Fatima” linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Kwa miaka yote hii, limekuwa ni rejea kwa maadhimisho mbalimbali yanayoendeshwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima. Changamoto ni kuwekeza katika mawasiliano ya jamii yanayojenga ujirani mwema, ili kukabiliana na changamoto mambo leo.

Ruffini Fatima
04 May 2022, 14:47