Kardinali Parolin:kukarabatiwa kwa kambi itawezesha Walinzi wa Uswiss kutekeleza vema utume wao
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kambi ya Walinzi wa Uswiss iliyoko Vacan ni jengo la thamani na ya kihistoria, iliyoanzishwa kwa upapa wa Pio IX (1846-1878) na Pio XI (1922-1939. Pia ni mahali pa Urithi wa Dunia wa UNESCO. Jengo hilo linafanyiwa ukarabati ili kuhakikisha faraja kubwa zaidi kwa wajumbe na familia za jeshi ndogo zaidi duniani. Kutokana na hiilo Jumatano asubuhi, tarehe 4 Mei 2022, katika Ukumbi wa Mikataba kwenye Jumba la Kitume, Mkataba wa Maelewano uliokuwa umetangazwa kati ya Sekretarieti ya Vatican na “Mfuko wa Ukarabati wa kambi ya Walinzi wa Uswiss wa Papa jijini Vatican umetiwa saini. Kardinali, Pietro Parolin, Katibu wa Vatican alitia saini katika hati hiyo. Kwa upande wa Vatican waloikuwepo kwa ajili ya kutia saini kisheria ni pamoja na Katibu msaidizi wa Vatican, Sr. Raffaella Petrini, Monsinyo Luigi Roberto Cona, Afisa wa Masuala Makuu ya Sekretarieti ya Vatican, na Dk. Fabio Gasperini, Katibu Mkuu wa APSA. Na kwa upande wa wawakilishi wa Mfuko wa Ukarabati, walikuwa Bwana Jean-Pierre Roth na Bwana Stephan Kuhn, wote wawili wakiwa Rais na Makamu Rais; Mheshimiwa Denis Knobel, Balozi wa Shirikisho la Uswiss anayewakilisha nchi yake Vatican, na Kanali Christoph Graf, Kamanda wa Walinzi wa Uswiss.
Hati hiyo ilitiwa saini katika muktadha wa sherehe za kuapishwa kwa wajaeshi wapya 36 zilizopangwa kufanyika katika uwanja wa Mtakatifu Damasus mnamo tarehe 6 Mei siku ambayo inakumbusha walinzi 147 waliokufa wakati wa wa vita jijini Roma wakimlinda Papa Clement VII. Na kuanza kwa kazi kwenye kambi hizo kutafanyika mwishoni mwa maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025. Dk Massimiliano Menichetti, mkuu Radio Vatican/Vatican News, amefanya mahojiano na Kardinali Parolin jinsi ulivyofanyika utiaji wa saini hiyo. Kutiwa saini kwa protokali hiyo kunawakilisha hatua muhimu ya njia iliyofanywa mwishoni mwa 2016, inayolenga kuboresha mali zinazounda kambi za sasa, ili kuzirekebisha kulingana na viwango vipya vya makazi na pia kulingana na vigezo vya ikolojia. Kwa ajili hiyo, Mfuko ulianzishwa nchini Uswiss ambao, kwa makubaliano na Mamlaka ya Vatican, iliwasilisha mpango wa awali kwa Baba Mtakatifu mnamo Oktoba 2020. Janga la uviko kwa namna moja lilitoa muda wa ziada wa kutafakari zaidi. Hivyo iliamuliwa kuwa itakuwa vigumu kufikiria kuanza kazi kabla ya Jubilei ya 2025. Wakati huo huo, uamuzi ulichukuliwa ili kufafanua zaidi mpango wa awali kwa kuzingatia vikwazo vya kihistoria, kisanii na mazingira ambayo Kambi hiyo inakabiliwa, bila kupuuza wajibu unaotokana na Vatiocn kujumuishwa kwa Jiji la Vatican katika Orodha ya Urithi wa Dunia wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Syansi na utamaduni(UNESCO).
Je, Mkataba wa Maelewano una thamani gani?
Mkataba wa Maelewano ni tamko la nia inayolenga kuelekeza kwa uwazi hatua zinazopaswa kuchukuliwa baadae. Mtu anaweza kusema kwamba saini ya leo inajumuisha kuanza tena kiukweli na sahihi baada ya kusimama kutokana na UVIKO na uamuzi wa kuweka Sheria hii katika muktadha wa maadhimisho ya kiapo cha Walinzi wapya wa Uswizi kunaonesha, kwa njia thabiti sana, ni kiasi gani tunajali kuhusu Jeshi la Walinzi wa Uswisi na huduma adhimu ambayo imekuwa ikiifanywa kwa takriban miaka 500 ya kumlinda Baba Mtakatifu.
Mji mzima wa Vatican umekuwa sehemu ya Urithi wa Dunia wa UNESCO tangu 1984 na kuna viunga vingi vya kihistoria na kisanaa. Je! ni hatua gani zinazofuata?
Kwanza kabisa, tutajitoa katika kukamilisha mpango wa awali. Hii ni muhimu kwa sababu ya thamani ya kihistoria ya kambi za sasa, ambazo majengo yake ni ya Upapa wa Pio IX na Pio XI. Kwa maana hii, kipengele muhimu kitakuwa uhifadhi wa sura zake za nje, pamoja na kizuizi cha urefu kilichowekwa na Misingi ya Bernini. Sehemu nyingine inawakilishwa na hitaji la kulinda na kuimarisha minara muhimu inayozunguka. Hapa ninarejea hasa ‘Passetto’ huko Borgo na ‘Porta Sancti Petri’, yaani ‘Mlango Mtakatifu wa Petro’ na muonekano wa kiakiolojia wa Kirumi kwenye msingi wa kambi ya chini ya ardhi. Hata kama 2026 inaonekana kuwa mbali sana, lakini hatua zinazopaswa kuchukuliwa zinahitaji ramani ya barabara ambayo itabidi ijumuishe idhini ya mpango wa mwisho na kwa kuzingatia sheria ya wazi ya Vatican na Kanuni za Mikataba, utoaji wa kazi na ufunguzi wa site ya jengo na matokeo ya uhamisho wa muda kwa Walinzi.
Je, gharama za ukarabati wa kambi hiyo zitalipwa na wafadhili?
Ndio, uungwaji mkono wa watu wa Uswiss kwa mpango mpya wa kambi hadi sasa umekuwa na sifa ya ukarimu mkubwa. Kufikia sasa, kiasi kikubwa cha pesa kilichotolewa na Mfuko kimehifadhiwa kwa njia ya zawadi na ahadi za mikataba za michango. Vatican inashukuru Baraza la Shirikisho la Uswiss, Cantons, jumuiya za kikanisa pamoja na mifuko mingi na wafadhili wa kibinafsi kwa kujitolea kwao. Shukrani zetu pia zinawaendea wale wote waliofanya kazi na wataendelea kufanya kazi ili kuhamasisha kampeni ya uchangishaji fedha, tukijua kwamba jitihada hii itawezesha kuwapatia Walinzi, familia zake na wale wote wanaoisaidia hali bora ya makazi kwa ajili ya kutekeleza utume wao tukufu.
Ukarabati wa Kambi ni jambo la lazima, anasisitiza rais wa Mfuko huo Bwana , Jean-Pierre Roth. “Majengo makuu ya Kambi hayatoi nafasi ya kutosha kwa walinzi na familia zao na yana gharama kubwa za matengenezo. Yanahitaji ukarabati mkubwa ili kukidhi mahitaji ya walinzi na viwango vya sasa vya mazingira. Mpango huu ni muhimu ili kudumisha usalama bora, kwa ajili ya huduma kwa Baba Mtakatifu na Ikulu ya Kitume.
Wazo la kukarabati kambi ya Walinzi ilianza kutimia mnamo 2017-2018 wakati Mfuko huo ulipotia saini na kampuni ya uhandisi ya Schnetzer-Puskas kuchunguza hali ya majengo ya sasa. Mnamo 2019-2020, Mfuko huo uliamuru kampuni ya usanifu ya Durisch&Nolli ya Massagno kuandaa mpango huo, ambao ulifadhiliwa pamoja na Sekretarieti ya Vatican. Mnamo tarehe 2 Oktoba 2020, mapngo wa awali uliwasilishwa kwa Papa na kuwasilishwa kwa Sekretarieti ya Vatican, kama ishara ya kuadhimisha Miaka 100 ya kuanza tena kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Shirikisho la Uswizi. Kamati ya Wafadhili nchini Uswiss imekuwa ikisimamia uchangishaji fedha katika miaka ya hivi karibuni: “Mwitikio wa idadi ya watu wa Uswiss umekuwa wa ukarimu wa ajabu na mzuri licha ya hali halisi, amesema rais wa Kamati hiyo, Doris Leuthard, akionesha imani kwamba: “tutaweza kuongeza fedha zilizosalia katika miezi ijayo. Hii inadhihirisha kushikamana kwa watu wa Uswiss kwa Walinzi wa Uswiss na jukumu lake katika ulinzi wa Baba Mtakatifu”. Shukrani na kuridhika sana pia kumeoneshwa na Walinzi wa Uswiss wenyewe: “Kambi mpya itaboresha kwa kiasi kikubwa ubora wa maisha yetu: faragha zaidi na wakati huo huo maisha zaidi ya jumuiya”, kwa mujibu wa msemaji, Naibu Koplo Manuel von Däniken: “Ukarabati huo unafungua juu ya mitazamo mipya kwa walinzi hai na ninaamini kuwa itawapa motisha vijana wa kiume kufanya na kupanua huduma yao kwa Papa”.