Askofu Paolo Martinelli(OFMcap)ni Msimamizi mpya wa kitume,Falme za Uarabuni
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua msimamizi wa Kitume wa Nchi za Falme za Kiarabu Kusini Askofu Paolo Martinelli, O.F.M. Cap., ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Milano, kwa kupewa Makao ya Musti ya Numidia. Uteuzi huo ni baadaya ya Baba Mtakatifu Francisko kupokea barua ya kung’atuka kwa Msimamizi wa Kitume katika Nchi za Uarabuni Kusini na visiwa vyake vya kiarabu iliyowakilishwa na Askofu Mkuu Paul Hinder, O.F.M. Cap.
Askofu Martinelli alizaliwa mjini Milano mnamo tarehe 22 Oktoba 1958, alikomaza wito wake wa Kifransiskani mnamo mwaka wa 1978 na kujiunga katika Shirika la Ndugu Wadogo Wafransiskani Wakapuchini katika jimbo la Makatifu Caroli, mkoa wa Lombardia, Italia. Alipewa daraja la Upadre mnamo Septemba 1985, na alisomea na kufundisha taalimungu katika vyuo vikuu mbalimbali vya kipapa. Tarehe 24 Mei 2014 aliteuliwa kuwa askofu msaidizi wa Milano Italia. Kusimikwa kwa uaskofu kulifanyika katika Kanisa Kuu mnamo tarehe 28 Juni 2014. Katika mji mkuu wa Ambrosiani yeye ni Askofu Msaidizi na ambaye alikuwa anatoa huduma kwa ajili ya maisha ya wakfu na huduma ya kichungaji shuleni, pia ni mjumbe wa Baraza la Maaskofu Italia CEI katika kitengo cha maisha ya wakfu na huduma ya kichungaji ya afya. Katika Baraza la Maaskofu Italia CEI yeye ni rais wa Tume ya Maaskofu kwa ajili ya Makasisi na Watawa. Anao ushirikiano mkubwa sana na mabaraza mengi ya kipapa.
Baada ya kupata habari hizo Dominika, Mei Mosi Askofu Mkuu wa Milano Mario Delpini wa Jimbo Kuu Katoliki Milano katika ujumbe wake, alikumbuka kwamba utume mpya unamtaka Askofu Martinelli kutunza waamini wa Kikatoliki waliopo katika eneo kubwa sana, na wengi wao wakiwa wahamiaji waaminifu kwa kazi kutoka nchi za Asia. Usimamizi huo unajumuisha katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Oman, na Yemen, kwa ujumla ya watu wapatao milioni 43. Kwa njia hiyo Askofu Mkuu Delipimi alitoa sauti kwa niaba ya Jimbo Kuu la Milano na Baraza la maaskofu wa Lombardi ili kutoa shukrani kubwa na pongezi kwa Askofu Paolo kuteuliwa huko katika shamba la Bwana.