Askofu Mkuu Gallagher anakwenda Lviv na Kiev kwa ajili ya mazungumzo
Vatican News
Kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vita ili kupeleka na kuonesha ukaribu wa Papa Francisko na Vatican kwa ujumla ndiyo utume utakaoanza Alhamisi 18 Mei 2022 wa Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Ushirikiano na Mataifa, Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher. Safari ya Kiongozi huyo wa Vatican Nchini Ukraine kwa hakika ni fursa ya kuadhimisha miaka 30 tangu kuanza kwa uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo ya Ulaya Mashariki. Safari hiyo pia ni kuthibitisha umuhimu wa mazungumzo kurejesha amani. Miongoni mwa miji ambayo itaguswa ni Lviv na Kiev. Ya kwanza inajumuisha siku ya Jumatano 18 Mei 2022 ambapo kutakuwa na mkutano na Askofu Mkuu Igor Vozniak wa Kigiriki-Katoliki wa Lviv, ikifuatiwa na ziara ya makazi ya wakimbizi. Alhamisi Mei 19, mkutano wa kwanza na rais wa mkoa wa Lviv, Maksym Kozytskyy, baadaye mkutano na Askofu Sviatoslav Shevchuk. Pia atakutana na Askofu mkuu Stanisław Gądecki wa Kanisa Katoliki la Kigiriki la Ukraine, na rais wa Baraza la Maaskofu wa Poland.
Vatican imekuwa ikiunga mkono kuhusu mazungumzo ya kidiplomasia
Askofu Mkuu Gallagher hata hivyo alikuwa tayari ametangaza juu ya safari yake katika mahojiano na televisheni, yaliyofanywa wiki iliyopita, wakati wa kipindi cha Rai "Tg2 post". Wakati wa mahojiano hayo ya dakika ishirini, Askofu Mkuu aligusia mada mbalimbali, kuanzia na vita vya Ukraine, hadi kusitisha silaha, athari za kimataifa na kiekumene za mzozo huo. Safari hiyo, alifafanua, kwamba ilikuwa tayari imepangwa kabla ya Pasaka na baadaye kuahirishwa kwa sababu za kiafya. Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa alikuwa amesisitiza pia kwamba: “mara kwa mara Vatican inaunga mkono jaribio lolote la mazungumzo ili kukuza maelewano na kutafuta suluhisho. "Maneno, yana uzito mkubwa katika hatua za kidiplomasia, hasa ikiwa maisha ya watu yanawategemea. Inahitajika kuzuia hatari ya unyonyaji na kurejesha ukweli wa dhati”.