Kard.Krajewski na Pasaka huko Kiev:Nimewaletea baraka ya Papa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Konrad Krajewski, Msimamizi wa Sadaka ya Kitume ya Papa akiwa mbele na macho yake yaliona kile kilichotendeka cha kushangaza na kusikitisha huko Borodjanka nchi Ukraine, sehemu moja ambayo imepata pigo kali sana tangu kuanza kwa mgogoro wa vita kati ya Urussi na Ukraine, mahali ambapo kuna shimo kubwa lenye maziko ya halaiki ya miili 80 ya wasio na majina. Alipiga magoti na kusali mbele ya kaburi hilo. Hilo ni tukio ambalo alilitimiza siku ya Njia ya Msalaba, Ijuma Kuu pamoja na Balozi wa Vatican nchini Ukraine, Askofu Mkuu Visvaldas Kulbokas.
Na “Katika uchungu mkali hatupaswi kujiachia katika maumivu hayo ambayo yanatufanya tufadhaike”, alisema hayo Kardinali wakati wa mahuburi yake katika Misa iliyoadhimishwa katika Kanisa kuu la Kiev, Dominika tarehe 17 Aprili 2022. Maadhimisho hayo hata hivyo yaliongozwa na Balozi wa Vatican Nchini Ukraine kwa ushiriki wa Askofu Vitalii Kryvytskyi, wa jimbo la Kyiv-Zhytomyr. Kardinali Krajewski amekumbusha kwamba Ufufuko wa Yesu ni ishara ya amani. “Yeye alikuwa afufuke kwa sababu, vinginevyo tungelazimika kukaa katika siku ya Ijumaa Kuu, kusimama hapo na kuacha tu mateso na dhambi na kuzungumza kibinadamu kusingekuwa na njia ya kutoka katika hali hiyo”.
Kwa maana hiyo Kardinali amebainisha kuwa “shukrani kwa Mungu, kuna Ufufuko, wakati Kristo anapoondoa maovu yote, kuna tumaini kwamba anatubariki”. Baadaye Kadinali Krajewski vile vile amekumbuka ujumbe wa Papa Francisko wa Urbi et Orbi alioulekeza kwa waamini wote wa Roma na ulimwengu mzima na mwaliko wa kuombea Ukraine. “Nanawaletea baraka za Baba Mtakatifu”. Na kwamba “Amani itawale, maana Mungu ameshinda maovu yote, amefufuka na sisi pia tutafufuka. Христос воскрес! Kwa lugha ya kiukreaine maana yake (Kristo amefufuka!).