Tafuta

Kardinali Leonardo Sandri anawashukuru na kuwapongeza Wafranciskani ambao wameendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati. Kardinali Leonardo Sandri anawashukuru na kuwapongeza Wafranciskani ambao wameendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati. 

Mchango wa Ijumaa Kuu: Upendo! Majiundo Na Elimu Nchi Takatifu

Mchango wa Ijumaa kuu kwa mwaka 2021 zilipatikana Dola za Kimarekani 6, 062, 789, 90. Fedha hii imetumika kwa ajili ya malezi na majiundo ya waseminari na mapadre walioko chini ya uongozi wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Fedha hii imetumika kutoa ruzuku ili kugharimia huduma katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi bila upendeleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, alitembelea Nchi Takatifu mwezi Januari 1964 na kuguswa na mahitaji ya Wakristo. Katika Wosia wake wa Kitume “Nobis in animo” yaani “Umuhimu wa Kanisa katika Nchi Takatifu” uliochapishwa tarehe 25 Machi 1974, alikazia umoja na mshikamano wa waamini. Huo ukawa ni chimbuko la Sadaka na Mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu: "Pro Terra Sancta".  Mtakatifu Paulo VI alihimiza sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu, kama amana na urithi wa imani; ushuhuda endelevu wa Jumuiya ya Wakristo unaoonesha jiografia ya ukombozi. Tangu wakati huo, Kanisa linaendelea kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoteseka kunyanyaswa na hata kuuwawa huko Mashariki ya Kati, lakini hasa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, ni alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa kwa watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uekumene wa damu, huduma na sala pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu katika misingi ya: haki, amani na maridhiano.

Ushuhuda wa upendo na mshikamano na watu wa Mungu Mashariki ya Kati
Ushuhuda wa upendo na mshikamano na watu wa Mungu Mashariki ya Kati

Ni kwa njia ya ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano Kanisa linataka kuwajengea waamini na watu wote wenye mapenzi huko Mashariki ya kati Injili ya amani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi ili kuondokana na: vita, vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kiimani, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika ujumbe wake kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa mwaka 2022 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari huruma na upendo wa Kristo Yesu uliotundikwa juu ya Msalaba. Katika kipindi cha mwaka 2021 Baba Mtakatifu Francisko alifanikiwa kufanya hija za kitume nchini Iraq, Cyprus na hatimaye, nchini Ugiriki huko alishuhudia mateso ya watu wa Mungu kutoka na vita, mwaliko kwa waamini kumwendea Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu, ili aweze kuwakirimia tena maisha mapya. Alishuhudia mateso, mahangaiko na matumaini ya wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa.

Katika hija zote hizi, Baba Mtakatifu alipania kuonesha uwepo na ukaribu wake kwa watu wa Mungu wanaoteseka, ili hatimaye, waweze kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu. Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na hafi tena. Lakini, Kristo Yesu anaendelea kuteseka katika Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa hususan huko Mashariki ya Kati. Bado kuna dhuluma na nyanyaso; watu wanaishi katika mazingira magumu na wasiwasi kuhusu usalama wa maisha yao. Kana kwamba, mahangaiko yote haya hayatoshi, vita imefumuka tena huko nchini Ukraine. Kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO-19 kwa muda wa miaka miwili mfululizo, waamini wanaoishi katika Nchi Takatifu wameshindwa kuadhimisha Sherehe za Noeli na Pasaka kwa uwepo na ushiriki wa mahujaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. UVIKO-19 umesababisha madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, umekuwa ni msaada mkubwa kwa watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu na Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Hiki ni kielelezo cha mshikamano na upendo wa udugu wa kibinadamu; matunda ya upendo na ushiriki mkamilifu katika shida na mahangaiko ya wengine.

Kardinali Leonardo Sandri anawashukuru waamini kwa upendo na mshikamano
Kardinali Leonardo Sandri anawashukuru waamini kwa upendo na mshikamano

Kardinali Leonardo Sandri anawashukuru na kuwapongeza Wafranciskani ambao wameendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati, lakini kwa namna ya pekee katika Nchi Takatifu. Maadhimisho Juma kuu, iwe ni fursa ya kusali, kutangaza na kushuhudia upendo, ukarimu, huruma na msamaha unaofumbatwa katika Njia ya Msalaba. Sala hii ya upendo na mshikamano inabubujika kutoka sehemu mbalimbali za dunia, isaidie kumtolea Mungu sifa na utukufu kwa njia ya ukarimu kwa watu wanaoishi katika Nchi Takatifu. Wakleri na watawa wawe mstari wa mbele kutoa pongezi na shukrani kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa mchango unaotolewa na waamini kwa ajili ya Nchi Takatifu. Nchi zinazofaidika na mchango huu ni pamoja na Maeneo ya Nchi Takatifu, Palestina, Israeli, Yordan, Cyprus, Siria, Lebanon, Misri, Ethiopia, Eritrea, Uturuki, Iran na Iraq. Mchango wa Ijumaa kuu kwa mwaka 2021 zilipatikana Dola za Kimarekani 6, 062, 789, 90. Fedha hii imetumika kwa ajili ya malezi na majiundo ya waseminari na mapadre walioko chini ya uongozi wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Fedha hii imetumika kutoa ruzuku ili kugharimia huduma katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Kimsingi mchango wa Ijumaa Kuu umeliwezesha Kanisa kutekeleza kwa makini shughuli mbalimbali za matendo ya huruma pamoja na maboresho ya mchakato wa huduma katika sekta ya elimu.

Mchango wa Ijumaa Kuu
13 April 2022, 15:41