Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 30 Aprili 2022 kutoa Daraja ya Ushemasi kwa Majandokasisi 24. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 30 Aprili 2022 kutoa Daraja ya Ushemasi kwa Majandokasisi 24. 

Mashemasi Watarajiwa 24 Yumo Xavery Dominic Binyoga, Kigoma

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 30 Aprili 2022, majira ya Saa 4: 00 Asubuhi kwa Saa za Ulaya, sawa na saa 5: 00 kwa Saa za Afrika Mashariki, anatarajiwa kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 24 kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Kutoka Afrika tunao Mashemasi watarajiwa sita! Yaani.

Na Xavery Dominic Binyoga, Roma.

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya huruma na upendo unaomwilishwa katika huduma kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Mashemasi ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo kwa njia ya maisha ya wakfu!

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 30 Aprili 2022, majira ya Saa 4: 00 Asubuhi kwa Saa za Ulaya, sawa na saa 5: 00 kwa Saa za Afrika Mashariki, anatarajiwa kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 24 kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Kutoka Barani Afrika tunao: Akonda Waran Charles Josep, Jimbo Katoliki la Yei, Sudan ya Kusini. Dinis Gelson Fernando Augusto, Jimbo kuu la Luanda, Angola. Fortes Monteiro Ricardo Jorge, Jimbo Katoliki la Mindelo, Cape Verde. Ndabijejimana Bonaventura, Jimbo Katoliki la Rutana, Burundi. Obambi Jenner Wandermann, Jimbo Katoliki la Gamboma, Congo. Tchari Tongambori Hubert, Jimbo Katoliki la Natitingou, Benin na hatimaye ni Tendeng Jean Pierre Amaye, Jimbo Katoliki la Zinguichor, nchini Benin. Kati yao yumo pia Xavery Dominic Binyoga, Mtanzania kutoka Jimbo Katoliki la Kigoma anayesimulia safari wito wake huku akiongozwa na kauli mbiu yake Kishemasi kwa kusema “Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tukiwaombea” Kol 1:3.

Kardinali Luis Tagle ndiye aliyekabidhiwa dhamana ya kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi
Kardinali Luis Tagle ndiye aliyekabidhiwa dhamana ya kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi

Naitwa Xavery Dominic Binyoga, Nilizaliwa mnamo tarehe 29 Januari 1992 katika kijiji cha Mukabuye Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma, nchini Tanzania na wazazi wangu ni Dominic Binyoga na Lucia Ntamakulilo. Ni mtoto wa pili kati ya watoto kumi. Nilibatizwa tarehe 12 Aprili 1992 katika Parokia ya Mabamba, Jimbo Katoliki la Kigoma. Nilipata Sakramenti ya Ekaristi takatifu tarehe 21 Juni 2003 katika Parokia ya Mabamba. Na Sakramenti ya Kipaimara tarehe 16 Julai 2004 katika Parokia hiyohiyo ya Mabamba. Nilianza masomo ya elimu ya msingi katika shule ya Msingi Mukabuye mwaka 2000 mpaka 2006. Elimu ya sekondari katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Yosefu Iterambogo iliyoko Jimbo Katoliki Kigoma kwa Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne mwaka 2007 mpaka 2010. Na Seminari ndogo ya Mtakatifu Kizito Mafinga, Jimbo Katoliki la Iringa kwa masomo ya kidato cha tano mpaka cha sita mwaka 2011-2013. Mwaka huohuo nilijiunga na Jeshi la kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria katika kambi ya Burombora. Nilihitimu mafunzo hayo na kurudi nyumbani kuendelea na tafakari ya wito.

Nilituma maombi ya kuanza sasa malezi na masomo ya Kipadre na Mwaka 2014 nilienda Nyumba ya malezi ya Watakatifu Petro na Paulo Iterambogo Jimbo Katoliki Kigoma. Oktoba mwaka 2014 nilitumwa katika Seminari ya Bikira Maria Malkia wa Malaika, Kibosho iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania kwa masomo ya Falsafa. Nilihitimu masomo hayo ya Falsafa mwaka 2017.  Mwezi Oktoba 2017, nilitumwa Seminari kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala Jimbo kuu la Tabora kwa masomo ya Taalimungu, nilikaa kwa kipindi cha takriban miezi 9, ambapo nilitumwa Roma kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu Cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu nikiishi “Collegio Ecclesiatico Internazionale Sedes Sapientiae kuanzia mwaka 2018-2021. Baadaye nilijiunga na Chuo kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselm kwa masomo ya Shahada ya Uzamili katika Liturujia ya Kanisa, ili Mwenyezi Mungu atukuzwe na mwanadamu aweze kutakatifuzwa.

HISTORIA YA WITO. Historia ya wito wangu inaanza hasa nikiwa mdogo sana, nilikuta napenda kuwa Padre, na kwa kweli hamu hasa ilianza kwa kiasi kikubwa nikiwa darasa la IV na nikiwa na umri wa miaka 11. Nilianza kuwaomba wazazi wangu ili nitume maombi ya kujiunga na seminari ndogo. Haikuwa rahisi maana upande wa wazazi hasa Baba hakuupokea vizuri mwelekeo huu kwa wakati huo.  Niliendelea kusali huku nikifurahia maisha ya kuwa karibu na wazazi kwa kuwasikiliza na kuwatii. Hivyo sikutuma maombi. Nikiwa nafuata mafundisho ya kupokea komunio ya kwanza, Katekista Silvanus Lambert aliyekuwa anatufundidha aliniambia, “Kijana Exa, uko vizuri na naona kuwa hata ukifanya mtihani wa Seminari unaweza kufaulu...” kwangu ilikuwa kama kuamsha ndoto iliyokuwa imeshaanza kufifia. Nilimweleza kuwa nia hiyo ninayo ila upande wa nyumbani, Baba hakuwa tayari kunipatia fursa hii ya kujiunga na malezi ya Seminari. Aliniahidi kwenda kuzungungumza nao. Mazungumzo hayakufua dafu! Niliendelea na kuwa na nia hiyo japo matumaini yakiwa madogo.

Daraja ya Ushemasi ni kwa ajili ya huduma ya Neno, upendo na huruma ya Kanisa
Daraja ya Ushemasi ni kwa ajili ya huduma ya Neno, upendo na huruma ya Kanisa

Nikiwa darasa la sita na ndoto hiyo ikiwa imefifia ya kujiunga na seminari ndogo, mwalimu Pastori Kanani aliyetufundisha shule ya msingi; ambaye alikuwa Ex- seminarian wa Seminari ya Ujiji naye pia aliniambia usemi ule ule wa Katekista, na nikamjibu kama nilivyomjibu Katekista, naye akaniahidi kwenda kuongea na Baba. Mazungumzo yao yakazaa matunda ya matumaini. Alimsisitizia baba kuwa sio kila aliyesomea seminari anakuwa Padre na akijitolea mfano yeye mweneyewe ambaye alikuwa na ndoa tayari.  Changamoto ikaja kuwa kulingana na utaratibu nilikuwa tayari nimeshachelewa kutuma Maombi, maana mwisho wa kutuma maombi ilikuwa ni darasa la tano, nami nilikuwa darasa la sita. Basi nikasubiri padre aje na bahati nzuri akaja Paroko msaidizi wakati huo, Padre Lucas Mashanya, nikamweleza yote na akasema tumeshachelewa lakini akasema niandike barua na kwa kuwa naenda jimboni niiipekele kabisa. Basi nikajawa na furaha nikandika barua na ikaenda na nikajibiwa. Nikafanya mtihani na nikachaguliwa kujiunga na Seminari ndogo ya Mtakatifu Yosefu Iterambogo ambapo ndipo wito wangu ulipoendelea kukua. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ana saa yake katika maisha ya kila mmoja wetu.

Niliendelea na masomo na tafakari wakati huo, nilipomaliza masomo ya kidato cha IV, ikaja sasa changamoto nyingine, kama naweza kuendelea na Seminari au niende shule ya serikali, baadhi ya ndugu wakashauri nisiendelee na Seminari ili nisije kuvutiwa na Upadre na wengine wakasema niendelee tu, basi nikaendelea na hatimaye, nikahitimu kidato cha VI, na kuanza kufanya maamuzi ya kuendelea na Seminari kuu. Na wakati huo, uchumi nyumbani ukawa umeyumba, nikafanya kazi kwa miezi kadhaa na nikiwa namthibitishia nia ya kuwa padre, Baba yangu mpendwa. Hatimaye nikapata baraka ya wazazi wote wawili. Nao wote kwa pamoja wakawa nami na kuahidi kunisindikiza katika safari yangu ya malezi na maisha kwa sala na sadaka zao. Na wamekuwa wakifanya hivyo mpaka sasa. Na baadaye nikajiunga na nyumba ya malezi 2014, nikafanya Falsafa Moshi, na baadaye nikaja Roma kwa Taalimungu na sasa naelekea kupewa Daraja ya Ushemasi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa kuwekewa mikono na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

Shemasi ni mhudumu wa Injili ya huruma, upendo na ukarimu
Shemasi ni mhudumu wa Injili ya huruma, upendo na ukarimu

NISEME NINI MIMI? Ni shukrani nyingi kwa Mwenyezi Mungu maana haya yote ameyawezesha Yeye. Lakini pia niwashukuru sana wazazi wangu walionizaa, kunilea na kunisindikiza katika safari hii ya wito kwa sala na sadaka yao. Nashukuru pia Jimbo Katoliki Kigoma na kwa namna ya pekee Baba Askofu Joseph Roman Mlola kwa kunipokea na kunituma katika Seminari mbalimbali kwa malezi na hatimaye, kunituma hapa Roma kwa malezi na masomo. Nawashukuru walezi wote, nikianza na walimu wangu na walezi wote walionilea katika seminari zote nilizopitia. Nawashukuru Ndugu, jamaa na marafiki ambao tumekuwa nao, ambao pia wana mchango mkubwa katika malezi na makuzi yangu.  Nawashukuru pia wafadhili wote hasa waliojitoa kwa michango na kunisindikiza hasa kipindi hiki nikiwa mbali na nyumbani. Nanyi vijana wenzangu msikate tamaa, Mwenyezi Mungu akikuita inawezekana. Nanyi wazazi msisite kusikia sauti ya Mungu inayowaita vijana wenu kumtumikia kama mapadre, watawa na watu wa ndoa. Muwe tayari pia kujitoa kwa hali na mali kuwasindikiza watoto wenu huku mkishirikiana na Mungu kuimarisha miito ndani mwao. Msiwe kikwazo kwa watoto wenu hasa katika miito ya Upadre na Utawa, kwani mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Mwenyezi Mungu awabariki na kuwalinda nyote kwa huruma na tunza yake ya Kibaba. Kwa unyenyekevu mkubwa, ninawaomba mzidi kunisindikiza katika sala na sadaka yenu.

Shemasi Kigoma
28 April 2022, 17:21