Kumbukizi la Miaka 30 ya Uhusiano Wa Kiplomasia na Mexico: Historia Tete Kwa Miaka 130
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Mtakatifu Yohane Paulo II alifanya hija ya kitume nchini Mexico kunako mwaka 1979. Matokeo ya hija hii ni Mexico na Vatican kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia, uliotiwa saini tarehe 21 Septemba 1992. Kumbe, tarehe 21 Septemba 2022, Vatican na Mexico zinafanya kumbukizi la miaka 30 lililovunja uhusiano tenge wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili uliokuwa umedumu kwa takribani miaka 130. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hija yake ya kitume nchini Mexico, tarehe 26 Aprili 2022 ameadhimisha kumbukizi hili la kihistoria. Katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha mahusiano chanya kati ya Serikali na Kanisa; Ushuhuda wa Wakristo katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; uhuru wa kidini; Mexico kama mfano wa Uinjilishaji wa kina uliokita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kardinali Pietro Parolin, amekazia umuhimu wa Serikali kujenga mahusiano na mafungamano chanya, ili kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani; udugu wa kibinadamu na haki jamii. Huu ni mwaliko kwa pande zote mbili kulinda haki msingi za binadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Imani ya Kikristo inawawezesha waamini kuitangaza na kuimwilisha katika vipaumbele vya maisha yao kama chachu ya mabadiliko chanya katika mifumo mbali mbali ya maisha ya mwanadamu. Tunu msingi za Kiinjili zimekuwa ni chachu katika falsafa, sheria pamoja na sera za kiuchumi.
Ni katika muktadha wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, Mama Kanisa amekuwa mstari wa mbele kupambana na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa daima linapenda kushirikiana na Serikali mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba, binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2.
Uhuru wa kidini uwawezeshe waamini kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii kwa ajili ya ujenzi wa nchi yao. Kumbe, Kanisa na Serikali zinapaswa kushirikiana kikamilifu. Uvamizi wa Kikoloni uliofanywa na Hispania nchini Mexico sanjari na harakati za uinjilishaji wa kina, Serikali ya Mexico ikajenga chuki dhidi ya Kanisa. Lakini kuna ushuhuda wa kutosha kwamba, hata katika hali hii tete ya mahusiano kati ya Kanisa la Serikali ya Mexico, bado kulikuwepo na wamisionari jasiri waliojipambanua kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Muujiza wa Bikira Maria kumtokea Mtakatifu Juan Diego kunako mwaka 1531 ni kielelezo makini cha ushuhuda huu unaosimikwa katika mchakato wa utamadunisho na uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Wapo watakatifu kama San Junìpero Sera waliosimama kidete kulinda utu wa binadamu. Serikali ya Mexico na Kanisa ni mashuhuda kwamba hata baada ya miaka 130 kushinda misimamo mikali ya kiitikadi ili kutengeneza mazingira yatakayorutubisha utamaduni wa udugu wa kibinadamu, uhuru, majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na mshikamano wa dhati. Vipaumbele vya Vatican katika diplomasia ya Kimataifa ni haki na amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kupambana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.
Kumbukizi la miaka 30 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Mexico na Vatican, pengine ni mapema sana, kupima matunda ya safari hii tete kati ya nchi hizi mbili; kati ya ushirikiano wa Serikali na Kanisa. Jambo la msingi anasema Kardinali Pietro Parolin, ni huduma makini kwa watu wa Mungu: kiroho na kimwili; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, amani ni chachu ya maendeleo fungamani ya binadamu.