Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amemtea Mheshimiwa sana Padre Wolfgang Pisa, O.F.M. Cap. kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Lindi, Tanzania. Baba Mtakatifu Francisko amemtea Mheshimiwa sana Padre Wolfgang Pisa, O.F.M. Cap. kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Lindi, Tanzania.  (AFP or licensors)

Askofu Wolfgang Pisa, Jimbo Katoliki la Lindi, Tanzania

Askofu mteule Wolfgang Pisa O.F.M. Cap. alizaliwa tarehe 6 Julai 1965 huko Karatu, Jimbo Katoliki la Mbulu. Baada ya masomo na malezi ya kitawa Lusaka, Zambia na Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro aliweka nadhiri za daima tarehe 15 Agosti 1998 na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 1 Septemba 1999. Hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu alikuwa Paroko-usu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Bruno Pius Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi, Tanzania la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Sana Padre Wolfgang Pisa O.F.M. Cap. kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Lindi. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Wolfgang Pisa O.F.M. Cap. alikuwa ni Paroko usu wa Parokia ya Kwangulelo Jimbo kuu la Arusha na Jalimu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania, SAUT, Tawi la Arusha. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Wolfgang Pisa O.F.M. Cap. alizaliwa tarehe 6 Julai 1965 huko Karatu, Jimbo Katoliki la Mbulu. Baada ya masomo na malezi ya kitawa Lusaka, Zambia na Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro aliweka nadhiri za daima tarehe 15 Agosti 1998 na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 1 Septemba 1999.

Askofu Wolfgang Pisa, Jimbo Katoliki la Lindi, Tanzania
Askofu Wolfgang Pisa, Jimbo Katoliki la Lindi, Tanzania

Tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre amewahi kutekeleza shughuli zake za kichungaji na kitume kama Jalimu na Mlezi, Seminari Ndogo ya Maua, Jimbo Katoliki la Moshi kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2000. Baadaye alitumwa na Shirika kujiendeleza zaidi katika masomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hapo akajipatia Shahada ya Uzamili. Akateuliwa kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Maua kati ya mwaka 2005-2008. Baadaye alijiendeleza zaidi katika masomo ya maadili Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Marekani, Catholic University of Amerika huko Washington, DC kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2011. Akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wakapuchini Kanda ya Tanzania na kuwaongoza tangu mwaka 2011 hadi mwaka 2017. Baadaye kati ya mwaka 20017-2019 akarejea tena darasani huko Catholic University of America huko Washington, DC na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Maadili. Amewahi kufanya shughuli zake za kichungaji Parokiani Kibaigwa, Jimbo kuu la Dodoma kati ya mwaka 2019-2020. Tangu wakati huo, hadi kuteuliwa kwake, Askofu mteule Wolfgang Pisa O.F.M. Cap. alikuwa ni Paroko usu wa Parokia Kwangulelo Jimbo kuu la Arusha na Jalimu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania, SAUT, Tawi la Arusha.

Mama Kanisa anampongeza na kumshukuru Askofu mstaafu Bruno Pius Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi, aliyezaliwa kunako tarehe 8 Agosti 1945 huko Magaura. Tarehe 8 Novemba 1974 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 6 Oktoba 1990 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi na kuwekwa wakfu na Mtakatifu Yohane Paulo II, Sherehe ya Tokeo la Bwana tarehe 6 Januari 1991, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Na ilipogota tarehe 9 Aprili 2022 akang'atuka kutoka madarakani. Waswahili wanasema Askofu Ngonyani "ameupiga mwingi sana sasa anaanza kupumzika kidogo."

Jimbo Lindi

 

09 April 2022, 11:56