Tafuta

Vatican inasema chanzo dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa UVIKO-19 inapaswa kutabuliwa kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu kwa vile inahusiana kwa karibu sana na ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inasema chanzo dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa UVIKO-19 inapaswa kutabuliwa kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu kwa vile inahusiana kwa karibu sana na ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Lindeni Na Kudumisha Haki Msingi Za Binadamu Kwa Mafao Ya Wengi

Askofu mkuu Fortunatus Nwachukwu, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva nchini Uswis amekazia umuhimu wa ugawaji wa chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi Vya Korona, UVIKO-19 kama sehemu ya haki msingi za binadamu kutokana na madhara yake makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kuimarisha afya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tamko la Kimataifa la Haki Msingi za Binadamu ni matokeo ya kukutana kati ya tamaduni za kidini na mila kati ya watu, pande zote zikiwa zinasukumwa na nia ya pamoja ya kumuweka mwanadamu kuwa ndiye kiini cha taasisi, sheria, matukio ya kijamii, tamaduni, dini na sayansi (Rej., Benedikto XVI, Hotuba kwa Umoja wa Mataifa, 18 Aprili 2008). Kwa hakika Tamko la Kimataifa la Haki Msingi za Binadamu ni jiwe la msingi lililowekwa katika historia ndefu na ngumu kwa Familia ya binadamu. Mtakatifu Yohane Paulo II amasema kwamba, maendeleo ya mwanadamu yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia: sayansi na teknolojia, lakini zaidi sana kwa kuzingatia maendeleo fungamani ya binadamu ya kiroho, kiutu na kimaadili (Rej. Yohane Paulo II, Hotuba kwa Umoja wa Mataifa, 2 Oktoba 1979). Haki msingi za binadamu zinachota uhalali wake kutoka katika kanuni asilia inayojumuisha wanadamu wote.  Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Tamko la Kimataifa la Haki msingi za Binadamu lina lengo la kuvunjilia mbali kuta za utengano na zinazoigawanya Familia ya binadamu, na kisha lisaidie kunogesha maendeleo fungamani ya binadamu Iwapo mwanadamu hatatazamwa katika: umoja, utu, hadhi, heshima na haki zake msingi hapo ndipo huwa chanzo cha ukosefu wa haki, kutokuwepo usawa wa kijamii na kufumuka kwa rushwa, ufisadi na nyanyaso za kila aina (Rej., Francisko, Hotuba kwa Wanadiplomasia mjini Vatican, 8 Januari 2018).

Chanjo dhidi ya UVIKO-19 inapaswa iwe ni sehemu ya haki msingi za binadamu.
Chanjo dhidi ya UVIKO-19 inapaswa iwe ni sehemu ya haki msingi za binadamu.

Tamko la Kimataifa la Haki Msingi za Binadamu ni nyenzo ya kutetea uhuru wa binadamu dhidi ya uonevu, umoja wa Familia ya binadamu dhidi ya utengano wa kinadharia, kisiasa, ama ubaguzi wa rangi, jinsia, lugha na kidini. Tamko hili tangu awali limelenga kumlinda na kumtetea mwanadamu dhidi ya tabia ya kuabudu taifa na kumpotezea raia. Tamko limelenga pia kushinda hatari za uhalifu kutokana na makosa ya uhaini na matokeo mabaya ya vita na mauaji ya kimbari ili kulinda na kutetea thamani ya uhai, uhuru na hadhi ya binadamu. Kanisa linao mtazamo wa haki stahiki inayofaa mahali pote ili kuepuka hatari ya mifumo mamboleo ya utumwa na unyanyasaji inayopaliliwa na Mataifa makubwa na Mashirika yake kwa kuwaonea maskini na wanyonge. Tamaduni za kitaifa zisichukue nafasi ya kutotilia maanani haki msingi za binadamu zilizotiwa mkwaju katika Tamko la Kimataifa. Haki za binadamu hazina mipaka kimataifa, hazigawanyiki, zinategemeana na zina mahusiano na mafungamano makubwa kati yake. Wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa ni kuhakikisha kwamba haki hizi zinalindwa na kutetewa katika kila kona ya dunia, huku zikipewa thamani yake stahiki.

Wakati huo huo kila taifa lihakikishe haki hizi zinazingatiwa katika nyanja zote kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni. Ulinzi na utetezi wa haki msingi za binadamu bado unakumbana na changamoto mamboleo, kumbe, ni muhimu kusoma alama za nyakati lakini bila kupoteza thamani yake na kwa kuzingatia kanuni asilia, kutogawanyika, kutegemeana; mahusiano na mafungamano kati yake. Iwapo kanuni hizi hazitatiliwa maanani, hatari ni kujikuta watu wanajiongezea haki na mifumo mipya kila siku inavyopelekea mpasuko kati ya mtu na mpasuko katika jamii. Mtazamo wa Kanisa ni wa msingi kusimamiwa kwamba, haki msingi za binadamu zinatokana na hadhi na utu wa binadamu mwenyewe ikiwa ni pamoja na thamani asilia ya haki hizo. Hivyo mwanadamu lazima awekwe kuwa ndiye kiini cha haki hizo katika nafsi ya kila mmoja na kisha katika upamoja kama jumuiya. Mtazamo huu ndio unaokuza juhudi za pamoja za kulinda na kutetea haki za kila mmoja na kwa jamii kwa ujumla kuhusu afya, elimu, lishe, ajira, usalama, mapumziko na maisha ya kifamilia.

Tafiti, ujuzi na maarifa yawe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Tafiti, ujuzi na maarifa yawe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Haki nyingi za binadamu ziko mashakani leo hii kufuatia baadhi ya matajiri na wenye nguvu kuwatazama wengine kana kwamba ni “bidhaa sokoni na sio watu tena”, hivyo kuwatumia watu hawa kwa ajili ya kujinufaisha bila kujali kabisa utu na heshima yao kama kibinadamu. Kanisa limekuwa mstari wa mbele siku zote kulinda na kutetea haki msingi za binadamu kwani binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni katika muktadha wa haki msingi za binadamu, hivi karibuni Askofu mkuu Fortunatus Nwachukwu, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva nchini Uswis amekazia umuhimu wa ugawaji wa chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi Vya Korona, UVIKO-19 kama sehemu ya haki msingi za binadamu kutokana na madhara yake makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utengenezaji na usambazaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 pamoja na teknolojia ni sehemu ya haki za ubunifu wa kiakili, “Intellectual property rights, IPRs.”

Baba Mtakatifu Francisko anasema, chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na huduma bora za afya ni sehemu ya wajibu wa kimaadili na kiutu. Katika mazingira kama haya, kamwe huduma ya afya ya jamii isilenge zaidi kwenye masilahi ya mtu binafsi. Badala yake, sera, sheria na kanuni za Jumuiya ya Kimataifa hazina budi kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, tafiti za kisayansi, ujuzi na maarifa hayana budi kukuza maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi, tayari kuanza kujieleza katika ujenzi wa jamii inayosimikwa haki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na ushiriki ili kudumisha sera na mikakati ya uchumi fungamani.

Haki za Binadamu

 

29 March 2022, 16:29