Tafakari Za Kipindi Cha Kwaresima 2022: Liturujia Ya Ekaristi Takatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 ni kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu na zinasimikwa katika sehemu hii ya Injili: “Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote; maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.” Mt 26: 26-28. Kumbe, kauli mbiu inayonogesha tafakari hizi ni: “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Hizi ni tafakari zinazotolewa kwa uwepo wa: Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Maaskofu, wasaidizi wake wa karibu, yaani “Curia Roma”, Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Magambera pamoja na wafanyakazi wa Jimbo kuu la Roma. Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, Ijumaa tarehe 18 Machi 2022 amejikita zaidi kwenye maneno ya Kristo Yesu aliyesema: “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Liturujia ya Ekaristi Takatifu ni kiini cha maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Kuna uhusiano kati ya Ekaristi Takatifu na Berakah ya Wayahudi. Kristo Yesu ni Kuhani na Sadaka inayotolewa, yaani Mwili na Damu yake Azizi, sadaka safi inayotolewa kwa Baba wa milele kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake, wewe Mungu Baba Mwenyezi katika umoja wa Roho Mtakatifu unapata heshima na utukufu wote, daima na milele.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiyahudi, wanaolisaidia Kanisa kuyaelewa Maandiko Matakatifu na Sakramenti za Kanisa. Mahusiano na tofauti zake zinafafanuliwa vyema na Mama Kanisa katika maisha na utume wake mintarafu Liturujia Takatifu ya Kanisa. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya Ekaristi Takatifu na Baraka ya Kiyahudi (בְּרָכָה; pl. בְּרָכוֹת, berakhot, brokhoys; "benediction," "blessing," kama unavyofafanuliwa na Mafundisho ya Mitume yaani “Didachè” na hivyo alama hii ya chakula cha kifamilia, ikawa ni tukio la Kikanisa. Mageuzo ya mkate na divai kuwa Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, kwa Mama Kanisa hii, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kumbukumbu ya kudumu ya Sadaka ya Kristo Yesu Msalabani. Haya ni maadhimisho ambayo Kristo Yesu ndiye Kuhani mkuu na sadaka inayotolewa Altareni, kiini cha historia ya maisha ya kidini ya mwanadamu duniani. Kristo Yesu, Mtu kweli na Mungu kweli akawa ni Sadaka safi inayompendeza Baba wa milele, kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wakakazia umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia Takatifu na kamwe wasiwe ni watazamaji tu, kwa kukazia ukamilifu na uelewa kwa ibada; muhimu wa Biblia, mahubiri, katekesi la lugha ya Liturujia. Rej. Sacrosanctum concilium, 5-40. Mababa wa Kanisa wanasema, Ekaristi Takatifu inaliunda Kanisa ni chemchemi ya utakatifu wa Maisha unaowasukuma waamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani zao, kama sadaka safi inayo mpendeza Mwenyezi Mungu. Hii ni sadaka ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya msamaha na maondoleo ya dhambi. Ni kielelezo cha kifo na maisha mapya yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Waamini wajifunze kusadaka maisha yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha sadaka ya upendo inayotolewa na Kristo Yesu kwa Baba wa milele kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake, wewe Mungu Baba Mwenyezi katika umoja wa Roho Mtakatifu unapata heshima na utukufu wote, daima na milele. Waamini wanahimizwa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa uelewa mkamilifu, ili hatimaye, hata wao wenyewe waweze kuwa ni Ekaristi safi kwa jirani zao na hasa kwa wale wanaohitaji msaada zaidi.