Tafuta

Tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2022 zinajikita katika Fumbo la Ekaristi Takatifu: Umuhimu wa kuendelea kupyaisha Katekesi kuhusu Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2022 zinajikita katika Fumbo la Ekaristi Takatifu: Umuhimu wa kuendelea kupyaisha Katekesi kuhusu Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. 

Tafakari Za Kipindi Cha Kwaresima: Fumbo la Ekaristi Takatifu: Katekesi

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo, Haki, Amani na Upatanisho. Maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamepelekea baadhi ya majimbo na Makanisa mahalia kujikita zaidi katika Katekesi kuhusu Ekaristi Takatifu na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, ipewe umuhimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Kipindi cha Kwaresima, kila Ijumaa, kuanzia tarehe 11, 18, 25 Machi pamoja na tarehe 1 na 8 Aprili 2022 kutakuwa na Tafakari za Kipindi cha Kwaresima kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu. “Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote; maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.” Mt 26: 26-28. Kumbe, kauli mbiu inayonogesha tafakari hizi ni: “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Hizi ni tafakari zinazotolewa kwa uwepo wa: Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Maaskofu, wasaidizi wake wa karibu, yaani “Curia Roma”, Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Magambera pamoja na wafanyakazi wa Jimbo kuu la Roma. Tafakari hizi zinatolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa na Ijumaa tarehe 11 Machi 2022 amejikita zaidi katika Liturujia ya Neno la Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu. Amegusia kuhusu umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Ekaristi Takatifu ni Fumbo endelevu la Pasaka ya Bwana inayoadhimishwa kila siku. Lakini waamini wanapaswa kuondokana na mazoea na badala yake wajenge utamaduni wa ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kujikita katika Liturujia ya Neno la Mungu kutoka katika Agano la Kale na Agano Jipya yaani Nyaraka pamoja na Injili, ili hatimaye, kumtambua Kristo Yesu anayezungumza kati yao. Kardinali Cantalamessa katika mahojiano maalum la Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo, Haki, Amani na Upatanisho. Maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamepelekea baadhi ya majimbo na Makanisa mahalia kujikita zaidi katika Katekesi kuhusu Ekaristi Takatifu na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB limechapisha Waraka Kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu Katika Maisha na Utume wa Kanisa: Kwa kukazia Ekaristi Takatifu kama zawadi, Sadaka ya Kristo Yesu inayoonesha uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Hiki kielelezo cha ushirika na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake unaohitaji majibu muafaka kutoka kwa waamini kama alama ya shukrani na ibada, inayomwezesha Kristo Yesu kuleta mabadiliko ya kina katika maisha ya waja wake, ili kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni maadhimisho yanayo dai toba na wongofu wa ndani, ili kushiriki kikamilifu katika hija ya maisha ya kiroho, kuelekea mbinguni kwenye maisha ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu inawahimiza waamini kutoka na kwenda kumtangaza Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa sababu Kristo Yesu ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho na Nyakati zote ni zake! Katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu inahitajika sana katika maisha na utume wa Kanisa na hasa nyakati za vitisho na ukosefu wa haki, amani na usalama wa raia na mali zao. Leo hii kuna waamini ambao wanashindwa kuhudhuria katika maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kutokana na vita kama ilivyo nchini Ukraine na sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni mwaliko wa kupyaisha tena umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani yake “Fide qua” na wala si tu kuwa ni kielelezo cha imani inayosadikiwa “fides quae.” Huu ni mwaliko wa kutambua ukuu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu ambalo, kila mara linaendelea kumshangaza mwamini. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, yalete hamasa kwa waamini kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kristo Yesu alijitoa sadaka na akawa mshindi kwa ufufuko wake kama anavyosema Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa “Victor quia victima” Kristo ni mshindi kwa sababu amekuwa ni sadaka. Ni mwaliko wa kusimamia ukweli, haki na amani na kukataaa kabisa propaganda. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Haki, Amani, Upendo na Mshikamano wa Kidugu.

Ekaristi Takatifu
17 March 2022, 17:06