Tafakari za Kipindi Cha Kwaresima 2022: Ushirika Wa Kiekaristi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 zinakita ujumbe wake kwenye Fumbo la Ekaristi Takatifu na kuchota utajiri wake kutoka katika sehemu hii ya Injili: “Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote; maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.” Mt 26: 26-28. Kumbe, kauli mbiu inayonogesha tafakari hizi ni: “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Hizi ni tafakari zinazotolewa kwa uwepo wa: Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Maaskofu, wasaidizi wake wa karibu, yaani “Curia Roma”, Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Magambera pamoja na wafanyakazi wa Jimbo kuu la Roma.
Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, Ijumaa tarehe 18 Machi 2022 alijikita zaidi kwenye maneno ya Kristo Yesu aliyesema: “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Liturujia ya Ekaristi Takatifu ni kiini cha maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Kuna uhusiano kati ya Ekaristi Takatifu na Berakah ya Wayahudi. Kristo Yesu ni Kuhani na Sadaka inayotolewa, yaani Mwili na Damu yake Azizi, sadaka safi inayotolewa kwa Baba wa milele kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake, wewe Mungu Baba Mwenyezi katika umoja wa Roho Mtakatifu unapata heshima na utukufu wote, daima na milele. Kardinali Cantalamessa katika tafakari yake, Ijumaa tarehe 25 Machi 2022 amekazia kuhusu ushiriki kama sehemu ya kiri ya ushirika wa Kisakramenti unaopewa kipaumbele cha kwanza kuliko hata hierarkia ya Kanisa. Huu ni ushirika na Kristo Yesu, Fumbo la Utatu Mtakatifu na Ushirika kati ya Waamini unaowasukuma kujenga ushirika na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hakuna tofauti ya ushiriki unaofanywa wakati wa kupokea Ekaristi Takatifu kwani wote ni sawa. “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.” 1Kor 10:16-17.
Mtakatifu Paulo katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu anazungumzia Mwili wa Kristo katika maana yake halisi, yaani mwili ulioteseka, ukafa na hatimaye kufufuka. Na sehemu ya pili ni Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kumbe, waamini wanaokula na kunywa Mwili na Damu yake Azizi wanakuwa ni sehemu ya ushirika na Kristo Yesu na hivyo kuwa ni Mwili mmoja na Kristo Yesu kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo: “Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye.” 1Kor 6:17. Huu ni ushiriki wa waamini unaopania kujenga na kudumisha ushirika wao kama ilivyo hata pia katika maisha ya ndoa na familia. Rej. Efe 5: 31-33. Kumbe, heri yao wanaoalikwa kwenye karamu ya Mwanakondoo. “Beati qui ad coenam Agni vocati sunt.” Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kukuza na kudumisha utakatifu wa maisha, ili waweze kufanana na Kristo Yesu katika maeno, lakini zaidi katika matendo yao adili. Waamini wanamshiriki Kristo Yesu kwa haki, lakini Yesu anashiriki pamoja nao kwa njia ya neema.
Ushirika katika Fumbo la Ekaristi Takatifu unawawezesha waamini kushiriki katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kujenga na kudumisha ushirika kama Kristo Yesu katika ile Sala yake ya Kikuhani anakazia ushirika kama kielelezo cha ushuhuda, ili watu waweze kuamini na hatimaye, kuokoka na kwamba, Kristo Yesu ni ufunuo wa Baba wa milele. Rej. Jn: 17:23, 14:9. Ni katika kipindi cha Mageuzi, Roho Mtakatifu anapovitakatifuza vipaji na kuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni zawadi ya Utatu Mtakatifu, Ekaristi Takatifu inayoadhimishwa kila siku kama Pasaka ya Bwana na ni kielelezo cha Pentekoste inayoadhimishwa pia kila siku, ili kujenga na kuimarisha ushirika wa Kanisa. Ushirika wa Fumbo la Ekaristi Takatifu na maskini ni mwaliko kwa waamini kujisadaka na kujimega katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama yanavyofafanuliwa na Kristo Yesu kwenye Hukumu ya mwisho Mt 25: 1-46. Ekaristi Takatifu, iwawezeshe waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Leo hii kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kuna akina Lazaro wengi wanaoteseka na kufa kwa baa la njaa duniani na utapiamlo wa kutisha, wakati ambapo kuna watu wanakula na kusaza kwa kufuru!