Tafuta

Siku ya Wanawake Duniani 2022: Kauli mbiu: Wanawake, Migogoro na Ustahimilivu. Siku ya Wanawake Duniani 2022: Kauli mbiu: Wanawake, Migogoro na Ustahimilivu. 

Siku ya Wanawake Duniani 2022: Wanawake, Migogoro na Ustahimilivu

Umekuwa ni mkutano wa kiekumene, kidini na kidiplomasia uliowaunganisha wawakilishi 400 wa Jumuiya za Wanawake kutoka katika nchi 70. Mkutano umeratibiwa na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini kwa kushirikiana kwa karibu sana na Shirikisho la WUCWO, UMOFC. Kauli mbiu ya maadhimisho haya imekuwa ni: “Wanawake, Migogoro na Ustahimilivu.” Yaani we acha tu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2022, tarehe 4 Machi 2022 limefanya mkutano kwa njia ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Hii pia imekuwa ni fursa kama sehemu ya kumbukizi la miaka 111 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho hili. Umekuwa ni mkutano wa kiekumene, kidini na kidiplomasia uliowaunganisha wawakilishi 400 wa Jumuiya za Wanawake kutoka katika nchi 70 ulimwenguni. Mkutano umeratibiwa na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini kwa kushirikiana kwa karibu sana na Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC. Kauli mbiu ya maadhimisho haya imekuwa ni: “Wanawake, Migogoro na Ustahimilivu.” Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, M.C.C.I, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini anasema, katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kufahamiana, kuheshimiana na kushirikiana kwa dhati katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Bikira Maria ni Mfano Bora wa Kuigwa na wanawake wote.
Bikira Maria ni Mfano Bora wa Kuigwa na wanawake wote.

Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano wa kidugu kati ya watu wa mataifa na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, linaendelea kukazia majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni na waamini wa dini mbalimbali duniani. Lengo ni kujenga na kudumisha umoja, udugu na urafiki kwa kusaidiana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kwa njia ya majadiliano ya kidini, watu wanakutana, wanazungumza, wanafahamiana na hivyo kuanzisha mchakato wa kutembea bega kwa bega kama ndugu wamoja. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuwa ni shuhuda na chombo cha amani, kwa kufyekelea mbali yale yote yanayosababisha: chuki, kinzani na mipasuko ya kidini, kiimani na kitamaduni. Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, amewapongeza wanawake kwa kuangalia migogoro na changamoto katika maisha yao kwa jicho la Bikira Maria, aliyeonesha ustahimilivu wa ajabu katika hija ya maisha yake hapa duniani, kiasi hata cha kuthubutu kusimama chini ya Msalaba na kupokea Maiti ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu.

Hata leo hii, wanawake wanaendelea kuonesha ustahimilivu wa hali ya juu na hasa kutokana na changamoto za janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Wanawake wamekuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa wale wote waliovunjika na kupondeka moyo. Wajumbe kutoka katika dini mbalimbali wamekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wanawake wajengewe uwezo wa kutambua na kusimamia haki zao msingi. Imekuwa ni fursa kwa wanawake kushirikishana changamoto wanazokabiliana nazo wanawake kutoka nchini Ukraine, ambao kwa sasa wako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Urussi iliyoivamia nchini yao kijeshi. Wanawake wanakabiliana na changamoto pevu za kulinda na kuwatunza watoto wao wadogo, wakati Baba zao wakiwa mstari wakiwa vitani kulinda nchi yao. Ni wanawake ambao wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika ujenzi wa matumaini, upendo na ujasiri.

Maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yameacha madhara makubwa kwa wanawake wengi duniani, lakini kwa namna ya pekee Afrika ya Kusini. Kumbe, huu ni wakati kwa wanawake kusimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya familia zao. Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani limebaianisha kwamba, Wanawake Amerika ya Kusini na Caribbean wameathirika sana kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kimsingi washiriki wa mkutano huu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, wamekazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wanawake wawe ni vyombo na mashuhuda wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu na urafikii wa kijamii ili kujenga upendo jamii na mafungamano ya kijamii.

Haki msingi, utu na heshima ya wanawake ilindwe.
Haki msingi, utu na heshima ya wanawake ilindwe.

Kwa upande wake, Bi María Lía Zervino, Rais Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC amekazia umuhimu wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.” Anasema, mahusiano na mafungamano ya kimataifa yanaweza pia kuangaliwa kwa njia ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanayozingatia haki msingi za binadamu pamoja na diplomasia ya kimataifa. Amani ya kweli inafungamana na wajenzi wa amani duniani; haki msingi za binadamu zinatekelezwa kwa kuangalia mahitaji msingi ya watu kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, mfano bora wa kuigwa. Udugu wa kibinadamu unakita mizizi yake katika umoja na ushirikiano. Kwa njia ya utamaduni wa udugu wa kibinadamu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia dhana ya upendo kwa watu wote, ili kujenga mahusiano, sheria, kanuni na taratibu zinazopania kudumisha amani na kuboresha maisha ya watu wote wa Mungu katika ujumla wao.

Bi María Lía Zervino kwa namna ya pekee, amewapongeza wanawake Barani Afrika kwa ustahimilivu wao na kuendelea kusimama kidete kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Wanawake wengi wamekuwa wakikabiliana na mfumo dume, hali ya kutengwa na kunyanyaswa bila kusahau ukatili wa majumbani. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Itakumbukwa kwamba, kauli mbiu iliyochaguliwa na Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2022 ni “Usawa wa Kijinsia wa leo kwa Maendeleo ya kesho.” Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kukuza na kudumisha usawa katika mazingira ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ikumbukwe kwamba, vita na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo.

Siku ya Wanawake duniani
08 March 2022, 16:53