Miaka 40 Ya Uhusiano Wa Kidiplomasia Kati ya Vatican na Uingereza
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ilikuwa ni tarehe Mosi Aprili 1980 Bwana Mark Evelyn Heath alipowasilisha Hati zake za Utambulisho kutoka kwa Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kama Balozi wa kwanza wa Uingereza mjini Vatican. Huu ukawa ni mwanzo wa mahusiano na ushirikiano wa Kimataifa kwa karibu zaidi kati ya Vatican na Uingereza. Hili ni tukio ambalo lilifungua mlango wa matumaini ndani na nje ya Uingereza kwa kuziba ukimya uliokuwepo kati ya Vatican na Uingereza kwa miaka zaidi ya 400. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Augustino wa Canterbury aliyezaliwa mjini Roma, Italia, 13 Novemba 534 akafariki dunia Canterbury, nchini Uingereza, 26 Mei 604 ndiye aliyekuwa mmonaki aliyetumwa na Papa Gregori I kama Askofu mmisionari nchini Uingereza kunako mwaka 597. Anaheshimiwa na Kanisa Katoliki, Waorthodox na Waanglikan kama Mtakatifu na "Mtume wa Uingereza.” Ni katika kumbukizi la maadhimisho ya Miaka 40 tangu Uingereza na Vatican zilizopoanzisha uhusiano wa kidiplomasia, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne tarehe 29 Machi 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma.
Hili ni Kanisa ambalo limetembelewa mara nyingi na Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza katika kipindi cha 70 ya utume wake kwa watu wa Mungu nchini Uingereza na Jumuiya ya Madola katika ujumla wake. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 28 Mei 1982 akatembelea Uingereza na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Westminster. Kardinali Pietro Parolin katika mahubiri yake hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima amekazia umuhimu wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa Maisha ya watu wa Mungu. Kuendeleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuzama na kushangaa matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Huu ni muda muafaka wa kujipatanisha na Mungu, Jirani na Mazingira nyumba ya wote sanjari kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu; utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Mkazo ni ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, licha tofauti zao msingi, lakini binadamu wote wanaunda familia kubwa ya watu wa Mungu.
Lengo ni kuwajengea watu matumaini na ujasiri wa kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Ni mwaliko kwa waamini katika ujumla wao kuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Mama Kanisa anaendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu hadi miisho ya dunia. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo Yesu pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao. Rej. Gaudium et spes, 1. Ni matumaini ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwamba, kumbukizi la Miaka 40 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Uingereza na Vatican litaendelea kuimarisha na kuboresha amana na tunu msingi ambazo zimesimamiwa na nchi hizi mbili katika kipindi cha Miaka 40 iliyopita. Ibada hii ya Misa Takatifu umehudhuriwa na viongozi wakuu na Kanisa kutoka Vatican na Uingereza bila kusahau ujumbe kutoka Uingereza ulioongozwa na Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales.