Kard.Parolin amempigia simu Lavrov:”mapigano yasimamishwe”
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Pietro Parolin katibu wa Vatican na waziri wa mambo ya Nchi za nje wa Shirikisho la Urusi Bwana Serghei Lavrov wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu, tarehe 8 Machi 2022. Kadinali Parolin amesisitiza kile ambacho Papa Francisko alikuwa ameomba mara kadhaa, yaani kukomesha mapigano ya kivita. Na pia Kardinali ameonesha utayari wa Vatican kwa njia yoyote ile ya kuingilia kati katika njia ya upatanisho unaonekana kuwa muhimu sana katika wakati huu wa kuhamasisha amani.
Kwa mujibu wa msemaji wa Vyombo vya Habari Vatican, Dk. Matteo Bruni amethibitisha juu ya habari ya simu kwamba, Kardinali amewasilisha wasiwasi mkubwa wa Papa Francisko wa vita vinavyoendelea nchini Ukraine na akathibitisha kile ambacho Papa tayari alikuwa amesema siku ya Dominika iliyopita wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana. Kwa namna ya pekee alisisitiza wito wake wa kukomesha mashambulizi ya silaha na kuhakikisha kwamba mikondo ya huduma ya kibinadamu kwa raia na waokoaji iwezeshwe na ili nafasi ya vurugu za silaha zibadilishwe kuwa za mazungumzo. Kwa maana hiyo, akihitimisha simu hiyo, Kardinali Parolin amethibitisha tena nia ya Vatican ya kutaka kufanya kile kinachowezekana kujiweka katika huduma ya amani hiyo.
Habari kuhusu mazungumzo hayo ziliripotiwa na wakala wa Interfax wakinukuu Wizara ya Mambo ya nje ya Moscow. “Pande hizo zimeelezea matumaini kuwa duru ijayo ya mazungumzo kati ya Moscow na Kiev, ifanyike kwa haraka na ili kwamba makubaliano kuhusu masuala muhimu yafikiwe, kwa lengo la kusitisha uhasama” kwa mujibu wa vyanzo vya habari Urusi. Msemaji wa Lavrov ameeleza kuwa waziri huyo alimweleza Kardinali Parolin “kuhusu sababu za Urusi na malengo ya operesheni maalum ya kijeshi iliyofanywa nchini Ukraine”.
Lakini Dominika iliyopita, kama itakumbukwa vizuri, Papa Francisko alisisitiza kwamba kinachoendelea nchini Ukraine sio operesheni ya kijeshi, bali ni vita. Kwa maana hiyo “Msisitizo maalum kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje uliwekwa katika masuala ya kibinadamu hasa kuhusiana na mzozo huo, ikiwa ni pamoja na hatua za kulinda raia, mashirika ya misaada na utekelezaji wa njia za huduma za kibinadamu pamoja na usaidizi kwa wakimbizi.”