Askofu Sebastien Kenda Ntumba Wa Jimbo Katoliki Tshilomba, DRC.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, tarehe 25 Machi 2022 ameunda Jimbo Katoliki Tshilomba lililoko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kumteuwa Mheshimiwa Sana Padre Sebastien Kenda Ntumba kuwa Askofu wake wa kwanza. Jimbo Katoliki la Tshilomba limemegwa kutoka katika Jimbo Katoliki la Luiza na ni sehemu ya Jimbo kuu la Kananga, DRC. Hadi kuteuliwa kwake, Askofu mteule Sebastien Kenda Ntumba alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Anthony wa Padua nchini DRC. Askofu mteule Sebastien Kenda Ntumba wa Jimbo Katoliki Tshilomba alizaliwa tarehe 11 Juni 1960 huko Tshiona, Jimbo Katoliki la Luiza. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 9 Agosti 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre huko Tshibala. Katika maisha na utume wake kama Padre amewahi kuwa: Mlezi Seminari Ndogo, Paroko na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kichungaji Jimbo. Kati ya mwaka 2003 hadi mwaka 2016 alitekeleza dhamana na utume wake nchini Italia kama sehemu ya Mapadre wa Zawadi ya Imani “Fidei Donum” katika Jimbo kuu la Agrigento nchini Italia.
Baadaye akajiendeleza kielimu na hatimaye kujipatia Shahada ya Uzamili katika Masomo ya Taalimungu. Na kati ya Mwaka 2016 hadi mwaka 2017 akateuliwa kufundisha kwenye Seminari ya Jimbo kuu la Agrigendo. Kuanzia mwaka 2017 hadi kuteuliwa kwake, amekuwa ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Anthony wa Padua nchini DRC. Takwimu zinaonesha kwamba, Jimbo Katoliki la Tshilomba “Tshilombana” liko katika Wilaya ya Lomani na linaundwa na miji ya Tshilomba, Mwenye-Ditu pamoja na vitongoji vya Katshisungu, Kaninchini na Melundi vilivyoko katika eneo la Kandakanda. Kanisa la Parokia ya “St Jacques Tshilomba” limeteuliwa kuwa ndilo Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Tshilomba ambalo kwa sasa lina Parokia 27 zinazohudumiwa na Mapadre 76 wa Jimbo. Kimsingi Jimbo lina Mashemasi 4 na Waseminari wakuu 23. Kuna watawa wa kike 233 na wa kiume 6. Kuna Mashirika 2 ya Kitawa yenye hadhi ya Mashirika ya Kipapa. Jimbo la Tshilomba linahudumiwa na Makatekista 213. Linamiliki na kuendesha shule 249 na Taasisi za Afya ni 40.