Askofu Mkuu Lucius Iwejuru Ugorji wa Jimbo kuu la Owerri, Nigeria
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu mkuu Anthony John Valentine Obinna wa Jimbo kuu la Owerri nchini Nigeria la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu Lucius Iwejuru Ugorji wa Jimbo Katoliki la Umuahia kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo Katoliki la Owerri. Ataendelea pia kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Ahiara “Sede vacante et ad nutum Sanctae Sedis”, Yaani, Msimamizi wa Kitume, anayewajibika moja kwa moja na Vatican katika masuala yote ya uongozi wa Jimbo Katoliki la Ahiara nchini Nigeria. Siku chache tu baada ya kuteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Owerri, amechaguliwa pia kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria Catholic Bishops Conference of Nigeria (CBCN), na hivyo kuchukua nafasi ya Askofu mkuu Augustine Obiora Akubeze wa Jimbo kuu la Benin City ambaye amemaliza muda wake wa uongozi wa miaka minne.
Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Lucius Iwejuru Ugorji wa Jimbo kuu la Owerri alizaliwa tarehe 13 Januari 1952 huko Naze, nchini Nigeria. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 16 Aprili 1977 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 2 Aprili 1990 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa jimbo Katoliki la Umuahia, Nigeria na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 1 Julai 1990. Tarehe 19 Februari 2018, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Msimamizi wa Kitume anayewajibika moja kwa moja Vatican katika masuala yote ya uongozi wa Jimbo Katoliki la Ahiara, Nigeria. Tarehe 6 Machi 2022, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Owerri, Nigeria.