Tafuta

Askofu Christian Carlassare, Askofu wa Jimbo Katoliki la Rumbek, Nchini Sudan ya Kusini, tarehe 25 Machi 2022. Askofu Christian Carlassare, Askofu wa Jimbo Katoliki la Rumbek, Nchini Sudan ya Kusini, tarehe 25 Machi 2022. 

Askofu Christian Carlassare, M.C.C.I. Jimbo Katoliki la Rumbek

Askofu Christian Carlassare wa Jimbo Katoliki la Rumbek alizaliwa mwaka 1977. Tarehe 19 Desemba 2003 aliweka nadhiri za daima kwenye Shirika la Wamisionari wa Comboni wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Tarehe 4 Septemba 2004 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 8 Machi 2021, akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rumbek na kuwekwa wakfu tarehe 25 Machi 2022. Yaani

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema, Uaskofu ni utimilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre, ambamo Askofu aliyewekwa wakfu anapewa dhamana ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Askofu ni kielelezo cha ukuhani mkuu, kilele cha huduma takatifu. Askofu kwa namna iliyo ya juu kabisa, hushika nafasi ya Kristo Yesu mwenyewe, aliye mwalimu, mchungaji na kuhani na kwamba, Askofu anatenda kazi yake katika nafsi yake. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Askofu anafanywa mwalimu kweli na halisi wa imani, kuhani na mchungaji. Kardinali Gabriel Zubeir Wako, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Khartoum, Sudan Kongwe amewaongoza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Rumbek kumwomba Roho Mtakatifu ili amweke wakfu Askofu Christian Carlassare, M.C.C.I. wa Jimbo Katoliki la Rumbek, Sudan ya Kusini. Sasa yuko tayari kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa tarehe 25 Machi 2022 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa Habari ya Kuzaliwa kwa Bwana, yaani Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Kardinali Gabrieli Zuberi Wako amewataka waamini kutambua kwamba, Uaskofu ni huduma ya mambo matakatifu ya Mungu na wala si kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya mtu binafsi.

Tarehe 8 Machi 2021 alishambuliwa na watu wasiojulikana.
Tarehe 8 Machi 2021 alishambuliwa na watu wasiojulikana.

Amesema, aliwekwa wakfu kuwa Askofu kunako mwaka 1975 kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Ni dhamana, jukumu na wajibu wa waamini kulitegemeza Kanisa kwa rasilimali fedha, karama na muda wao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amemsifu na kumpongeza Askofu Christian Carlassare kwa kukubali na kulichagua Jimbo Katoliki la Rumbek, kama sehemu yake maalum ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Itakumbukwa kwamba, Askofu Christian Carlassare, M.C.C.I. wa Jimbo Katoliki la Rumbek, Sudan ya Kusini alizaliwa tarehe 1 Oktoba 1977 huko Schio, Jimbo Katoliki la Vicenza nchini Italia. Tarehe 19 Desemba 2003 aliweka nadhiri za daima kwenye Shirika la Wamisionari wa Comboni wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Tarehe 4 Septemba 2004 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 8 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rumbek, Sudan ya Kusini na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 25 Machi 2022 na Kardinali Gabriel Zubeir Wako, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Khartoum, Sudan Kongwe. Katika Ibada hii amesaidiana na Askofu mkuu Mstaafu Stephen Ameyu Martin Mulla wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini pamoja na Askofu Matthew Remijio Adam Gbitiku, M.C.C.I. wa Jimbo Katoliki la Wau. Ibada hii imehudhuriwa pia na Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria van Megen, Balozi wa Vatican nchini Kenya, Sudan ya Kusini na Mwakilishi wa Vatican kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 14 Machi 2022 alikutana na kuzungumza na Askofu Christian Carlassare, M.C.C.I. wa Jimbo Katoliki la Rumbek, Sudan ya Kusini aliyewekwa wakfu na kuwa Askofu tarehe 25 Machi 2022 pamoja na ujumbe wake. Baba Mtakatifu alimtia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Rumbek. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Christian Carlassare, M.C.C.I. wa Jimbo Katoliki la Rumbek, Sudan ya Kusini, aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Machi 2021, lakini kabla ya kuwekwa wakfu, alishambuliwa na hatimaye, kulazwa kwa matibabu zaidi, Nairobi nchini Kenya. Askofu Christian Carlassare, anatumainia kwamba, madonda yake yatasaidia kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Rumbek, Sudan ya Kusini. Kipindi cha mwaka mzima, cha kusubiri kabla ya kuwekwa wakfu, imekuwa ni fursa pia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kwa watu wa Mungu kuweza kupokea Habari Njema ya Wokovu, kwa ari na moyo mkuu. Hii ni fursa ya kujenga na kudumisha Jumuiya iliyokomaa, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano.

Mwanzo mpya katika maisha na utume wa Askofu Jimbo Katoliki la Rumbek.
Mwanzo mpya katika maisha na utume wa Askofu Jimbo Katoliki la Rumbek.

Askofu Christian Carlassare, M.C.C.I. anakiri kwamba, kipindi hiki cha mwaka mmoja, kimemwezesha katika hali ya wasi wasi wa magonjwa na kifo, kujifunza zaidi kunyenyekea na kujiaminisha na kuendelea kushirikiana na Mwenyezi Mungu, tangu siku ile aliposhambuliwa na watu wasiojulika hadi wakati huu anapojiandaa kuwekwa wakfu kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Rumbek. Anasema, huu ni wakati wa ujenzi wa Kanisa linaloangalia mahitaji msingi ya waamini wake na dunia katika ujumla wake. Ni wakati wa ujenzi wa umoja, ushiriki na utume, kwa kuunganisha nguvu kwa pamoja. Askofu Christian Carlassare, M.C.C.I. wa Jimbo Katoliki la Rumbek, alimshukuru na kumpongeza Askofu Matthew Remijio Adam Gbitiku, M.C.C.I wa Jimbo Katoliki la Wau, Sudan ya Kusini kwa kusimamia vyema Jimbo Katoliki la Rumbek tangu Mwezi Mei 2021. Muda wote huu, ameonesha kuwa ni kiongozi aliyekita nguvu na matumaini yake kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Analishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan kwa mshikamano karika urika wao. Kwa namna ya pekee kabisa, anapenda kuwashukuru watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Rumbek na Sudan ya Kusini katika ujumla wao, kwa kumpokea kama kiongozi wao wao tayari kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza kama Askofu mahalia. Kwa vile amewekwa wakfu wakati wa Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa Habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, tangu sasa anaonja upendo, ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika maisha na utume wake, changamoto ya kutembea kama Kanisa lenye utume wa kinabii.

Askofu Rumbek
27 March 2022, 15:45