Ungamo la dhati kutoka ndani ya moyo
ANDREA TORNIELLI
Kama alivyoahidi, hatimaye Benedikto XVI amezungumza. Amezungumza kama Mkristo. Mkristo mwenye umri wa karibu miaka tisini na tano, ambaye anaishi miaka ya mwisho ya maisha yake marefu akizidi kudhoofika mwilini mwake, akiwa na sauti dhaifu na akili timamu, na ambaye kwa mara nyingine amejikuta katikati ya shutuma na mabishano. Jibu fupi na la kutoka moyoni mwake linatokana na mtazamo wake wa kina wa imani. Ratzinger alipata msukumo wa “maungamo” yake ya kibinafsi na ya kusisimua kutokana na tendo la toba la Misa ya kila siku. Mwanzoni mwa kila liturujia ya Ekaristi, mshereheshaji na waamini hurudia “mea culpa”, yaani “nimekosa mimi” wakimalizia kwa maneno “Nimekosa sana”.
Ni ufahamu wa kuwa wakosefu na hivyo kuhitaji kuomba huruma na msamaha. Huu ni mtazamo wa kutubu ulio mbali na ule imani ya ushindi unaolichukulia Kanisa kuwa ni nguvu ya kidunia, na kutokana na mtindo wa ushirika ambao unaopunguza maisha yake kuwa shirika, muundo na mikakati. Mtazamo ulio mbali na mtazamo ulioenea wa kuhukumu wengine kila wakati na makosa yao, badala ya kujiuliza juu yao mwenyewe.
Joseph Ratzinger akiwa kama Mwenyekiti wa awali wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, mwanzoni mwa milenia mpya alipambana dhidi ya unyanyasaji kwa upande wa makleri. Akiwa Papa alitangaza sheria kali sana za kupambana na balaa hili la kuchukiza. Lakini katika barua yake hakumbuki wala hadai chochote kati ya hayo yote. Siku zilizofuata baada ya kuchapishwa kwa ripoti hiyo zilikuwa fursa kwake kwa ajili ya “uchunguzi wa dhamiri” na “tafakari” yake binafsi kuhusu kile kilichotokea. Papa Mstaafu anasema kwamba alitazama machoni mwa matokeo ya hatia kubwa sana” katika kukutana na wale ambao wamenyanyaswa, na kwamba alijifunza kuwa “sisi wenyewe tunaingizwa kwenye hatia hii kubwa sana tunapoipuuza au tusipo kabiliana nayo kwa uamuzi unaohitajika na wajibu, kama ilivyotokea na hutokea mara nyingi sana”.
Inaoneesha “aibu kubwa”, “maumivu makubwa” na “ombi la dhati la msamaha” kwa sababu ya nyanyaso na makosa yote, hata kwa yale yaliyotokea wakati akiwa katika mamlaka kwenye maeneo husika ambapo alihudumia, huko Ujerumani na Roma. Yeye anaandika, bila kujiondoa kuwa yeye mwenyewe anahisi changamoto kwa mtazamo wa wale ambao bado wanadharau jambo hilo leo hii, yaani na wale wanaolala, kama vile mitume walivyolala kwenye Mlima wa Mizeituni, wakimuacha Yesu peke yake kuomba na kutokwa jasho la damu mbele ya shimo la dhambi. Kutokana na hilo anawaomba “kaka na dada” zake wamwombee.
Hayo ya Benedikto XVI katika barua hiyo ni maneno ya mtu mzee asiye na ulinzi, ambaye sasa anahisi yuko karibu kukutana na Mungu na ambaye jina lake ni huruma. Haya ni maneno ya “mtenda kazi mnyenyekevu katika shamba la mizabibu la Bwana” ambaye anaomba msamaha kwa dhati bila kukwepa uthabiti wa matatizo na anaalika Kanisa zima kuhisi jeraha kama lao binafsi linalovuja damu ya nyanyaso.