Tafuta

Mkataba wa Lateran kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Italia ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu. Mkataba wa Lateran kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Italia ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu. 

Kumbukizi la Mkataba wa Lateran Miaka 93 ya Nchi ya Vatican: Diplomasia

Mkataba huu ulitoa uhuru kwa Kanisa Katoliki nchini Italia kuweza kujiamria mambo yake bila kuingiliwa na Serikali. Huu ni msingi wa uhuru wa kuabudu. Vatican ikapewa mamlaka kamili ya kujisimamia yenyewe katika shughuli zake na Serikali ya Italia. Mkataba huu, uliiwezesha Vatican “Kiti Kitakatifu-Holy See” kuwa na uhuru kamili kuhusiana na masuala ya dini, imani na maadili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 11 Februari 2022 inabeba matukio mazito katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni Siku ya Kumbukizi la Mkataba wa Lateran uliotenganisha Kanisa na Serikali ya Italia. Pili ni kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 30 ya Wagonjwa Duniani inayoongozwana na kauli mbiu “Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Lk. 6:36: Kusimama karibu na wale wanaoteseka ni njia ya upendo.” Hii ni Siku ya Sala na Tafakari kuhusu Fumbo la Mateso. Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipotangaza kung’atuka kutoka madarakani kutokana na hali yake ya afya kuanza kudhorota. Walimwengu wakapigwa bumbuwazi. Tumkumbuke katika sala na sadaka zetu ili katika uzee wake, aendelee kuliombea Kanisa la Kristo Yesu. Vatican ni kati ya nchi ndogo kabisa duniani, tarehe 11 Februari, 2022 inatimiza miaka 93 tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana saini Mkataba na Serikali ya Italia “Inter Sanctam Sedem e Italiae Regnum Conventiones” kwa kifupi “Patti Lateranensi” yaani “Mkataba wa Lateran.” Hii ni Italia iliyokuwa inaibuka baada ya kutenganisha shughuli za Kanisa na Serikali ya Italia. Kardinali Pietro Gasparri, Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati huo kwa niaba ya Kanisa pamoja na Bwana Benito Mussolini, Waziri Mkuu wa Italia kwa niaba ya Serikali ya Italia, walitiliana saini Mkataba wa Lateran maarufu kama “Patti Lateranensi”.

Mkataba huu ulikuwa na sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuhitimisha kinzani na mpasuko uliokuwa umejitokeza baada ya Serikali ya Italia kuvamia mji wa Roma kunako mwaka 1870. Mkataba huu ulitoa uhuru kwa Kanisa Katoliki nchini Italia kuweza kujiamria mambo yake bila kuingiliwa na Serikali. Huu ni msingi wa uhuru wa kuabudu. Vatican ikapewa mamlaka kamili ya kujisimamia yenyewe katika shughuli zake na Serikali ya Italia, tangu wakati huo ikatambua uhuru na mamlaka ya mji wa Vatican hata katika udogo wake. Mkataba huu, uliiwezesha Vatican “Kiti Kitakatifu-Holy See” kuwa na uhuru kamili kuhusiana na masuala ya dini na imani. Sehemu ya Pili ya Mkataba huu, uliitaka Serikali ya Italia kulipa fidia kwa Vatican kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na Serikali wakati wa kuvamia mji wa Roma ambao ulikuwa ni ngome ya Kanisa Katoliki, kunako mwaka 1870. Serikali ikailipa Vatican fidia. Sehemu ya tatu ya Mkataba huu ni kuhusu “Makubaliano ya Kifedha” “Convenzionale Finanzarie”. Huu ni utaratibu na kanuni zinazoratibu mchakato wa mahusiano ya ndani kati ya Serikali ya Italia na Kanisa Katoliki nchini Italia. Katika sehemu hii, Maaskofu walipaswa kula kiapo cha utii kwa Serikali. Na Serikali kwa upande wake, ikalipatia Kanisa upendeleo wa kufundisha dini na kumwilisha Mafundisho tanzu ya Kanisa katika maisha ya hadhara.

Kumbukizi la Miaka 93 ya Mkataba wa Lateran
Kumbukizi la Miaka 93 ya Mkataba wa Lateran

Serikali ya Italia ikatambua Sakramenti ya Ndoa na utenguzi wake kufanyika kwenye Mahakama za Kanisa. Mkataba wa Lateran uliifanya Vatican kutambuliwa rasmi kama nchi huru yenye uwezo wa kujiamria mambo yake yenyewe katika medani za kimataifa bila kuingiliwa na Serikali ya Italia. Papa Pio XI alilitaka Kanisa kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Italia: kiroho na kimwili; kwa kutumia amana na utajiri wake wa kihistoria, kitamaduni na kisanaa; mambo yanayofumbatwa katika Ukristo. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuihakikishia Italia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili kweli nchi ya Italia, iendelee kuwa aminifu kwa Mapokeo pamoja kupyaisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu ambao umeipambanua Italia kwa miaka mingi. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni katika hotuba yake elekezi kwenye Kongamano la kitaifa lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko Roma na kuongozwa na mada “Umuhimu wa Vatican katika muktadha wa Jumuiya ya Kimataifa 1929 – 2019”, alikazia: uhuru wa kuabudu, uhuru wa kidini, utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Amesema, hizi ni changamoto ambazo zimepewa kipaumbele cha pekee na Vatican katika kipindi cha zaidi ya miaka 90 ya uwepo na utume wake.

Vatican imekazia umuhimu wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu dhamiri nyofu za watu, mahali patakatifu sana katika maisha ya mwanadamu! Ikumbukwe kwamba, Haki msingi za binadamu zinazozungumziwa hapa ni zile zinazofafanuliwa katika Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na wala si ukoloni wa kiitikadi unaotaka kupenyezwa kwa mataifa maskini duniani! Kardinali Parolin, alitumia fursa ya mkutano huu, kufafanua vipengele mbali mbali vilivyomo kwenye Mkataba wa Lateran kwa kusema, kwamba, Mkataba huu, umekuwa ni ngome na ulinzi thabiti kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kuweza kutekeleza dhamana na utume wake kwa uhuru zaidi, bila kuingiliwa na chombo chochote kile! Dhamana na wito wa Vatican katika diplomasia, unafumbatwa katika utume wake wa maisha ya kiroho, kimaadili na utu wema kwa ajili ya familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Vatican haipendi kuingilia mambo ya ndani ya nchi, bali inapenda kusikilizwa kwa makini, kama chombo cha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, dhamana inayotekelezwa kwa unyoofu na unyenyekevu mkuu!

Itakumbukwa kwamba, Mkataba wa Lateran, ulifanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984 wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kuendana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizokuwa zimeibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican. Ushirikiano kati ya Serikali ya Italia na Vatican unaolenga kulinda, kudumisha na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mkataba unaojipambanua kwa kukazia uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Nchi ya Vatican inapaswa kuendelea kuwepo, ikiwa huru katika kujiamria mambo yake yenyewe, ili kutekeleza utume wake katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili ulimwenguni kote. Mifumo ya kisiasa na sera mbali mbali zinazogusa utu, heshima na maisha ya mwanadamu na hata wakati mwingine kuzama katika undani wake. Vatican imekuwa mstari wa mbele kukemea uhuru usiokuwa na mipaka wala uwajibikaji; imekazia majadiliano katika ukweli na uwazi na mshikamano wa kidugu. Vatican ni kati ya nchi ambazo ziko mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu, kama mtu mmoja mmoja au taifa. Zote hizi ni kati ya sababu ambazo zinahalalisha uwepo wa Nchi ya Vatican ili iweze kutekeleza majukumu yake katika misingi ya ukweli, haki na uwazi.

Vatican inashiriki kikamilifu katika diplomasia ya Kimataifa
Vatican inashiriki kikamilifu katika diplomasia ya Kimataifa

Vatican kutokana na ushiriki wake kwenye Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kutoa mchango mkubwa unaofumbata maendeleo fungamani binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, uhuru wa kuabudu na ule wa kidini unazingatiwa na kuheshimiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Mama Kanisa anapenda kutekeleza wajibu na utume wake akiwa huru kabisa, ili kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uhuru wa kidini ni haki ya kila dini au dhehebu lolote lile kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za nchi husika. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamekazia umuhimu wa Kanisa na Serikali kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu: kiroho na kimwili. Uhusiano kati ya Kanisa na Serikali unategemea kwa kiasi kikubwa: hali ya kitamaduni, kijamii, kisiasa na kihistoria kwa nchi husika. Mahali ambapo utawala wa sheria unaheshimiwa, Kanisa limekuwa likitekeleza wajibu kwa ajili ya maendeleo ya watu kiroho na kimwili. Lakini, katika baadhi ya nchi, Kanisa limekuwa likikumbana na madhulumu na sera za kibaguzi zinazolibeza Kanisa kwa kudhani kwamba, linaingilia mambo yake. Kanuni ya mpe Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu inapaswa kuwaongoza wanasiasa wenye misimamo mikali ya maisha.

Kanisa, daima limeendelea kusoma alama za nyakati na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anapaswa kutekeleza dhamana na utume wake katika mazingira huru kabisa. Kamwe, Khalifa wa Mtakatifu Petro, hatasita kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki msingi za wakimbizi na wahamiaji pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Biashara haramu ya silaha duniani, biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyavalia njuga katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Mkataba wa Lateran
11 February 2022, 14:34