Miaka 54 ya Maisha na Utume wa Jumuiya ya Mt. Egidio: Sala, Maskini na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Professa Andrea Riccardi, akiwa kijana mbichi bado, hapo tarehe 7 Februari 1968, yaani miaka 54 iliyopita alianzisha Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma na kujikita katika mambo makuu matatu yaani: Sala, Maskini na Amani duniani. Kanisa kuu la Bikira Maria wa Trastevere yakawa ni makao makuu ya sala, maisha na utume wao sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni mchakato unaopaswa kujikita kwa namna ya pekee kabisa katika Tafakari ya Neno la Mungu na kuendelea kusoma alama za nyakati ili kukuza na kudumisha utandawazi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu na maisha ya kiroho unaofumbatwa katika mtazamo wa Uso wa huruma ya Mungu. Jumuiya hii inapaswa kuwa na ari na mwamko mpya zaidi wa Kiinjili ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kuwa na moyo wazi kwa wote bila ubaguzi kwa kisingizio cha uadui, ili kuendeleza maisha hadi kufikia utimilifu wake! Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 11 Machi 2018 kama sehemu ya mwendelezo wa Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ambayo imeenea sehemu mbalimbali za dunia.
Baba Mtakatifu alikazia karama ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inayofumbatwa katika: Sala, Maskini na Amani; karama ambayo imeendelea kukua na kukomaa katika kipindi cha miaka zaidi ya hamsini iliyopita. Changamoto iliyoko mbele yake kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, wanaiwekeza ili iweze kuzaa matunda mengi zaidi ili kung’oa hofu, mashaka na hasira dhidi ya wakimbizi, wahamiaji na wageni, maskini na watu ambao wanaotofautiana nao kwa sababu mbalimbali. Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, tarehe 10 Februari 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran kama sehemu ya kumbukizi la miaka 54 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao makuu yake mjini Roma. Imekuwa ni fursa ya kukutana tena na wanajumuiya ya Mtakatifu Egidio ambao kwa muda wa miaka 54 wametembea kwa pamoja katika sera na mikakati ya haki, amani na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa muda wa miaka 54, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imejipambanua katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii katika nchi 70. Hawa ni maskini, wakimbizi, wahamiaji, wahanga wa biashara ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo.
Hii ni Jumuiya ambayo imeendelea kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wanyonge; pamoja na kusoma alama za nyakati. Misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu inaendelea kupewa kipaumbele cha pekee na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, mambo ambayo yanafumbiwa macho kwenye sera na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa. Ni Jumuiya ambayo inaendelea kujielekeza katika umwilishaji wa ndoto ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili hatimaye, kuondokana na Vita Baridi inayotishia amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Udugu wa kibinadamu usaidie mchakato wa ujenzi na huduma kwa watu wote wa Mungu. Kardinali Gualtiero Bassetti amekazia huduma inayochota utajiri wake kutoka katika: Neno la Mungu, linalomwilishwa katika Sala na huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko wa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu katika mchakato wa ujenzi wa udugu na urafiki wa kibinadamu. Katika maisha na utume wao, watu wa Mungu kamwe wasichoke “kuchakarika” katika ujenzi wa amani duniani na kamwe wasiogope, kwa kuna umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali dunia wanatumainia kupata huduma hii makini na kwamba, Mwenyezi Mungu katika shida, magumu na changamoto za maisha ataendelea kuwalinda na kuwategemeza.
Katika Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake, Baba Mtakatifu Francisko aliitaka Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iwe ni mahali pa kukuza na kudumisha karama hizi kwa ajili ya kuendeleza maisha hadi utimilifu wake. Wanachama wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio wanapaswa kutambua kwamba, safari ya maisha na utume wao kwa siku za usoni inaambatana na Kanisa, kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mababa wa Mtaguso wanakaza kusema, ilimpendeza Mwenyezi Mungu kuwatakatifuza na kuwaokoa watu, siyo mmoja mmoja na pasipo muungano kati yao, bali kwa kuwaunda kama taifa moja, lenye kumjua katika ukweli na kumtumikia kitakatifu. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yanayojikita katika ujumbe na roho yake! Neno la Mungu linapaswa kuwa ni dira, mwongozo na taa inayoangazia mapito yao, kwa kuwalinda dhidi ya vishawishi vya sera na mikakati mamboleo; Neno la Mungu limewaokoa kutoka katika hofu na mashaka, kumbe, Jumuiya ijitahidi daima kupenda: kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wake. Neno la Mungu ni chemchemi ya huruma na faraja kwa maskini, wahanga wa vita na majeruhi katika maisha! Neno la Mungu liwasaidie wanajumuiya kusonga mbele kwa imani na matumaini, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati, tayari kumwilisha imani katika matendo, changamoto na mwaliko kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iwe ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu na katika maisha ya kiroho dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayowatenga na kuwanyanyasa maskini; na kwamba, kwa sasa tofauti kati ya watu inakuwa ni chanzo cha kinzani na uhasama. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma; wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja wa binadamu, kati ya watu wa mataifa, familia na tamaduni zao. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iendelee kushikamana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuwapatia nafasi ya kwenda katika shule ya amani! Wawe karibu sana na wazee wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, lakini kwao wawe ni marafiki bila kusawahau waathirika wa vita, njaa na magonjwa. Baba Mtakatifu alikaza kusema, maskini wawe ni amana na utajiri wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, kwani wote ni wa Kristo, dira na mwongozo wa kuyaangalia ya mbeleni kwa ari na moyo mkuu, wakijitahidi kudumu katika sala, huduma kwa maskini pamoja na kutafuta ili hatimaye kuendeleza amani duniani!