Tafuta

Kuanzia tarehe 17-19 Februari 2022 kunafanyika Kongamano la Kimataifa Kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre. Kuanzia tarehe 17-19 Februari 2022 kunafanyika Kongamano la Kimataifa Kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre.  

Kongamano Kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre: Mada Kuu: Wito

Ni fursa kwa wanataalimungu kupembua tema msingi za maisha na wito wa kipadre kadiri ya Mapokeo ya Kanisa na mielekeo mipya katika ulimwengu mamboleo. Ni Kongamano linalojadili kuhusu: Fumbo la Utatu Mtakatifu, Utume na Sakramenti ya Daraja Takatifu. Washiriki wanayo nafasi pia ya kudadavua kuhusu “Useja, Karama na Tasaufi ya maisha na wito wa Kipadre”. Utakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Marc Armand Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu anasema kuanzia tarehe 17-19 Februari 2022 kunafanyika Kongamano la Kimataifa Kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre. Ni fursa kwa wanataalimungu na wataalam kupembua kwa kina na mapana tema msingi za maisha na wito wa kipadre kadiri ya Mapokeo ya Kanisa na mielekeo mipya katika ulimwengu mamboleo. Ni Kongamano linalojadili kuhusu: Fumbo la Utatu Mtakatifu, Utume na Sakramenti ya Daraja Takatifu. Sanjari na tema hizi, washiriki wanayo nafasi pia ya kudadavua kuhusu “Useja, Karama na Tasaufi ya maisha na wito wa Kipadre”. Katika ulimwengu mamboleo kumekuwepo na kinzani, migawanyiko na mitazamo inayotishia amani, ushirika na udugu wa kibinadamu mintarafu maisha na utume wa Mapadre. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa na kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Kuna haja ya kuwa na ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Kumbe, umoja, ushiriki na utume; upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Kardinali Marc Armand Ouellet anasema, katika maadhimisho ya Kongamano hili, wakleri, watawa na waamini walei, kwa pamoja wanatafakari na kuchambua kuhusu mahusiano na mafungamano yaliyopo kati yao. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa ni Takatifu kwa maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu anayetangazwa pamoja na Baba na Roho Mtakatifu kwamba ni peke yake mtakatifu, amelipenda Kanisa kama Bibiarusi wake, akajitoa mwenyewe kwa ajili yake ili alitakatifuze, akaliunganisha naye kama mwili wake, akalijazia kipaji cha Roho Mtakatifu, kwa utukufu wa Mungu!

Tema msingi za maisha na utume wa Kipadre zinajadiliwa
Tema msingi za maisha na utume wa Kipadre zinajadiliwa

Hivyo basi, watu wote wa familia ya Mungu wanaitwa kuwa ni watakatifu! Haya ndiyo mapenzi ya Mungu. Kristo Yesu ndiye chemchemi na utimilifu wa utakatifu wote! Waamini wanahimizwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu na wawe na matunda ya Roho Mtakatifu ili wafanywe watakatifu. Kutokana na udhaifu wa binadamu, waamini wanahitaji mara kwa mara kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanaendelea kudadavua kuhusu Fumbo la Kanisa kwa kusema, Wakristo wote wanaitwa na kuhamasishwa kushiriki utakatifu mmoja, kwa kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli; kwa kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa ni: mtii, fukara na mnyenyekevu wa moyo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa njia hii, wastahilishwe kushiriki utukufu wa Kristo! Familia yote ya Mungu inapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima. Ni wakati kwa waamini walei kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa.

Kardinali Marc Armand Ouellet anasikitika kusema kwamba, katika historia, maisha na utume wa Kanisa kumekuwepo na matumizi mabaya ya madaraka na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa. Kuna haja ya kufanya utafiti makini wa kihistoria na kitaalimungu ili kuweza kukabiliana fika na kashfa za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa, ambazo zimechafua maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho mbalimbali ya Sinodi yamegusia kuhusu changamoto ya Useja katika maisha na utume wa Mapadre. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wabatizwa wanakuwa mawe hai, ili kujenga nyumba ya kiroho na kuwa makuhani watakatifu na hivyo kushiriki ukuhani wa Kristo, utume wake wa kinabii na wa kifalme. Ubatizo hutoa sehemu katika ukuhani wa jumla wa waamini. Rej. KKK 1267-1270. Kongamano linataka kuzama zaidi katika dhana ya ukuhani wa jumla wa waamini unaowashirikisha watu wote wa Mungu katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Useja, Karama na Tasaufi ya maisha na wito wa Kipadre
Useja, Karama na Tasaufi ya maisha na wito wa Kipadre

Umoja, ushiriki na utume wa watu wote wa Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Injili ya Kristo Yesu iwe ni dira na mwongozo rejea katika majadiliano yanayopania kuwajengea uwezo wanawake kwani Kristo Yesu aliwajali na kuwathamini sana wanawake, akawapatia uhuru wa kushiriki katika maisha na utume wake, kiasi cha kuwafanya kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko, kiini cha imani na maisha ya Kanisa. Alijali na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu. Katika maadhimisho ya Kongamano hili, wanawake wanashiriki kikamilifu kama wataalam wawezeshaji na washiriki. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutembea kwa pamoja kama watoto wa Mungu, ili kuhamasisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa.

Kongamano Wito

 

17 February 2022, 15:45