Limezinduliwa shindano la kimataifa kwa ajili ya kuandaa Nembo ya Jubilei 2025
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tarehe 22 Februari 2022 wamezindua shindano la Kimataifa kwa ajili ya kuandaa Nembo ya Jubilei na hata uundaji wa Tovuti mpya kwa ajili ya Mwaka Mtakatifu 2025. Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari Vatican wanabainisha kuwa hili ni shindano la nembo rasmi itakayo wakilisha mwaka 2025, ambapo Kanisa linaadhimisha Mwaka wake Mtakatifu. Baada ya Jubile Kuu ya 2000, sasa imesalia miaka mitatu pekee yake ili kumalizika kwa miaka ishirini na mitano inayopita kati ya kila Jubilei ya kawaida.
Chaguo la nembo
Kwa maana hiyo Baba Mtakatifu Francisko alikuwa tayari ameliagiza Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya kuandaa Jubilei ya 2025 na maandalizi tayari yanaendelea. Miongoni mwa shughuli za kwanza zinazopaswa kufanywa ni chaguo la Nembo rasmi, inayoonesha utambulisho na mada maalum ya kiroho ya kila Mwaka Mtakatifu, ikiambata na maana ya kitalimungu ambamo uteuzi huu wa kihistoria unaendelezwa na kutimizwa. Katika barua ambayo Baba Mtakatifu Francisko alimwandikia Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya, baadhi ya mada muhimu zinapaswa kuwemo katika kutunga Nembo hiyo. Kauli mbiu ni “Mahujaji wa matumaini”, hakika ni kidokezo cha upendeleo ambacho kwa washiriki wataweza kupata msukumo zaidi katika kuwakilisha nembo hiyo.
Shindano ni kwa watu wote
Kutokana na hilo Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya limezindua shindano hili lililo wazi kwa watu wote kwa ajili ya kuunda Nembo rasmi ya Jubilei ya Mwaka 2025. Mtu yeyote anaweza kushiriki, kulingana na kukubalika kwa Kanuni, ambazo zina taarifa zote muhimu ili kuweza kuwasilisha kazi zao kwa kamati ya uteuzi. Taarifa hiyo inapatikana kwenye tovuti “iubilaeum2025.va/it/logo” ambapo hivi karibuni itawezekana kuweka faili la kidijitali ya kazi yako. Shindano hilo meanza leo Jumanne tarehe 22 Februari na litamalizika tarehe 20 Mei 2022.
Nembo kwa ishara uwakilisha ujumbe wa haraka
Katika Mwaka Mtakatifu wa 2000, kazi hiyo, ambayo sasa iliingia katika historia, ilichaguliwa ya msichana mwenye umri wa miaka 22, mwanafunzi wa taasisi ya sanaa. Nembo ya Jubilee kwa ishara huwasilisha ujumbe kwa njia ya haraka na inayofaa, na ni kielelezo cha ujumbe wa Kanisa ulimwenguni pote na mahitaji maalum ya kiroho ya watu wa zama zetu hizi, wanaopata faraja katika ujumbe huo, wakiongozwa na mada ya matumaini. Aidha, Nembo hiyo ithibitishe rasmi mipango, mawasiliano na matukio yatakayopendekezwa kwa ajili ya maandalizi na maadhimisho ya Jubilei ya 2025.