Tafuta

Kardinali Leonardo Sandri ametumia fursa hii kutoa wito wa amani kwa ajili ya Ukraine, inayotishiwa kuvamiwaz kijeshi na Urussi. Kardinali Leonardo Sandri ametumia fursa hii kutoa wito wa amani kwa ajili ya Ukraine, inayotishiwa kuvamiwaz kijeshi na Urussi.  

Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki: Wito wa Amani Ukraine

Anawaomba viongozi wa Makanisa ya Kikristo nchini Ukraine, kushikamana katika sala, ili kamwe ulimwengu usigeuke na kuwa ni uwanja wa kifo kutokana na maafa makubwa yanayoweza kusababishwa na vita. Watu wanateseka, kumbe, huu ni wakati wa kusutwa na dhamiri nyofu, ili kuitikia wito na kilio cha kuachana na vita, ili amani iweze kutawala katika akili na nyoyo za watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa Kwa Makanisa ya Mashariki, Ijumaa tarehe 18 Februari 2022 katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na wajumbe wa Baraza waliohitimisha mkutano wao wao 95 amekazia pamoja na mambo mengine, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Mwongozo wa Sheria za Kanisa Kuhusu Liturujia utolewe na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 6 Januari 1996. Hii imekuwa ni fursa ya ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana kama sehemu ya umwilisho wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kukazia: Umoja, Ushiriki na Utume. Hii ni changamoto inayopaswa kuelekezwa hata kwenye Makanisa mahalia. Miaka mia moja imegota tangu Papa Benedikto XV alipofariki dunia, muasisi wa Baraza la Kipapa Kwa Makanisa ya Mashariki, aliyelianzisha Mei Mosi 1917 na tarehe 1 Agosti 1917 akawaandikia ujumbe wa amani wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa akiwataka kujenga na kudumisha amani, ili kuepuka Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia akisema “Vita ni mauaji yasiyo na maana” “Inutile strage, frustra caedem.”

Wito wa amani nchini Ukraine
Wito wa amani nchini Ukraine

Ni katika muktadha huu, Kardinali Leonardo Sandri ametumia fursa hii kutoa wito wa amani kwa ajili ya Ukraine, inayotishiwa kuvamiwa kijeshi na Urussi. Anawaomba viongozi wa Makanisa ya Kikristo nchini Ukraine, kushikamana katika sala, ili kamwe ulimwengu usigeuke na kuwa ni uwanja wa kifo kutokana na maafa makubwa yanayoweza kusababishwa na vita. Tayari watu wa Mungu nchini Ukraine, wanateseka, kumbe, huu ni wakati wa kusutwa na dhamiri nyofu, kwa kuitikia wito na kilio cha kuachana na vita, ili amani iweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wachunguze na kupima dhamiri zao nyofu mbele ya Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, waweze kufanya maamuzi magumu na mazito ili kulinda na kudumisha amani. Kristo Yesu ni Mfalme wa kweli na uzima, Ufalme wake ni wa utakatifu na wa neema, Ufalme wa haki, mapendo na amani awasaidie kufanya maamuzi mazito kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hakuna kitu chchote kinachoweza kupotea kwa njia ya amani, lakini yote yanapotea na kutoweka kwa njia ya vita. Wana heri wenye kiu ya haki na amani, wanaojisadaka na kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali Sandri

 

18 February 2022, 16:17