Askofu mkuu Javier H. Corona Balozi wa Vatican: Congo na Gabon!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Februari 2022 ameteuwa Monsinyo Javier Herrera Corona, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Congo Brazzaville na Gabon na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu. Askofu mkuu mteule Javier Herrera Corona kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Mshauri katika Ubalozi wa Vatican. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Javier Herrera Corona alizaliwa tarehe 15 Mei 1968 huko Autlàn nchini Mexico.
Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 21 Septemba 1993 akapewa Daraja takatifu ya Upadre na kuingizwa katika Jimbo Katoliki la Autlàn nchini Mexico. Askofu mkuu mteule Javier Herrera Corona ana shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa. Alianza kutoa huduma katika diplomasia ya Kanisa kunako tarehe 1 Julai 2003. Na tangu wakati huo, amekwisha kutekeleza utume huu nchini Pakistan, Perù, Kenya, Uingereza pamoja na nchini Ufilippin.