Tafuta

Waraka wa Kiekumene: Askofu na Umoja wa Wakristo: Vademecum ya Kiekumene ya tarehe 12 Desemba 2020. Waraka wa Kiekumene: Askofu na Umoja wa Wakristo: Vademecum ya Kiekumene ya tarehe 12 Desemba 2020. 

Askofu na Umoja wa Wakristo: Vademecum ya Kiekumene

Waraka wa Kiekumene unaojulikana kama “Askofu na Umoja wa Wakristo: Vademecum ya Kiekumene”, Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo na Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, wanawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo na kuendelea kutembea pamoja katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2023.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, tarehe 12 Desemba 2020 lilichapisha Waraka wa Kiekumene unaojulikana kama “Askofu na Umoja wa Wakristo: Vademecum ya Kiekumene”. Lengo lilikuwa ni kuwaamasisha Maaskofu kudumisha upendo na udugu miongoni mwa Wakristo, kwa kutambua kwamba, wanawajibika kikamilifu kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene kwa sababu umoja wa wakristo ni changamoto inayotokana na asili ya Kanisa lenyewe kama Kristo Yesu alivyokazia katika Sala yake ya Kikuhani, ili wawe wamoja. Umoja wa Wakristo bado haujakamilika na hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Kanisa zima, kwa kutambua kwamba, Askofu ni kielelezo cha umoja wa Kanisa. Baraza hili la Kipapa katika Waraka huu, lilichapisha Vademecum ili kumwezesha Askofu kufanya mang’amuzi ya kina. Kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba, anasaidia kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa Katoliki kwa kutambua kwamba, umoja wa Wakristo ni changamoto kubwa kwa Wakristo Wakatoliki. Askofu ajitahidi kushiriki katika majadiliano ya kiekumene katika ngazi mbalimbali za uongozi, kwa kuwatetuwa viongozi wa shughuli za kiekumene tangu katika ngazi ya jimbo, taifa na kanda.

Askofu asaidie mchakato wa majiundo ya kiekumene miongoni mwa watu wa Mungu, ili waweze kushiriki kikamilifu. Majiundo na malezi haya yaanzie kwa waamini walei, waseminaristi, watawa na wakleri. Maaskofu wajitahidi kuragibisha majadiliano ya kiekumene kwa kutumia nyenzo, vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Kanisa Katoliki linazo njia mbalimbali za kuweza kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kiekumene hasa kwa kukazia uekumene wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika sala, toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo ni juhudi za kukuza na kudumisha umoja wa Wakristo kadiri ya imani ya Kanisa ili kuuendea utimilifu ambao Kristo Yesu anautaka kwa ajili ya Kanisa lake. Kanisa Katoliki lijitahidi kusoma alama za nyakati na kusikiliza kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kutoka kwa Kanisa kwa wakati huu. Mchakato wa majadiliano ya kiekumene unavuka uwezo na nguvu za kibinadamu. Ndiyo maana Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican waliweka tumaini lao lote katika sala ya Kikristo kwa ajili ya Kanisa, katika upendo wa Mungu Baba na katika nguvu ya Roho Mtakatifu. Rej. UR 24.

Kanisa Katoliki lishiriki kikamilifu kusali kwa ajili ya mahitaji ya watu wa Mungu ulimwenguni. Lijenge na kudumisha utamaduni wa “Lectio Divina.” Maana yake halisi ni “Masomo ya kimungu” yaani njia ya kutafakari Neno la Mungu katika hatua nne: Mosi, Kusoma, “Lectio”, Neno la Mungu kwa umakini na utii mkubwa kwa Neno la Mungu, ili kuweza kufahamu mambo msingi yanayofumbatwa katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu.Hatua inayofuata ni kuzama katika tafakari kwa msaada wa Neno la Mungu, kiasi kwamba, vile vifungu vya Maandiko Matakatifu vinakuwa ni sehemu ya sala. Hii ndiyo hatua ya Pili yaani: Kuwaza, “Meditatio”. Sehemu ya tatu ni Kusali “Orati”, hatimaye ni Kutafakari “Contemplatio”. Wakatoliki wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya sherehe na sikukuu za Kanisa na watakatifu ili kukuza na kudumisha uekumene wa damu. Watawa washirikishwe kikamilifu katika majadiliano ya kiekumene na kwamba, kuna haja ya kuendelea kujikita katika mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya utengano kati ya Wakristo.

Wakristo waendelee kujikita katika mchakato wa uekumene wa upendo kwa kutambua kwamba, Wakristo wote kwa njia ya Ubatizo wanashiriki: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo. Wanao wajibu na haki zao zinazopaswa kunogeshwa kwa njia ya majadiliano. Wakristo waendeleze utamaduni wa kukutana na ndugu zao katika Kristo Yesu kwa kushiriki katika matukio mbalimbali pale inapowezekana. Majadiliano ya ukweli yawasaidie kuufahamu Ukweli wenyewe ambao ni Kristo Yesu. Majadiliano ya kitaalimungu yaendelezwe na Kanisa katika ngazi mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa na wawe tayari kuupokea Ukweli. Lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, majadiliano ya kiekumene yanajikita katika uhalisia wa maisha ya Wakristo, katika shughuli za kichungaji, utume pamoja na ushirikianaji wa rasilimali mbalimbali kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika utume na katekesi makini.

Wakatoliki wajibidiishe katika kujenga ushirikiano mwema katika maisha ya Ndoa na Sakramenti za Kanisa. Lengo ni kuwawezesha Wakristo wote kushirikiana katika ujenzi wa uekumene wa huduma na ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, ambao pia unaweza kutumika kama msingi wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani. Na huu unaweza pia kuwa ni mwanzo wa majadiliano ya kiekumene katika tamaduni za binadamu. Ni katika muktakdha wa Waraka wa Kiekumene unaojulikana kama “Askofu na Umoja wa Wakristo: Vademecum ya Kiekumene”, Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo chini ya uongozi wa Kardinali Kurt Koch na Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, wanawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo na kuendelea kutembea pamoja katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2023.

Sinodi hii, inanogeshwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Ikumbukwe kwamba, Wakristo wote wanatembea katika umoja, huku wakuongozwa na Mwanga angavu kutoka mbinguni, wanapokutana na giza nene katika ulimwengu mamboleo. Sinodi na majadiliano ya kiekumene ni sawa na chanda na pete, ni mambo yanayokamilishana. Nyota angavu iliwaongoza Mamajusi kutoka Mashariki hadi mjini Bethlehemu na huko wakamwona Mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia, wakamtolea tunu: dhahabu, uvumba na manemane. Rej. Mt. 2: 1-12. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa hata kwa Wakristo katika kipindi hiki cha miaka miwili ya maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Wawe na uthubutu wa kufungua hazina na tunu ambazo Jumuiya mbalimbali za Kikristo zimejaliwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ujenzi wa Wakristo. Kumbe, Wakristo wanaweza pia kunogesha maadhimisho ya Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa sala ifuatayo:

Ee Mungu Baba Mwenyezi wa mbinguni, kama ilivyokuwa kwa Mamajusi kusafiri kwenda Bethlehemu huku wakiongozwa na nyota, kwa njia hii, mwanga wetu wa mbinguni, uliongoze Kanisa Katoliki ili liweze kutembea pamoja na Wakristo wote katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu. Kama ilivyokuwa kwa Mamajusi waliounganishwa ili kusali kwa Kristo Yesu, utuongoze ili tuweze kuwa karibu zaidi na Mwanao wa pekee, Kristo Yesu; ufungue tunu zetu kama zawadi tunazoweza kubadilishana, ili tuweze kuwa ni alama ya umoja ambao Mwenyezi Mungu anaunuia kwa ajili ya Kanisa lake na kwa viumbe vyote. Tunaomba haya kwa njia ya Kristo Yesu, Bwana wetu. Amina.

Maaskofu na Uekumene
18 January 2022, 15:12