Tafuta

Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 183. Kuna Mabalozi wakazi 87 wanaoishi mjini Roma. Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 183. Kuna Mabalozi wakazi 87 wanaoishi mjini Roma.  

Vatican Ina Uhusiano wa Kimataifa Na Nchi 183: Utu , Haki na Amani

Kuna nchi 183 zenye uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican. Pia kuna Umoja wa Ulaya, Shirika la Kimataifa la Malta, Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina. Balozi na Mashirika ya Kimataifa yenye makao yake mjini Roma kwa sasa ni 87 baada ya nchi za Belize, Burkina Faso, Guinea Equatorial pamoja na Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina kuanzisha makao yake mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe 10 Januari 2022, kuna nchi 183 zenye uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican. Licha ya nchi hizi, pia kuna Umoja wa Ulaya, Shirika la Kimataifa la Malta pamoja na Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina. Balozi na Mashirika ya Kimataifa yenye makao yake mjini Roma kwa sasa ni 87 baada ya nchi za Belize, Burkina Faso, Guinea Equatorial pamoja na Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina kuanzisha makao yake mjini Roma. Kuna pia Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR. Tarehe 12 Oktoba 2020 Vatican na Austria zilitiliana saini Nyongeza katika Mkataba wa VII wa Makubaliano kuhusu uratibu wa mali ya Kanisa uliotiwa mkwaju na nchi hizi mbili tarehe 23 Juni 1960 huko mjini Vienna, Austria. Tarehe 26 Novemba 2021 Vatican na Austria zilibadilisha hati za kutendea kazi kwa kutambua kisheria elimu inayotolewa na taasisi za Kanisa kama ilivyobainishwa kwenye Mkataba kati ya Vatican na UNESCO wa terehe 25 Novemba 2019. Tarehe 31 Mei, Shirika la Afya Duniani, WHO liliridhia Vatican kushiriki katika mikutano yake kama Mwanachama msikilizaji.

Vatican pia imekwisha kuridhia Mkataba kati yake na DRC uliotiwa mkwaju tarehe 20 Mei 2016 pamoja na Mkataba na Burkina Faso ulioridhiwa na nchi hizi mbili tarehe 12 Julai 2019. Tarehe 5 Mei 2008 Vatican iliridhia Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 “Montreal Protocol of 1987”. Huu ni Mkataba wa Kimataifa ulioridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zenye kemikali zinazomong’onyoa tabaka la hewa ya ozoni angani, ambayo ni muhimu sana katika kudhibiti kiwango cha mionzi ya jua inayotua ardhini. Ozoni ni hewa iliyoko kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 10 hadi 50 juu ya ardhi. Kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mnururisho wa mionzi kama “Ultraviolet B” isifike kwenye uso wa dunia. Itifaki hii pamoja na mambo mengine inapania kuhamasisha ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kuratibu shughuli mbali mbali za binadamu zinazotishia kuharibu tabaka la hewa ya ozoni angani na hivyo kuchochea kuongezeka kwa joto duniani. Itifaki imepata mafanikio makubwa katika Jumuiya ya Kimataifa kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa ambayo ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kuna uhusiano wa karibu kati ya ongezeko la joto duniani na kumong’onyoka kwa tabaka la hewa ya ozoni angani. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu. Elimu makini haina budi kutolewa kwenye vituo vya elimu na utamaduni, mahali wanapoandaliwa wanasiasa, wanasayansi na raia, ili hatimaye, waweze kuwajibika barabara katika maamuzi yao. Ustawi, mafao ya wengi sanjari na maendeleo fungamani yasaidie kuleta maboresho makubwa katika maisha ya watu. Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China, ulitiwa saini tarehe 22 Septemba 2018 kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia. Tarehe 22 Oktoba 2020, Mkataba huu uliongezwa kwa muda wa miaka miwili. Lengo la Vatican ni kuwapata wachungaji bora watakaotekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu katika huduma kwa watu wa Mungu, katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina ulioanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ukaendelezwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko akashuhudia matunda ya juhudi hizi katika ukweli na uwazi. Mkazo ni kuhusu shughuli za kichungaji na kitume, ili kuwawezesha waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchakato huu pamoja na mambo mengine unapania kukoleza: imani na matumaini; umoja na mshikamano wa kidugu.

Uteuzi wa Maaskofu kwa ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya China ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini China na kwamba, huo ni mwanzo wa ushirikiano mpana zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni. Serikali ya China inatambua kunathamini dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kama Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki. Huo ni mwanzo wa amani na utulivu miongoni mwa watu wa Mungu nchini China. Kumbe, Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China hauna uhusiano na masuala ya kisiasa bali unajikita zaidi katika maisha na utume wa Kanisa nchini China, kama kielelezo cha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tarehe 26 Juni 2018, Vatican na nchi ya San Marino waliridhia kwa pamoja mkataba wa ushirikiano na Kanisa ili kutoa fursa ya kufundisha dini shuleni. Tarehe 23 Agosti 2018 Vatican na Benin ziliridhia mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa na kwamba, kwa sasa Serikali ya Benin inalitambua Kanisa Katoliki kisheria! Tarehe 22 Septemba, 2018 Vatican na China zilitiliana saini mkataba wa muda unaotoa fursa na uwezo kwa Kanisa kuteuwa Maaskofu mahalia. Kwa mara ya kwanza, Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha Maaskofu wote nchini China kuwa na umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika mchakato wa uinjilishaji wa familia ya Mungu nchini China.

Tarehe 16 Julai 2018, Vatican iliridhia Mkataba na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO kuhusu umuhimu wa utamaduni kama chombo cha kujenga na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu. Ushirikiano huu unapania kujenga na kudumisha haki msingi za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria Barani Ulaya. Itakumbukwa kwamba, tarehe 21 Machi 2018 Vatican iliridhia mkataba wa kufundisha elimu ya juu Barani Asia na kwenye Visiwa vya Pacific. Na hatimaye, tarehe 30 Novemba 2018 Vatican pia ilijiunga na malipo ya huduma kwa kutumia Euro, maarufu kama (SEPA). Hapo tarehe 4 Juni 2015 Vatican imekuwa pia ni mwanachama mtazamaji wa Jumuiya ya Caraibi, CARICOM.

Uhusiano wa Kimataifa
12 January 2022, 14:47