Tafuta

Kwa wafuasi wa Kristo Yesu, Jana, Leo na Daima, uongozi ni huduma na nguvu pekee wanayoweza kujivunia ni Fumbo la Msalaba watangaze na kushuhudia nguvu ya Msalaba. Kwa wafuasi wa Kristo Yesu, Jana, Leo na Daima, uongozi ni huduma na nguvu pekee wanayoweza kujivunia ni Fumbo la Msalaba watangaze na kushuhudia nguvu ya Msalaba. 

Wamisionari wa Damu Azizi: C.PP.S., Shuhudieni Nguvu ya Msalaba Katika Huduma

Watambue kwamba, wanashiriki na kuenzi karama na zawadi ya Roho Mtakatifu aliyopewa Mtakatifu Gaspare del Bufalo. Wao wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujumbe wa Msalaba unaokita maudhui yake katika Damu Azizi iliyomwagika pale Msalabani kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu Bikira Maria alipokubali na kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake kama Mjakazi wa Bwana, alijiweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kutekeleza mpango wake wa upendo kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Alionesha upendo mkuu kwa Mungu na jirani, kwa kujisadaka kwenda kumsaidia binamu yake Elizabeth aliyekuwa ni mjamzito. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Neno wa Mungu akatwaa mwili na kuzaliwa kwake Bikira Maria, ambaye alikuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu. Bikira Maria aliendelea kuwa mwanafunzi mwaminifu kwa Kristo Yesu, kiasi hata cha kushuhudia akiteswa na kufa Msalabani. Hii ni baada ya matukio makuu yaliyotendeka Siku ile iliyotangulia kufa kwake. Alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu: Mwili na Damu yake Azizi; alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu na huduma ya upendo kwa kuwaosha miguu wanafunzi wake, kielelezo cha unyenyekevu wa hali ya juu kabisa na mafano maridhawa wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo inayosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Pamoja na mambo yote hayo makuu yaliyotendeka katika maisha na utume wa Kristo Yesu, bado aliendelea kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu.

Hii ni sehemu ya wosia na tafakari iliyotolewa na Askofu mkuu Lazzaro You Heung Sik Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri wakati alipokuwa anatoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Pham Hao Anh, C.PP.S., na Vu Hoa Thai Vincent, C.PP.S., pamoja na Daraja ya Ushemasi kwa Phung Van Ky Joseph, C.PP.S. Wote watatu ni Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., kutoka nchini Vietnam. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Parokia ya “Santa Maria delle Grazie alle Fornaci”, Jimbo kuu la Roma. Askofu mkuu Lazzaro You Heung Sik amewakumbusha Mapadre wapya na Shemasi kwamba, tangu walipopokelewa rasmi na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu na kuweka ahadi za: Utii, Ufukara na Useja, waliwekwa wakfu kwa ajili ya kuwatumikia watu watakatifu wa Mungu katika shughuli mbalimbali za kichungaji kadiri watakavyopangiwa na wakuu wao wa Shirika. Kwa nguvu na neema ya Sakramenti ya Daraja, Mwenyezi Mungu anawawezesha kuwa ni wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Hii ni neema inayowawezesha kutekeleza dhamana na utume wao wa kimisionari mintarafu karama ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, yaani kutangaza na kushuhudia huruma, upendo na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika Damu yake Azizi, kwa ajili ya kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, mahali popote pale watakapotumwa na Shirika. Mapadre na Shemasi mpya wamekumbushwa madaraka katika Kanisa ni kwa ajili ya huduma kama anavyokazia Kristo Yesu mwenyewe akisema: “Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mk 10: 43. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwamba, kwa wafuasi wa Kristo Yesu, Jana, Leo na Daima, uongozi ni huduma na nguvu pekee wanayoweza kujivunia ni Fumbo la Msalaba. Watambue kwamba, wanashiriki na kuenzi karama na zawadi ya Roho Mtakatifu aliyopewa Mtakatifu Gaspare del Bufalo, Muasisi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu.

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujumbe wa Msalaba unaokita maudhui yake katika Damu Azizi ya Kristo Yesu iliyomwagika pale Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Kuna zaidi ya watu wa Mungu 130, 000 wametoa sadaka maisha na kumwaga damu yao kama Mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu huko nchini Vietnam na kati yao 117 tu ndio wanaotambuliwa rasmi na Mama Kanisa kuwa ni Wafiadini. Hawa ni nguzo ambayo imeendelea kulisimika Kanisa nchini Vietnam na kwa hakika, wao ni chemchemi ya maisha ya Kikristo na wito wao wa Kipadre na Kimisionari. Huu ni muda wa kukesha na kuwa tayari, kumpokea Kristo Yesu anapokuja kuwatembelea. Askofu mkuu Lazzaro You Heung Sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, mwishoni mwa mahubiri yake, amependa kuwahakikishia sala zake bila kusahau kwamba, kuna umati wa wamisionari, ndugu, jamaa na marafiki wanaowaombea katika maisha na utume wao wa Kikuhani.

Ibada hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu wakiongozwa na Mheshimiwa Padre Emmanuele Lupi, C.PP.S., Mkuu wa Shirika Ulimwenguni bila kumsahau Padre Francis Bartolon, C.PP.S. ambaye kwa miaka mingi ametekeleza utume wake wa Kimisionari nchini Tanzania na anakumbukwa zaidi kwenye malezi ya wamisionari wa Damu Azizi Kanda ya Tanzania. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu anawapongeza Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kwa kuchukua dhamana ya kuanzisha utume nchini Vietnam, kwa sababu hiki ni kipindi cha neema kitakazozaa matunda kwa wakati wake.

Wakati huo huo, Jumamosi tarehe 11 Januari 2022 Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida, Tanzania ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi John Francis Kisori na Abel William Missanga wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania kwenye Parokia ya Leo Mkuu, Makiungu, Jimbo Katoliki la Singida, inayoendeshwa na Shirika la Mtakatifu Vincent wa Palloti, aliyekuwa rafiki wa karibu sana wa Mtakatifu Gaspare del Bufalo. Mt. Vincent wa Pallotti ni kielelezo cha Kasisi makini aliyejitoa kwa ajili ya Kanisa kati ya mwaka 1795 hadi mwaka 1850; Nabii wa umoja wa Kanisa, aliyetangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 20 Januari 1963, wakati wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hadi tarehe 22 Januari 2022, Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania lina Mapadre 84 kadiri ya taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Padre Vedasto Ngowi, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania.

CPPS Madaraja
22 January 2022, 14:37