Tafuta

Jarida la 'Terra Santa' Mwaka 2022 linaadhimisha Kumbukizi la Jubilei ya Miaka 100 tangtu lilipozinduliwa kunako mwaka 1921. Jarida la 'Terra Santa' Mwaka 2022 linaadhimisha Kumbukizi la Jubilei ya Miaka 100 tangtu lilipozinduliwa kunako mwaka 1921.  (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 100 ya Jarida la "Terra Santa": Nchi Takatifu: Ushuhuda

Ni matumaini ya viongozi wakuu wa kidini kwamba, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, utakuwa huru kwa waamini wa dini hizi tatu kuwa na uhakika wa kuendesha Ibada zao, ili Sala na sadaka zinazotolewa mahali hapa ziweze kumfikia Mwenyezi Mungu, Muumbaji, kwa ajili ya amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu duniani; ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mji wa Yerusalemu kimsingi ni kwa ajili ya mafao ya Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni Mji Mtakatifu unaoheshimiwa na waamini wa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam. Kumbe, kwa waamini wa dini hizi, huu ni Mji mkuu wa maisha ya kiroho na kitovu cha majadiliano ya kidini, kiekumene, upatanisho na amani huko Mashariki ya Kati! Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, kuna haja pia ya kuzingatia maoni ya viongozi wa kidini badala ya kujikita katika maamuzi ya kisiasa peke yake! Utakatifu, Asili na Tunu msingi za Mji wa Yerusalemu vinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Morocco, tarehe 30 Machi 2019 pamoja na Mfalme Mohammed VI wa Morocco walitia saini kwenye tamko la pamoja linalojulikana kama “Tamko la Mji Mtakatifu wa Yerusalemu na Mahali Pa Kuwakutanisha watu.” Viongozi hawa wanatambua utakatifu, ukuu na umuhimu wa Mji wa Yerusalemu katika maisha ya kiroho ya waamini wa dini hizi tatu zinazomwabudu Mungu mmoja. Huu ni mji wa wa amani, amana na urithi wa binadamu wote, hususan waamini wa dini hizi tatu. Ni mahali pa watu kukutana na kwamba, Yerusalemu ni mji wa amani, mahali ambapo watu wanapaswa kuishi kwa utulivu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene.

Ni katika muktadha huu wa maisha ya kiroho na utambulisho wa kitamaduni, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu unapaswa kulindwa na kuendelezwa. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, utakuwa huru kwa waamini wa dini hizi tatu kuwa na uhakika wa kuendesha Ibada zao, ili Sala na sadaka zinazotolewa mahali hapa ziweze kumfikia Mwenyezi Mungu, Muumbaji, kwa ajili ya amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu duniani. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jarida la “Terra Santa” linaloratibiwa na Mfuko wa Nchi Takatifu “Fondazione Terra Santa”, yaani kunako mwaka 1921, Jumatatu, tarehe 17 Januari 2022 viongozi na wafanyakazi wa Jarida hili wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Huu ni ujumbe wa Kimataifa katika maadhimisho haya kutoka Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, ambao kwa takribani karne nane, unasimamiwa na Wafransikani wa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Hawa ndio walinzi wakuu wa Madhahabu ya maeneo matakatifu huko Nchi Takatifu, wanaowasindikiza mahujaji katika maeneo mbalimbali ya maisha na utume wa Kristo Yesu, lakini zaidi, wanajikita katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu na Mambo ya Kale.

Jarida la “Terrasanta” linachapishwa kila baada ya miezi miwili, kwa kuboreshwa na habari kutoka: Israeli, Palestina, Yordan, Lebanon, Siria, Misri na Visiwa vya Ugiriki ambako Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko linatekeleza dhamana na wajibu wake wa kichungaji. Jarida hili ni nyenzo msingi katika mchakato wa kufahamu mengi zaidi kuhusu Nchi Takatifu mintarafu maisha ya kidini kati ya waamini wa dini ya Kiislam, Kiyahudi na Wakristo. Ni Jarida linalozama zaidi katika masuala ya kitamaduni, Sayansi ya Biblia, Mambo Kale bila kusahau majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli Yerusalemu uweze kuwa ni kitovu cha amani na utulivu. Jarida hili linachapishwa na kusambazwa na Kituo cha Uchapishaji cha Wafranciskani, “Franciscan Printing Press na kwa wakati huu linachapishwa pia katika mfumo wa “TS Edition” ni maarufu sana katika uchapaji wa vitabu na majarida mbalimbali. Kazi yote hii inanogeshwa na Idara ya Uchapaji ya “Christian Media Center.”

Fondazione T. Santa
18 January 2022, 08:27