Wanatumia teknolojia mpya kama vile akili bandia na utambuzi wa uso katika mapigano na shambulio la kwanza la ndege isiyo na rubani tayari lilitokea nchini Libya Wanatumia teknolojia mpya kama vile akili bandia na utambuzi wa uso katika mapigano na shambulio la kwanza la ndege isiyo na rubani tayari lilitokea nchini Libya 

Mkutano wa UN umefungwa bila makubaliano kuhusu akili bandia katika matumizi ya silaha

Katika mkutano uliofanyika kuanzia tarehe 13-17 Desemba 2021 haukufikia makubaliano kwa ajili ya sheria ambayo inahusisha udhibiti wa kibinadamu na sio wa akili bandia katika matumizi ya silaha za maangamizi.

Na Sr. Angella Rwezaula – Vatican.

Mkutano wa Sita wa Mapitio ya Mkataba wa kupiga Marufuku au Vizuizi vya Matumizi ya baadhi ya Silaha, ulimalizika bila makubaliano. Mkutano huo ulikuwa na malengo na miongoni mwake, lile la kutambua haja ya kupata sheria na kanuni za maadili ili kuhakikisha udhibiti wa binadamu juu ya matumizi ya silaha hatari zinazojiendesha. Pia ilikuwa na nia ya kuanza mazungumzo juu ya chombo kinachofunga kisheria. Mkutano huo badala yake ulimalizika kwa maelekezo ya kuzingatia mapendekezo kwa kufafanua hatua zinazowezekana kuzingatia itifaki zilizopo na  kuahirisha kila kitu kwa majadiliano mapya mnamo 2022.

Tofauti na silaha za nusu-kujitosheleza, zile zinazojiendesha kikamilifu zinasimamiwa na aina fulani ya  programu. Wanatumia teknolojia mpya kama vile akili bandia na utambuzi wa uso. Hali, hii kwa sasa inaoonekana katika baadhi ya filamu lakini ambayo tayari imetengenezwa kwa kiasi na teknolojia, ni ya mizinga, nyambizi, roboti na ndege zisizo na rubani zinazolenga shabaha bila uangalizi wowote wa kibinadamu. Katika ripoti ya Umoja wa Mataifa, (UN) iliyochapishwa mwezi Machi uliopita inasisitizwa kuwa shambulio la kwanza la ndege isiyo na rubani tayari lilitokea nchini Libya. Baadhi ya nchi, ikiwa ni pamoja na Marekani na Urusi, zimetoa kiasi kikubwa cha fedha katika utengenezaji wa silaha hizo. Kwa ujumla, takwimu za matumizi ya kijeshi duniani ni kubwa: kumekuwa na kuongezeka maradufu, kuanzia mwaka 2000 hadi leo hii, duniani kote, kufikia karibu dola trilioni mbili kwa mwaka, mbele ya vita vingi, vimesahaulika na vinavyoikumba dunia.

Mazungumzo ya kimataifa ndiyo njia ya kuendeleza na siyo silaha. Alikuw amesema Papa Francisko mnamo tarehe 12 Desemba 2021, mara baada ya Sala ya malika wa Bwana akikumbusha hata takwimu za kushangaza. “Mimi nimeshikwa huzuni sana kuona takwimu zilizosoma za mwisho: mwaka huu wametengeneza silaha zaidi ya mwaka janga. Silaha sio njia, ni kufanya mazungumzo”, alisema. Na katika Waraka wake wa Fratelli Tutti, Baba Mtakatifu anaandika kuwa “vita ni ishara ya kushindwa kwa sera za kisisasa na ubinadamu ambao umeleta aibu na kushindwa mbele ya nguvu za ubaya”.

Mifumo ya kisilaha kwa namna ya pekee ili inayaojitegemea, inaibua maswali ya kimaalidi na kijamii. Kwa mujibu wa Vatican ni muhimu kuhakikisha usimamizi wa kutosha, wenye maana na thabiti wa kibinadamu kwa kuwa ni wanadamu pekee wanaoweza kuona matokeo ya matendo yao na kuelewa uhusiano kati ya sababu na athari. Kama sehemu ya mkutano uliofanyika  huko Geneva, Baraza Kuu pia lilisisitiza haja ya kufanya kila juhudi ili kuelekea upokonyaji wa silaha kwa ujumla na kamili chini ya udhibiti mkali na mzuri wa kimataifa.  Katika hotuba yake kwenye Mkutano ho lililofanyika Uswizi, Monsinyo John D. Putzer, Balozi wa muda katika Uwakilishi  wa Kudumu wa Vatican  katika ofisi za  Umoja wa Mataifa huko Geneva, pia alionesha kipaumbele cha kuendeleza uadilifu na maendeleo endelevu ya sheria za kimataifa zinazotumika katika migogoro ya silaha

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo alisema ni lazima kubadilisha dira kuelekea matumizi ya akili bandia shirikishi kati ya Mataifa na kwa malengo ya amani badala ya kijeshi. Vatican inahimiza Mataifa kuzingatia uundaji wa mashirika ya kimataifa kwa ajili ya akili banda, ili kuharakisha na kuhakikisha haki za mataifa yote ushiriki wa kubadilishana habari iwezekanavyo za kisayansi na kiteknolojia kwa ajili ya matumizi ya amani na kwa ajili ya wema wa familia nzima ya kibinadamu. Kipindi hiki cha msukosuko wa janga kwa mjibu wa Monsinyo Putzer, ni muhimu kuweka teknolojia zilizopo katika huduma ya binadamu  na matumizi ya amani na kwa ajili ya amaendeleo fungamani ya binadamu.

Mkutano wa Sita wa Mapitio ya Mkataba wa Kupiga Marufuku au Uzuiaji wa Matumizi ya Silaha kwa  maana hiyo haukuleta maelewano, bali ulikuwa na fursa ya kufanya mjadala na makabiliano. Mataifa yalikubali kuendelea na kazi kwenye teknolojia zinazoibuka katika eneo la mifumo ya silaha hatari kwa mwaka mwingine. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Antonio Guterres, amezitaka nchi hizo kuwasilisha mpango kabambe kuhusu sheria mpya. Austria na New Zealand zimependekeza, hasa, kuundwa kwa sheria mpya ya kimataifa inayodhibiti silaha zinazojiendesha. Nchi nyingi zilielezea kusikitishwa kwao na kushindwa kufikia makubaliano katika Mkutano wa Geneva. “Kwa sasa, kasi ya maendeleo ya teknolojia inahatarisha kupita maazimio yetu”, alisema Balozi wa Uswizi Felix Baumann alisema.

Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi katika suala hili yamesikitika sana. Waliwataka wajadili kuanza kufanyia kazi mkataba wa kimataifa wa kuanzisha sheria mpya zinazowabana kisheria. “Hii ni fursa iliyokosa,"alisema mshauri wa kisayansi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, Neil Davison. Aidha Muungano wa “Stop Killer Robots” ulielezea kusikitishwa kwake, kwamba  mataifa machache, hasa Marekani  na Urusi, yamezuia nchi nyingi kuchukua fursa ya kihistoria, lakini pia ikasisitiza kwamba itaendelea kufanya kazi ili kuhakikisha ulimwengu unakuwepo,  mahali ambapo teknolojia inaendelezwa na kutumika kukuza amani.

20 December 2021, 14:21