Askofu Mkuu Dieudonnè Datonou Balozi wa Vatican nchini Burundi awekwa wakfu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 20 Novemba 2021. Askofu Mkuu Dieudonnè Datonou Balozi wa Vatican nchini Burundi awekwa wakfu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 20 Novemba 2021. 

Askofu Mkuu Dieudonné Datonou, Balozi wa Vatican Nchini Burundi

Askofu mkuu Dieudonné Datonou alizaliwa 3 Machi 1962 huko Dèkanmè, Benin. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 7 Desemba 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Cotonou. Tarehe 7 Oktoba 2021 akateuliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Burundi sanjari na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameufunga Mwaka wa Kanisa sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu kwa kumweka wakfu Monsinyo Dieudonné Datonou, kuwa Askofu mkuu baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Burundi. Amefafanua umuhimu wa Sherehe hii katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia Injili ya huduma kwa watu wa Mungu na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma inayosimikwa katika: Kweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki, Amani na Mapendo. Kanisa ambalo linapata chimbuko lake pale juu Msalabani ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote. Askofu mkuu Dieudonné Datonou atambue kwamba, ameteuliwa na kutumwa na Baba Mtakatifu Francisko kama Balozi wa Vatican nchini Burundi ili kujenga na kuimarisha ushirika kati ya Kanisa mahalia na Khalifa wa Matakatifu Petro. Kumbe, anapaswa kuwa ni mtu wa amani, mjenzi na shuhuda wa amani. Awe ni daraja la majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwenye Makanisa mahalia. Upendo, ukweli na huruma ni utambulisho makini kwa Balozi wa Vatican popote pale alipo.

Anasema, Balozi wa Vatican ni mtu anayeongozwa kwa Neno la Mungu, ili kuweza kufikiri, kuamua na kutenda; daima akijikabidhi na kujiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mungu. Ni mtu asiyekubali kiurahisi kumezwa na malimwengu.Sifa za mtu wa Mungu ni pamoja na: haki, upendo, huruma, ibada na msamaha! Pale wanaposhindwa kujitambua kwamba, ni watu wa Mungu wanakuwa ni chanzo cha kuanguka kwao wenyewe pamoja na kusababisha madhara kwa watu wengine. Balozi wa Vatican ni mtu wa Kanisa kwani anamwakilisha Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa. Anapaswa kuwaheshimu, kuwalinda na kuwaendeleza wale wote anaokutana nao katika maisha na utume wake, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni kwa ajili ya huduma inayofumbatwa katika unyenyekevu. Ni watu wanaopaswa kushuhudia fadhila za kibaba na kichungaji.

Askofu mkuu Dieudonné Datonou ni kiongozi mwenye uzoefu na mang’amuzi mazito, msaada mkubwa katika maisha na utume wake nchini Burundi. Huu ni mwaliko kwake kuendelea kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu katika: Sala, Sakramenti, Neno la Mungu na huduma makini. Lengo ni kuimarisha mapendo, uaminifu na unyenyekevu katika huduma. Waamini wa Kanisa Katoliki Burundi wanahudumiwa katika majimbo manane nayo ni: Jimbo la Bubanza, Jimbo kuu la Bujumbura; Jimbo la Bururi; Jimbo kuu la Gitega; Jimbo la Muyinga; Jimbo la Ngozi; Jimbo la Rutana pamoja na Jimbo la Ruyigi. Ni wajibu wa Askofu mkuu Dieudonné Datonou kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu nchini Burundi wanaonja uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu katika maisha na utume wao. Burundi bado ina makovu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe. Inakabiliwa na hali tete ya kisiasa, madhara ambayo yanasikika kwa wananchi wa kawaida. Bado kuna umaskini, baa la njaa, na maradhi. Akiwa nchini Burundi anapaswa kuwa ni sauti ya maskini na wanyonge, ili kudumisha: huduma ya amani; kwa kuwalinda na kuwatetea wanyonge na kuendeleza mchakato wa majadiliano na watu wote wa Mungu nchini Burundi! Yote haya yanapaswa kutekelezwa kwa kujikita katika misingi ya hekima na busara; ujasiri, ustawi na mafao ya wengi.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alimteuwa Monsinyo Dieudonné Datonou kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Burundi na kumpandisha hadhi ya kuwa ni Askofu mkuu. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Dieudonné Datonou alikuwa ni mratibu wa hija za kichungaji za Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Huu ni uteuzi uliotangazwa moja kwa moja na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Hungaria tarehe 12 Septemba 2021. Askofu mkuu Dieudonné Datonou ndiye aliye ratibu pia hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia iliyonogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu.” Aliratibu pia hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq. Baba Mtakatifu Francisko alisema, hija yake ya kitume ya 33 kimataifa nchini Iraq ni kati ya hija ambazo zilikuwa hatari sana katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Alitumia muda mrefu kusali na kutafakari. Akapima madhara na faida yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Iraq.

Askofu mkuu Dieudonné Datonou alianza safari ya huduma ya diplomasia ya Kanisa tarehe Mosi Julai 1995. Tayari alikwisha kufanya utume wake nchini Angola, Equador, Cameroon, Iran, India, El Salvador na baadaye kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Askofu mkuu Dieudonné Datonou alizaliwa tarehe 3 Machi 1962 huko Dèkanmè, nchini Benin. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 7 Desemba 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Cotonou, nchini Benin. Tarehe 7 Oktoba 2021 akateuliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Burundi sanjari na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu. Historia inaonesha kwamba, tukio kama hili liliwahi kufanywa na Mtakatifu Paulo VI tarehe 5 Januari 1964 alimpoteua Monsinyo Jaques Martin kuwa Askofu baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume iliyoacha historia ya pekee katika maisha na utume wake Nchi Takatifu. Huo ukawa ni mwanzo wa hija za kitume zilizoanza kutekelezwa na Mapapa baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Burundi
21 November 2021, 16:06