Mwelekeo mpya wa mahusiano ya Korea na Jumuiya ya Kimataifa: Kwa ajili ya amani, uchumi na maisha. Mchango wa Kanisa: Kanuni maadili, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwelekeo mpya wa mahusiano ya Korea na Jumuiya ya Kimataifa: Kwa ajili ya amani, uchumi na maisha. Mchango wa Kanisa: Kanuni maadili, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Kardinali Parolin: Korea: Amani, Upatanisho, Uchumi na Maisha!

Papa Francisko anakazia: Kuwakaribisha wengine, kuwasindikiza sanjari na kukuza kipaji cha kusikilizana katika ukweli na uwazi. Kanuni maadili inawataka wananchi wa Korea kutafuta yale mambo msingi yanayowaunganisha zaidi badala ya kushabikia yale mambo yanayowagawa na kuwasambaratisha kama Jamii kama kielelezo cha umoja, upendo na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Mwelekeo Mpya wa Mahusiano ya Korea na Jumuiya: Kwa Ajili ya Amani, Uchumi na Maisha. Mchango wa Kanisa Katoliki katika mchakato wa kuanzisha amani nchini Korea. Kanisa kwa upande wake, linaweza kuchangia kanuni maadili na tunu msingi zinazopewa kipaumbele katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa kuwakaribisha wengine, kuwasindikiza sanjari na kukuza kipaji cha kusikilizana katika ukweli na uwazi. Kanuni maadili inawataka wananchi wa Korea kutafuta yale mambo msingi yanayowaunganisha zaidi badala ya kushabikia yale mambo yanayowagawa na kuwasambaratisha kama Jamii kama kielelezo cha umoja, upendo na udugu wa kibinadamu. Diplomasia ya Vatican na Kanisa katika ujumla wake, kimsingi inakazia kwa namna ya pekee kabisa: huduma makini ya maendeleo fungamani ya binadamu; kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mambo mengine msingi ni amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani; elimu, afya, biashara, mawasiliano, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na haki miliki ya kiakili. Hizi ni kanuni msingi zinazofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa dira na mwongozo makini kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kukuza na kudumisha utamaduni wa amani, haki, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu.

Hii ni sehemu muhimu sana ya utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Vatican katika masuala ya kidiplomasia inafuata kwa makini sana sheria, taratibu na kanuni za Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii inayojikita katika kanuni maadili na ushirikiano unaosimamiwa na kuratibiwa na kanuni auni. Amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa kujengwa siku kwa siku. Amani ni matokeo ya haki inayomwilishwa katika upendo, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. GS 78. Amani ya kweli inakolezwa katika urafiki wa kidugu. Upatanisho ni mchakato unaopania kuboresha maisha ya mbeleni na unafumbatwa katika toba, msamaha na wongofu wa ndani, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo, chemchemi ya amani ya kudumu. Kwa ufupi huu ndio mchango uliotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenye hotuba yake elekezi katika ufunguzi wa Mkutano wa Korea uliofanyika kuanzia tarehe 31 Agosti 2021 hadi tarehe 2 Septemba 2021. Kardinali Parolin katika hotuba yake amekazia umuhimu wa familia ya Mungu nchini Korea kuwa na mwamko mpya kuhusu: amani, uchumi na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume Evangelii gaudium, yaani Furaha ya Injili, anakazia kuhusu mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika umoja, mshikamano na mafungamano katika misingi ya ukweli, uwazi na upendo, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Katika muktadha huu, hakuna maadui, bali wote wanakuwa ni wandani wa safari. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kukosa na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu. Kumbe, kuna haja ya kukaribishana na kuanza kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, ili kujenga mafungamano ya kweli, kwa kushirikiana na kusaidiana katika maisha. Wananchi wanahamasishwa kusindikizana kwa kuheshimu Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na kujikita katika haki msingi za binadamu. Utamaduni wa kusikilizana unajengeka katika misingi ya kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja; kupokea na kukubali mawazo ya jirani zako kama kielelezo cha udugu wa upendo wa kibinadamu. Huu ni mchakato wa kutafuta na kuambata yale mambo msingi yanayowaunganisha Wakorea kama nchi moja, kwa kuzama katika mazuri ya jirani!

Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kidiplomasia na uhusiano wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa anakazia kwa namna ya pekee: Mosi, umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu wa kibinadamu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vatican inakazia: ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita, mipasuko, kinzani na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia! Lengo la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi. Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani!

Kanisa linapenda kudumisha mchakato wa haki, amani, utulivu na maridhiano kwa kuzimisha moto wa machafuko, kinzani na vita kwa maji ya baraka, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia unaojikita katika kubainisha mbinu mkakati wa mawasiliano, vikwazo na vizingiziti vinavyoweza kujitokeza pamoja na kuunda mazingira ya kuaminiana na kuthaminiana, ili kuendeleza majadiliano. Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Amani ya kweli ni matunda ya upendo, urafiki na udugu wa kibinadamu. Kanuni ya dhahabu hapa ni kushinda uovu kwa kutenda mema! Baba Mtakatifu Francisko katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa mkwaju mwezi Februari 2019 anakazia udugu.

Huu ni udugu unaopaswa kumwilishwa katika matendo kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni udugu unaofumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Baba Mtakatifu anapenda pia kukazia msamaha na upatanisho wa kweli; kumbukumbu hai pamoja na haki. Kila mtu anao wajibu na haki ya kulinda utu na heshima yake, kwa sababu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anawataka watu wa Mungu Korea kuwa wahusika wakuu wanaotaka kuandika upya historia ya nchi yao katika misingi ya amani, uchumi fungamanishi na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Watu waheshimiane na kuthaminiana kama ndugu wamoja!

Paroloin Korea
06 September 2021, 14:00