Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi ameunda Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mbweni, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi ameunda Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mbweni, Jimbo kuu la Dar es Salaam. 

Uzinduzi wa Parokia ya Mt. Francisko wa Assisi, Mbweni, DSM!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi tarehe 7 Julai 2021 ameanzisha Parokia Mpya ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mbweni, ambayo hapo awali, kilikuwa ni Kigango cha Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Parokia Mpya ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ambayo imezinduliwa rasmi tarehe 1 Agosti 2021 iko chini ya uongozi wa Pd. Placid Siyoyi Beda na Padre John Kaniki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni wasanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee, katika Injili ya huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia”. Huu ndio mchakato wa mageuzi na upyaishaji wa Parokia unaoendelea katika maisha na utume wa Kanisa, sehemu mbali mbali za dunia. Mchakato huu, hauna budi kuratibiwa na Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati.

Katika muktadha huu, upyaisho unapaswa kuliangalia Kanisa zima si tu kama Kanisa mahalia! Upyaisho wa huduma Parokiani hauna budi kujikita katika miundombinu ya kimisionari iliyoko Parokiani. Huu ni mwaliko wa kujielekeza zaidi katika masuala ya maisha ya kiroho na wongofu wa kichungaji unaokita mizizi yake katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa. Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji na uwepo endelevu na fungamani wa Kristo Yesu kwa waja wake! Parokia ni mahali muafaka pa waamini kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa upendo na huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara.

Upyaisho wa kimisionari unalenga kuwahamasisha wabatizwa wote kutambua uzuri wa imani na furaha ya Injili, tayari kuwashirikisha watu wengine, mang’amuzi haya ya maisha ya kiroho baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Ni nafasi ya kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili hata wale waliokuwa wamesahau “mlango wa Kanisa” waweze kurejea tena kwa ari, nguvu na kasi mpya na hivyo kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anataka kutembea na kuambatana nao katika safari ya maisha yao ya kila siku! Huu ni mpango mkakati wa shughuli za kichungaji ambao ni shirikishi, kwa sababu waamini wote katika umoja na tofauti zao, wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni wakati muafaka kwa waamini kuwaendea jirani zao, huko “vijiweni” ili kuwatangazia na kuwashuhudia ile furaha ya Injili, kwa wale ambao bado wanatafuta fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Mapadre, watawa, mashemasi na waamini walei kwa pamoja, wanapaswa kujifunga kibwebwe kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Ni wakati wa kutumia rasilimali muda, vitu, fedha na uwepo kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa kuthamini familia kama shule ya kwanza ya uinjilishaji, huruma na upendo; hapa ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini. Kuna haja ya Parokia kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili kujenga Jumuiya kubwa zaidi ya watu wanaoinjilisha na kuinjilishwa. Katika mchakato huu, Paroko anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Wote wanaitwa na wanahamasishwa kushiriki katika safari hii ya imani, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani unaofumbatwa katika ari na mwamko wa kimisionari! Yote haya yamebanishwa kwa kina na mapana na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, ambapo tarehe 29 Juni 2020 lilichapisha Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa”. “Instruction: The pastoral conversion of the Parish community in the service of the evangelising mission of the Church.”

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam nchini Tanzania, tarehe 7 Julai 2021 ameanzisha Parokia Mpya ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mbweni, ambayo hapo awali, kilikuwa ni Kigango cha Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, inayohudumiwa na Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi Kanda ya Tanzania, C.PP.S. Parokia Mpya ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ambayo imezinduliwa rasmi tarehe 1 Agosti 2021 inahudumiwa na Shirika la Mateso “Passionist Fathers and Brothers” na iko chini ya uongozi wa Padre Placid Siyoyi Beda akishirikiana na Padre John Kaniki kama Paroko-usu ambao wamesimikwa na Padre Audax Mathias Kaasa, Dekano wa Dekania ya Mtakatifu Gaspare Jimbo kuu la Dar es Salaam. Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mbweni inaunganisha vitongoji vya Teta, Mpiji Magoe na Mbweni yenyewe. Na wakazi wengi wa eneo hili ni waamini wa dini ya Kiislam na wengi wao walikuwa ni wavuvi.

Tangu mwaka 1982 eneo hili lilikuwa linahudumiwa na Wamisionari wa Damu Azizi, C.PP.S. Kwa namna ya pekee kabisa, familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam inawakumbuka Padre Dominico Altieri, C.PP.S aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Mwili na Damu Azizi ya Yesu, Tegeta pamoja na Marehemu Padre Antonio Calabrese, C.PP.S. Kama sehemu ya majadiliano ya kidini, Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali, walianzisha mradi wa kituo cha Afya Mbweni, Maji safi na salama pamoja na uvuvi kwa ajili ya vijana wa Mbweni! Kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, Mheshimiwa Padre Francesco Bartoloni, C.PP.S. kama sehemu ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliamua kujenga Kanisa la Kigango cha Mbweni, ambalo Jumapili tarehe 1 Agosti 2021 limekuwa ni Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi. Juhudi za kuboresha huduma za kichungaji eneo la Mbweni zilinogeshwa kwa uwepo wa Kijiji cha Furaha, Mbweni kinachoendeshwa na Mapadre wa Mateso! Mchango wa waamini walei chini ya Mzee Simon M. Mapalala ambaye kwa miaka mingi amekuwa Katibu wa Kigango zimekiwezesha Kigango cha Mbweni kuwa ni Parokia kamili.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa ni kiini cha Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana; Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani tendaji! Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Inasikitisha kuona kwamba, kuna waamini wengi ambao hawashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa parokiani. Kumbe, kuna haja ya kuweka mbinu mkakati ya kuwaendea na kuwatafuta waamini hao, mahali wanapoishi na kufanya kazi, ili kuwapatia tena nafasi ya kukutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao.

Waamini wawe tayari kuwashirikisha wengine uzoefu na mang’amuzi yao katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya. Kila wakati waamini wanapokutana na watu watambue kwamba, hapo wanatekeleza dhamana na wajibu unaoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya jirani zao. Watu wanavutwa kwa ushuhuda wa maisha na wala si wongofu wa shuruti. Waamini wawe na ujasiri wa kuwaonjesha jirani zao Injili ya upendo, huruma na matumaini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa kutekeleza yote haya watambue kwamba, wanamtendea Kristo Yesu ambaye amejitambulisha na maskini pamoja na wahitaji mbalimbali. Vyama vya Kitume Parokiani vinatekeleza dhamana na wajibu wao kwa njia ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; Huduma kwa maskini na wanyonge zaidi, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na shuhuda za maisha yao zinazobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili.

Padre Emmanuel Makusaro, C.PP.S., Mmisionari wa Shirika la Damu Azizi na Paroko wa Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko, Jimbo kuu la Dar es Salaam amemwosia Padre Placid Siyoyi Beda wa Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi asijitafutie magonjwa ya bure kabisa kwa kuhangaikia fedha za ujenzi wa Parokia mpya, jambo la msingi ni kujenga roho za watu na waamini watajisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Parokia yao: kiroho na kimwili! Na kwa wosia huu, Paroko hata akiwa mwembamba kiasi gani, atapata kitambi tu kwa sababu waamini watakuwa wanatumia karama na mapaji yao kwa ajili ya ujenzi wa Parokia!

Parokia ya Mbweni
01 August 2021, 15:34