Kifo cha Padre Raymond Saba: Waamini Jiandaeni Kupokea Fumbo la Msalaba katika maisha yenu! Kifo cha Padre Raymond Saba: Waamini Jiandaeni Kupokea Fumbo la Msalaba katika maisha yenu! 

Padre Raymond Saba: Jiandaeni Kupokea Fumbo la Msalaba!

Padre Raymond Saba ametekelezwa wajibu wake huu, kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu; kwa kutoa mafungo na semina. Kwake, Fumbo la Msalaba, lilikuwa ni jinsi ya kujishikamanisha na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka! Kwake Msalaba ulikuwa ni chemchemi ya: wokovu unaofumbatwa katika imani, matumaini na mapendo bila ya kujitafuta! Jiandaeni kufa kifo chema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumatatu tarehe 9 Agosti 2021 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumsindikiza Padre Raymond K. S. Saba katika makao ya uzima wa milele. Mahubiri yametolewa na Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora. Ibada ya mazishi imeongozwa na Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS, wa Jimbo Katoliki la Kigoma nchini Tanzania. Imehudhuriwa na Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo la Rulenge-Ngara, Askofu Desiderius M. Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba, wawakilishi wa Maaskofu pamoja na watu wa Mungu katika ujumla wao! Padre Raymond K. S. Saba wa Jimbo Katoliki la Kigoma, aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kati ya Mwezi Julai, 2013 hadi Juni 2018 amefariki dunia tarehe 3 Agosti 2021 akiwa anapatiwa matibabu huko “Rabininsia Memorial Hospital” iliyoko Jijini Dar es Salaam na kuzikwa kwenye Makaburi ya Kabanga, Jimbo Katoliki la Kigoma.

Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kuhusu imani katika ufufuko wa wafu na uzima wa milele kama ilivyoshuhudiwa na familia ya akina Mariamu, Martha na Lazaro na Kristo Yesu akakazia na kusema, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.” Yn 11: 25-27. Hata katika Agano la Kale watu walichanga fedha kwa ajili ya kuwaombea Marehemu wao, hali inayoonesha imani katika ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Askofu mkuu Ruzoka amesema kwamba, msiba una wenyewe na wenyewe ndio hao waamini waliomimina kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania ili kumsindikiza katika sala na sadaka ya Misa Takatifu Marehemu Padre Raymond Saba, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumrehemu, kumsamehe na kumtasa, ili hatimaye, aweze kushiriki katika maisha ya uzima wa milele na Kristo Yesu.

Mtakatifu Paulo Mtume, alipokuwa anawaaga wazee wa Efeso aliwakumbusha kwamba, aliwafundisha na kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Huko mbeleni anakabiliwa na vifungo na dhiki. Lakini hakuyahesabu maisha yake kuwa ni kitu cha thamani sana kwake, bali ameumaliza mwendo, ametangaza na kushuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu. Rej. Mdo 20:24. Padre Raymond Saba aliupenda na kuuthamini sana Upadre wake; akajitahidi kuishi kiaminifu, kwa kutweka hadi kilindini. Katika kipindi cha miaka 47 ya uhai wake, Padre Raymond Saba amewafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 18, si haba! Alitambua dhamana na wajibu wa Padre kama mhudumu wa Altare anayepasika kuwasaidia watu kukutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao, na hatimaye, kwenda mbinguni. Ni Padre aliyebahatika kutumia karama na mapaji yake kwa ajili ya kumtafuta, kumjua na kumpenda Mungu, ili aweze kumtakasa na kupyaisha maisha yake. Dhana ya kifo katika maisha ya mwanadamu inaogopesha ndiyo maana watu wanajitahidi kuboresha afya zao, lakini kifo ni lazima.

Jambo la msingi kwa waamini ni kujibidiisha kwenda mbinguni “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.” Ebr 9:27-28. Waamini wajitahidi kufa na kuishi katika Kristo Yesu. Mapadre katika maisha na utume wao, wawe ni vyombo na mabawa ya kuwanyanyua watu wa Mungu, kwa kushughulikia zaidi mambo ya kiroho, ili kuwatakatifuza na hatimaye, waweze kufikia heri za Kimungu. Padre Raymond ametekelezwa wajibu wake huu, kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu; kwa kutoa mafungo na semina. Kwake, Fumbo la Msalaba, lilikuwa ni jinsi ya kujishikamanisha na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kwake Msalaba ulikuwa ni chemchemi ya: wokovu unaofumbatwa katika imani, matumaini na mapendo bila ya kujitafuta! Kwa ufupi anasema Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora kwamba, kwa hakika Padre Raymond Saba anaweza kusema kama Mtakatifu Paulo Mtume: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.” 2Tim 4:7-8. Familia ya Mungu inamwombea Padre Raymond Saba ili Mwenyezi Mungu sasa aweze kumkirimia taji la haki na neema ya kukutana na Mwenyezi Mungu!

Wakati huo huo, Prof. Joyce Lazaro Ndalichako, Waziri wa elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi nchini Tanzania, amewasilisha salam za rambirambi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako amemwelezea Padre Raymond Saba kuwa ni kiongozi aliyejaliwa karama na mapaji ambayo ameyatumia kwa kuhubiri, mafungo na kutoa semina mbalimbali. Lakini jambo kubwa zaidi ni kwamba, alitumia nafasi yake kujielimisha zaidi kwa kusoma, ili kupambana na hali na mazingira, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Amewashauri watanzania kujenga utamaduni wa kujisomea, ili kupata uelewa zaidi, kuchambua mambo na ikiwezekana kuandika vitabu. Amelishauri Jimbo Katoliki la Kigoma na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika ujumla wake, kuangalia uwezekano wa kuanzisha Mfuko wa Padre Raymond Saba, kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya watanzania katika elimu!

Naye Askofu msaidizi mteule Henry Mchamungu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea na kumuaga Padre Raymond Saba kwenye Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC Kurasini amesema, Kifo, Ufufuko na Maisha ya uzima wa milele ni mambo makuu ambayo wafuasi wa Emau walikuwa wakijadiliana njiani baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu wao. Ni watu waliokuwa wamechanganyikiwa kutokana na Kashfa na upuuzi wa Msalaba, uliozika matumaini yao yote. Wanafunzi hawa walijenga matumaini yao kwa Kristo Yesu ambaye amekufa na kushindwa vibaya, kiasi kwamba amezikwa pamoja na matumaini yao yote! Wafuasi wa Emau baada ya kukutana, kuzungumza na kutembea na Yesu Kristo Mfufuka, wakarejea wakiwa wamesheheni furaha, imani na matumaini kedekede, tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka aliyewafufua kutoka katika makaburi yao ya kutoamini na kujikatia tamaa. Kwa kukutana na Kristo Mfufuka wakapata nafasi ya kufafanuliwa utimilifu wa Maandiko Matakatifu, Sheria na Unabii na hatimaye, kufahamu kwa kina maana ya Kashfa ya Msalaba.

Kwa mang’amuzi ya Fumbo la Msalaba wakaweza kufikia ukweli wa Ufufuko kiini cha matumaini mapya. Neno la Mungu na Sadaka ya Misa Takatifu iwe ni faraja na chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu walioguswa na msiba wa Padre Raymond Saba. Waendelee kuwa na imani na matumaini katika ufufuko, maisha na uzima wa milele. Padre Raymond Saba katika maisha na utume wake alikabiliana na changamoto za kiafya, akapata nafasi ya kuzama na kulitafakari Fumbo la Msalaba katika maisha yake. Tafakari hii, ikawa ni chemchem ya faraja, amani na utulivu wa ndani katika mapambano dhidi ya changamoto za kiafya. Katika kipindi hiki, akajikita zaidi katika kuandika na kutoa tafakari za maisha ya kiroho. Waamini katika safari ya maisha yao hapa duniani, wajenge utamaduni wa kujiandaa kupokea Fumbo la kifo chema katika maisha yao. Waamini waendelee kumkumbuka na kumwombea Padre Raymond Saba. Wajitahidi kuubeba msiba huu kwa imani, matumaini na mapendo thabiti.

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Padre Raymond K. S. Saba alizaliwa tarehe 19 Mei 1974, Parokiani Katubuka, Kigango cha Katubuka, Jimbo Katoliki la Kigoma. Alipata masomo na majiundo yake yake ya Kikasisi kutoka Nyumba ya Malezi ya Watakatifu Petro na Paulo, Iterambogo kwa mwaka wa malezi. Baadaye aliendelea na masomo ya Falsafa kutoka Seminari kuu ya Bikira Maria Malkia wa Malaika, Kibosho. Na masomo ya Taalimungu, alipelekwa Seminari kuu ya Mtakatifu Kalori Lwanga, Segerea na baadaye akapewa Daraja Takatifu ya Ushemasi hapo tarehe 25 Januari 2003, Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Ilikuwa ni tarehe 13 Julai 2003 alipopewa Daraja ya Upadre na Askofu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo Katoliki la Kigoma, kwenye Parokia ya Bikira Maria Mshindaji, Jimbo Katoliki la Kigoma.

Kama Padre aliteuliwa kuwa Katibu muhtasi wa Askofu kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2004 na baadaye akatumwa Jimbo Katoliki la Kahama kuwa Gambera Msaidizi wa Seminari Ndogo ya Malkia wa Mitume, Ushirombo, Jimbo Katoliki la Kahama. Katika kipindi cha kati ya mwezi Januari hadi Juni 2006 aliteuliwa kuwa ni Baba wa maisha ya kiroho, Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yosefu, Iterambogo, Jimbo Katoliki la Kigoma. Kati ya Mwezi Julai 2006 hadi Julai 2011 alitumwa na Jimbo kwenda Italia kujiendeleza zaidi kwa masomo kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesianum na huko akajipatia Shahada ya Uzamili katika Nyaraka za Kikristo “Christian Letters and Classics.”

Kati ya Mwezi Julai 2011 aliteuliwa na Askofu Protase Rugambwa wa Jimbo Katoliki Kigoma kuwa Gambera Msaidizi wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yosefu, Iterambogo. Wakati huo huo, akateuliwa pia kuwa Wakili Paroko Parokia ya Mtakatifu Clara, Kidahwe hadi mwezi Julai 2012. Baadaye kuanzia Mwezi Julai 2012 hadi Julai 2013 aliteuliwa kuwa Naibu Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC na Katibu mtendaji Idara ya Uchungaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kati ya Mwezi Julai 2013 hadi Juni 2018 aliteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Tarehe 16 Aprili 2019, Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS, wa Jimbo Katoliki la Kigoma akamteuwa kuwa Paroko wa Parokia teule ya Mtakatifu Petro, Murobona hadi tarehe 5 Mei 2021. Tarehe 3 Agosti 2021 akaaga dunia katika hali ya amani na utulivu huko “Rabininsia Memorial Hospital” iliyoko Jijini Dar es Salaam na kuzikwa kwenye Makaburi ya Kabanga, Jimbo Katoliki la Kigoma.

Pd Raymond Saba

 

10 August 2021, 15:15