Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya familia yawasaidie waamini kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa. Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya familia yawasaidie waamini kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa. 

Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: Ndoa Takatifu

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, SACBS, kuanzia tarehe 22 Agosti hadi tarehe 9 Oktoba 2021 linaadhimisha Siku Maalum za Kuragibisha Sakramenti ya Ndoa. Wanandoa kwa kumfuata Kristo Yesu, kwa kujikana wao wenyewe na kwa kuchukua kila mmoja Msalaba wake, watu wa Ndoa Takatifu wanaweza kupokea maana halisi ya ndoa na kuiishi kwa msaada Kristo Yesu! Yaani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” kuanzia tarehe 19 Machi 2021 hadi tarehe 26 Juni, 2022 yanaongozwa na kauli mbiu “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.” Malengo makuu ni: kujitahidi kunafsisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka ili kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama shule ya upendo, huruma, haki, amani na ukarimu. Itakumbukwa kwamba, Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, uhai na upendo kielelezo cha ukomavu wa imani. Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu. Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana.

Mkazo uwe ni kwa ajili ya malezi, katekesi na majiundo ya awali na endelevu kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani inayoweza kutolewa ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo! Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, SACBS, kuanzia tarehe 22 Agosti hadi tarehe 9 Oktoba 2021 linaadhimisha Siku Maalum za Kuragibisha Sakramenti ya Ndoa kati ya Bwana na Bibi. Wanandoa kwa kumfuata Kristo Yesu, kwa kujikana wao wenyewe na kwa kuchukua kila mmoja Msalaba wake, watu wa Ndoa Takatifu wanaweza kupokea maana halisi ya ndoa na kuiishi kwa msaada Kristo Yesu. Neema hii ya ndoa ya Kikristo ni tunda la Msalaba wa Kristo Yesu, chemchemi ya maisha yote ya Kikristo! Ndiyo maana Mtakatifu Paulo, Mtume anakazia sana upendo kati ya wanandoa, kielelezo makini cha upendo wa Kristo Yesu kwa Kanisa lake! Rej. KKK 1613-1617. Baba Mtakatifu Francisko anasema hakuna familia ambayo hudondoka kutoka mbinguni ikiwa imeundwa kikamilifu; familia zina haja ya kukua na kupevuka katika uwezo wa kupenda.

Huu ni wito endelevu na fungamani katika maisha ya wanandoa unaochota amana na utajiri wake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linahamasika kuwatafuta na kuwasaidia wale ambao wanaogelea katika shida na mahangaiko mbalimbali ya maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anawahimiza watu wa Mungu kufunga safari na kutembea huku wakiwa wameshikamana bila ya kukata wala kukatishwa tamaa kwa sababu ya mapungufu yao ya kibinadamu. Kamwe wasiache kutafuta utimilifu wa upendo na ushirika wanaooneshwa na kufunuliwa na Mwenyezi Mungu. Rej. AL 325. Uamuzi huu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini umechukuliwa baada ya tafiti kubaini kwamba kuna waamini wengi ambao wametopea katika uchumba sugu, kiasi kwamba hata ile hamu ya kutoka huko na kuanza kuchanja mbuga imeanza kufifia pole pole na kuigeuza changamoto hii kuwa kana kwamba, ni jambo la kawaida! Katika kipindi chote hiki, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii itatumika kuragibisha maadhimisho haya. Maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha: Ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika maisha ya ndoa, kuna matatizo, raha na karaha zake! Huko ni patashika nguo kuchanika, lakini yote haya ni mambo mpito, jambo la msingi ni kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kwani Ndoa ni Sakramenti ya Kanisa kwa ajili pamoja na Kanisa na kwamba, upendo wa dhati kabisa unawezekana hata katika ulimwengu mamboleo. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanadumu katika nia njema, upendo wa dhati na uaminifu endelevu katika taabu na raha; katika magonjwa na afya; wapendane na kuheshimiana siku zote za maisha yao! Huu ndio uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni ushuhuda wa Injili ya familia unaotangazwa katika ukimya. Jubilei ya Miaka 50 au 25 ya Ndoa si habari wala mali kitu kwa baadhi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, wao wanasubiri kashfa! Wametalakiana na kutengana, eti hii ndiyo “habari ya mujini” anasema Baba Mtakatifu Francisko. Inawezekana wanandoa kutengana ili kuepuka maafa na majanga makubwa katika familia!

Ikumbukwe kwamba, uvumilivu ni fadhila muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia. Katika kipindi hiki chote, mada mbalimbali zinaendelea kuchambuliwa kwa kina na mapana na wanandoa wenyewe. Lakini zaidi ni kuhusu: Ndoa Takatifu kadiri ya mpango wa Mungu. Sifa na jinsi ya kuchagua mchumba bora zaidi. Ndoa kama Sakramenti ya Kanisa. Umuhimu wa adhimisho la Kiliturujia la Ndoa Takatifu kwani kwa lenyewe lazima liwe halali, lenye hadhi na lenye kuzaa matunda. Ukubaliano wa ndoa ni muhimu sana ili wanandoa waweze kupata matunda ya Sakramenti ya Ndoa kadiri ya mpango wa Mama Kanisa. Wakleri, watawa na waamini katika ujumla wao, wamegawana majukumu ili kunogesha Siku Maalum za Kuragibisha Sakramenti ya Ndoa kati ya Bwana na Bibi. Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” usaidie kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano kati ya familia na Kanisa, kwa kuwashirikisha zaidi wanandoa katika maisha na utume wa Kanisa. Malezi na katekesi ya kina, itolewe kwa mihimili yote ya Uinjilishaji, ili kukabiliana barabara na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazoendelea kuibuliwa katika maisha ya ndoa na familia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, familia kama Kanisa dogo la nyumbani inaimarishwa zaidi, kwa kutambua dhamana na utume wake usiokuwa na mbadala!

Ni wakati wa kukuza na kuhamasisha wito wa kimisionari ndani ya familia, kwa kuwajengea wazazi na walezi uwezo wa kufundisha na kuwarithisha watoto wao: imani na tunu msingi za Kiinjili; kwa kuwaandaa kikamilifu tangu awali kushiriki na kujisadaka katika maisha ya ndoa na familia, bila kusahau wito wa Daraja Takatifu. Kumbukizi ya ndoa iwe ni fursa ya kupyaisha tena katekesi na maagano ya ndoa, ili kuweza kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linabainisha kwamba, hii pia ni sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Maadhimisho yalizinduliwa tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa rasmi kwa kudema hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi katika maisha.

Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Mtakatifu Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika katika ndoto. Lengo la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu Yosefu anasema Baba Mtakatifu, ni kuwasaidia waamini kumfahamu na kumpenda Mtakatifu Yosefu aliyekuwa na mang’amuzi ya kibinadamu kama walivyo waamini wengi duniani. Ni Mtakatifu ambaye hakushtushwa sana na mambo, hakuwa na karama maalum wala kati ya watu wa nyakati zake, hakuwa mtu mashuhuri. Na wala Maandiko Matakatifu hayaoneshi maneno yaliyotoka kinywani mwake hata kidogo, lakini machoni pa Mwenyezi Mungu, aliweza kutenda matendo makuuu katika maisha na utume wake.

Sakramenti ya Ndoa

 

26 August 2021, 15:34