Askofu mkuu Lazarus You Heung-Sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makleri, tarehe 21 Agosti 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa, Jubilei ya Miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mt. Andrea Kim Taegon Askofu mkuu Lazarus You Heung-Sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makleri, tarehe 21 Agosti 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa, Jubilei ya Miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mt. Andrea Kim Taegon 

Misa Ya Jubilei ya Miaka 200 Tangu Kuzaliwa kwa Mt. Andrea K. Taegon

Askofu mkuu Lazarus You Heung-sik katika mahubiri amegusia: Mchakato wa uinjilishaji nchini Korea, Ushuhuda wa imani uliooneshwa na Mtakatifu Andrea Taegon na wenzake 102, mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika chanjo dhidi ya UVIKO-19, Umoja na mshikamano wa watu wa Mungu Korea bila kusahau mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Askofu mkuu Lazarus You Heung-sik Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, Jumamosi, tarehe 21 Agosti 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kumbukizi la Miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Andrea Kim Taegon, yaani tarehe 21 Agosti 1821. Mtakatifu Andrea Kim Taegon, alikuwa ni Padre wa kwanza mzalendo kuwekwa wakfu nchini Korea. Aliuwawa kikatili tarehe 16 Septemba 1846 wakati wa madhulumu nchini Korea kati ya Mwaka 1839-1846. Papa Pio XI tarehe 5 Mei 1925 akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 6 Mei 1984. Mama Kanisa anamkumbuka Mtakatifu Andrea Kim Taegon na wenzake 102 kila mwaka ifikapo tarehe 16 Septemba. Ibada ya Misa Takatifu imeadhimishwa katika lugha ya Kikorea kuonesha amana na utajiri wa Kanisa la Kristo Yesu unaofumbatwa katika mila na tamaduni za watu mbalimbali. Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Andrea Kim Taegon.  

Askofu mkuu Lazarus You Heung-sik katika mahubiri yake amegusia kuhusu mchakato wa uinjilishaji nchini Korea, Ushuhuda wa imani uliooneshwa na Mtakatifu Andrea Taegon na wenzake 102, mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Umoja na mshikamano wa watu wa Mungu Korea ya Kusini na Kaskazini bila kusahau mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutokana na majanga asilia pamoja na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Mtakatifu Andrea Kim Taegon, alikuwa ni Padre wa kwanza mzalendo kuwekwa wakfu nchini Korea kunako tarehe 17 Agosti 1845. Haya ni matunda ya juhudi za uinjilishaji zilizotekelezwa kwanza kabisa na waamini walei kutokana na uhaba wa Mapadre na hatimaye wamisionari kutoka nchini Ufaransa kuanzia mwaka 1836. Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014 alifanya hija ya kichungaji nchini Korea ya Kusini na kuwapongeza watu wa Mungu nchini humo waliojikita katika mchakato wa uinjilishaji kwa kukazia tunu msingi za Kiinjili, utu, heshima na haki msingi za binadamu, daima umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa vikipewa msukumo wa pekee, kama kielelezo cha imani tendaji!

Askofu mkuu Lazarus You Heung-sik anasema, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika mkutano wake wa 40, lilitangaza kwamba, Jubilei ya Miaka 200 ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Andrea Kim Taegon, iwe ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya kumbukumbu ya maisha na ushuhuda wa Mtakatifu Andrea Kim Taegon. Iwe ni fursa ya kusherehekea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kujikita zaidi katika huduma kwa maskini; umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Iwe ni fursa ya kuondokana na uchoyo, ubinafsi na ubaguzi hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu Francisko katika Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji ndani ya Kanisa, yaani “Magisterium” anakazia zaidi umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kama njia ya kupambana na changamoto kubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Msamaria mwema anawekwa kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kukoleza Injili ya huduma ya upendo. Huu ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini, limefanikiwa kuchangisha kiasi cha dola za Kimarekani milioni 5 zitakazotolewa kwa ajili ya kuchangia mchakato wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika nchi maskini zaidi ulimwenguni kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Imegota miaka 70 tangu Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini ziliposambaratika na kumeguka. Kwa sasa kuna dalili za kutaka kuunganisha tena Korea hizi mbili ili iweze kurejea na kuwa nchi moja. Kuna matumaini makubwa kwamba, iko siku Baba Mtakatifu Francisko atafanya hija ya kitume nchini Korea ya Kaskazini. Ibada hii ya Misa Takatifu imekuwa pia ni fursa ya kuwakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu wanaoteseka kutokana na majanga na maafa asilia huko Haiti. Wamewakumbuka pia watu wanaoteseka kutokana na vita, machafuko ya kisiasa na kijamii kama huko Myanmar na Afghanistan, bila kuwasahau wale wote wanaoendelea kuambukizwa na hata kupoteza maisha kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu ndiyo suluhu ya matatizo na changamoto zote hizi, sehemu mbalimbali za dunia!

Mt. Andrea Kim 200
21 August 2021, 16:25