Familia ya Mungu nchini Korea inaadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Andrea Kim Taegon, Padre wa kwanza mzalendo na mfiadini. Familia ya Mungu nchini Korea inaadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Andrea Kim Taegon, Padre wa kwanza mzalendo na mfiadini.  

Miaka 200 Tangu Kuzaliwa kwa Mt. Andrea Kim Taegon, Mfiadini!

Mtakatifu Andrea Kim Taegon, alikuwa ni Padre Mzalendo wa kwanza nchini Korea. Aliuwawa kikatili tarehe 16 Septemba 1846. Papa Pio XI tarehe 5 Mei 1925 akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 6 Mei 1984. Mama Kanisa anamkumbuka Mtakatifu Andrea Kim Taegon na wenzake 102 kila mwaka ifikapo tarehe 16 Septemba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Askofu mkuu Lazarus You Heung-sik Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, Jumamosi majira ya Alasiri, tarehe 21 Agosti 2021 anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kumbukizi la Miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Andrea Kim Taegon, yaani tarehe 21 Agosti 1821. Mtakatifu Andrea Kim Taegon, alikuwa ni Padre wa kwanza Mkatoliki kuwekwa wakfu nchini Korea. Aliuwawa kikatili tarehe 16 Septemba 1846 wakati wa madhulumu nchini Korea kati ya Mwaka 1839-1846. Papa Pio XI tarehe 5 Mei 1925 akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 6 Mei 1984. Mama Kanisa anamkumbuka Mtakatifu Andrea Kim Taegon na wenzake 102 kila mwaka ifikapo tarehe 16 Septemba. Ibada hii ya Misa Takatifu inaadhimishwa katika lugha ya Kikorea kuonesha amana na utajiri wa Kanisa la Kristo Yesu unaofumbatwa katika mila na tamaduni njema. Ibada hii ya Misa Takatifu inahudhuriwa na watu wa Mungu kutoka Korea!

Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa kuwatangaza Wenyeheri hawa kuwa Watakatifu tarehe 6 Mei 1984 alisema kwamba, kwa hakika, hawa walikuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa! Ukweli wa Kristo Mfufuka umeenea katika historia na tamaduni za watu sehemu mbalimbali za dunia. Ukweli huu uliandikwa nchini Korea kwa Machapisho ya Kidini kutoka China na baadaye, wakafanikiwa kupata Biblia Takatifu, kielelezo cha imani hai ya Kanisa. Kunako mwaka 1874, Mkristo wa kwanza kutoka Korea alitumwa kubatizwa nchini China na huo ukawa ni mwanzo wa Jumuiya ya Wakristo nchini Korea. Ukristo nchini Korea ulianza kushuhudia mateso na madhulumu tangu mwaka 1791. Wamisionari wa kwanza kutoka Ufaransa waliuwawa kikatili kunako mwaka 1836. Jubilei ya Miaka 100 ya Ukristo Nchini Korea, ikapambwa kwa Wenyeheri 103 kutangazwa kuwa Watakatifu na hivyo kuingizwa katika Kitabu cha Watakatifu wa Kanisa Katoliki!

Ni Mashuhuda wa imani, ambao waliamua kusimama kidete kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu kwa kusadaka maisha yao, kama Maandiko Matakatifu yanavyosema “Siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti.” 2 Kor 4:10-11. Mama Kanisa kwa moyo wa shukrani, akauimbia Utatu Mtakatifu wimbo wa sifa, ukuu na utukufu, mwanzo wa maisha na utume mpya wa Kanisa nchini Korea. Kwa hakika, damu ya mashuhuda wa imani, tangu mwanzo, imekuwa ni mbegu ya Ukristo sehemu mbalimbali za dunia. Waamini kutoka Korea ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Kristo Yesu ni ukweli, njia na uzima, anayeendelea kuwashibisha waja wake kwa chakula cha uzima, kilichoshuka kutoka mbinguni, yaani Ekaristi Takatifu, chemchemi ya utakatifu na ushuhuda wa imani. Tangu mwanzo, Kanisa nchini Korea limesimikwa katika damu ya mashuhuda wa imani!

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Lazarus You Heung-sik Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, alizaliwa tarehe 17 Novemba 1951 huko Nonsan-gun Chungnam. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 9 Desemba 1979 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 9 Julai 2003 akamteuwa kuwa ni Askofu mwandamizi wa Jimbo Katoliki la Daejeon {Taejon}, na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 1 Aprili 2003. Na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 11 Juni 2021 akamteuwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu. Askofu mkuu Lazarus You Heung-sik akiwa nchini Korea ya Kusini licha ya majukumu na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu, alibahatika kuteuliwa kuwa ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini. Ni katika muktadha huu, amewahi kutembelea Korea ya Kaskazini ili kunogesha mchakato wa uponyaji na maridhiano kati ya Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini.

Mtakatifu Andrea Kim
20 August 2021, 15:20