Ibada ya Bikira Maria inapata chimbuko lake chini ya Msalaba wa Kristo Yesu. Bikira Maria ni daraja inayowaunganisha waamini na Kristo Yesu. Ibada ya Bikira Maria inapata chimbuko lake chini ya Msalaba wa Kristo Yesu. Bikira Maria ni daraja inayowaunganisha waamini na Kristo Yesu. 

Ibada kwa Bikira Maria Inapata Chimbuko Lake Chini ya Msalaba!

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 29 Agosti 2021 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 500 ya Kuvikwa Taji kwa Bikira Maria wa Oropa, kwenye Madhabahu ya Jimbo Katoliki Biella, lililoko Kaskazini mwa Italia. Bikira Maria kuvikwa taji la dhahabu ni tukio linaloadhimishwa kila baada ya miaka 100. Shukrani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya utimilifu na utakatifu wa maisha. Hapa ni mahali pa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu! Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni sehemu ya familia kubwa ya Wakristo, daima wako chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Wakristo ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kumbe, kama sehemu ya Kanisa wanao wajibu na dhamana ya kuliombea Kanisa zima; kuwaombea watu wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali; watu wanaoogelea katika dimbwi la huzuni na machungu ya maisha; wagonjwa na wale wote walioko kufani; wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau watu wanaoteseka kutokana na athari za majanga asilia.  Haya ni maeneo yanayodhihirisha ufunuo wa: Upendo, ukuu, wema na huruma ya Mungu kwa waja wake.

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 29 Agosti 2021 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 500 ya Kuvikwa Taji kwa Bikira Maria wa Oropa, kwenye Madhabahu ya Jimbo Katoliki Biella, lililoko Kaskazini mwa Italia. Bikira Maria kuvikwa taji la dhahabu ni tukio linaloadhimishwa kila baada ya miaka 100. Kwa mara ya kwanza tukio hili liliadhimishwa tarehe 30 Agosti 1620, kama alama ya shukrani kwa Bikira Maria aliyewalinda na kuwakinga dhidi mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza mwaka 1599. Tangu wakati huo, kumekuwepo na mabadiliko makubwa yaliyofanywa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Oropa na hivyo kuwawezesha mahujaji kupata amani na utulivu wa ndani, huku wakimtumainia Mwenyezi Mungu, chemchemi ya faraja na upendo.

Katika mahubiri yake, Kardinali Giovanni Battista Re amekazia kuhusu Ibada kwa Bikira Maria inayopata chimbuko lake chini ya Msalaba wa Kristo Yesu. Bikira Maria ni daraja inayowawezesha waamini kumwendea Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo kamili. Jubilei hii iwawezeshe waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Bikira Maria, kama Mama, Malkia na nyota angavu anayeonesha njia, ili waamini waweze kujiaminisha kwake. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba Mwenyezi Mungu anapewa nafasi ya kwanza katika maisha ya waamini kwa kushika kikamilifu Amri Kumi za Mungu, dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ilibidi kuhailisha maadhimisho haya kwa kipindi cha mwaka mmoja, hadi kufikia mwaka 2021. Hii ni fursa ya kumtolea Bikira Maria mateso, mahangaiko na matumaini ya watu wa Mungu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kwa zaidi ya miaka 500 waamini wamekuwa wakimiminika katika madhabahu hii, wakiomba msaada, ulinzi na tunza kutoka kwa Bikira Maria.

Wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuathirika sana kutokana na madhara makubwa yanayosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ni ugonjwa ambao umegusa na kutikisa msingi wa imani, sekta ya afya, uchumi pamoja na kupukitisha fursa za ajira. Wanafunzi wengi wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na changamoto zilizojitokeza katika sekta ya elimu. Ndiyo maana kwa mara nyingine tena, waamini wanakimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria ili awasaidie kupambana na janga la UVIKO-19. Hiki ni kipindi cha kupyaisha imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani sanjari na kuzingatia mambo msingi katika maisha. Ni changamoto ya kutangaza na kushuhudia upyaisho wa maisha ya Kikristo, ili kujenga na kudumisha: ukarimu, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, daima wakijielekeza kuangalia kesho ya binafamu. Wakristo waoneshe uaminifu kwa dhamana na maisha yao ya Kikristo. Waamini wasisite kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwani Kristo Yesu akiwa Msalabani aliwakabidhi wafuasi wake wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Kristo Yesu akiwa juu Msalabani alimkabidhi Bikira Maria kwa Mtakatifu Yohane na hivyo Bikira Maria akawa Mama wa maisha ya kiroho, tayari kuwaombea msaada wale wote wanaokimbilia ulinzi na tunza yake.

Zawadi kubwa ambazo Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake ni Bikira Maria kama Mama wa Kanisa na Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria anachukua nafasi ya pekee katika Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka. Bikira Maria ni shule maalum ya kuweza kumjifunza Kristo Yesu na njia inayowapeleka waamini kwa Kristo Yesu. Waamini wajenge na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, huku wakimtukuza Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele, daima wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Kwa njia ya Kristo Yesu na kwa maombezi ya Bikira Maria, waamini wajitahidi kuwa ni mashuhuda waaminifu wa tunu msingi za Kikristo katika maisha yao ya kila siku. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali anasema, Bikira Maria ni shule ya imani kwa Mwenyezi Mungu; upendo kwa Mungu na jirani. Kristo Yesu ni mwingi wa huruma na mapendo, kwa wale waamini wanaokimbilia chini ya mbawa zake kama alivyofanya kwa Mtakatifu Petro alipomkana mara tatu na alipokutana mubashara na Mtakatifu Paulo Mtume akiwa njiani kuelekea Dameski. Ni furaha kwa Bikira Maria kuwaona watoto wake wakikimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu ili kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Bikira Maria, Mama wa huruma, awaombee mwanga angavu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kuweza kubadili yale ambayo yamo katika uwezo wao. Wawe na moyo wa utulivu, kupokea yale wasiyoweza kubadili. Awakirimie hekima na busara ya kuweza kung’amua mema yakufuata katika maisha!

Ibada ya Misa Maria Oropa
29 August 2021, 15:48