Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka viongozi wa kidini kukoleza majadiliano ya kidini kwa kuumwilisha Waraka wa Fratelli tutti katika uhalisia wa maisha ya watu! Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka viongozi wa kidini kukoleza majadiliano ya kidini kwa kuumwilisha Waraka wa Fratelli tutti katika uhalisia wa maisha ya watu! 

Hati ya Udugu wa Kibinadamu Itekelezwe katika Maisha Ya Watu

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawachangamotisha viongozi wa kidini sehemu mbalimbali za dunia, kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kikamilifu katika utekelezaji wa Waraka wa Kitume Baba Mtakatifu Francisko wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” katika ngazi ya maisha ya wananchi wa kawaida anasema Askofu Willbard Kitogho Lagho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na matunda yake ni Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbalimbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote.

Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ayatollah Ali Sistani anasema, udugu wa kibinadamu unapata chimbuko lake katika kazi ya uumbaji inayowafanya kuwa ndugu na katika imani inayowaunganisha na kuwafanya kuwa ni ndugu wamoja. Usawa kama watoto wa Mungu ndilo jambo muhimu si tu katika masuala ya kidini bali hata katika utamaduni. Kwa Wakristo udugu huu umefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, lakini imewachukua watu wa Mungu miaka mingi sana kuutambua na kuumwilisha udugu huu katika vipaumbele vyao vya maisha.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu kama nguzo ya majadiliano ya kidini, inalenga kudumisha amani duniani. Ni sehemu ya utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kama hata kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Hii ni hati ambayo imeandaliwa kwa sala na tafakari ya kina, ili kuweza kudhibiti: vita, uharibifu unaosababishwa na vitendo vya kigaidi, chuki na uhasama kati ya watu! Lengo ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, chachu muhimu sana ya ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu! Hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani duniani. Hii ni hati inayopata chimbuko katika misingi ya imani kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo! Iliandaliwa kwa usiri mkubwa. Lakini pamoja na faida zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko mara kwa mara amekuwa akipokea shutuma kali dhidi yake na wakati mwingine inambidi kufanya maamuzi mazito! Haya ni maamuzi yanayotolewa baada ya sala, tafakari ya kina na ushauri.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawachangamotisha viongozi wa kidini sehemu mbalimbali za dunia, kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kikamilifu katika utekelezaji wa Waraka wa Kitume Baba Mtakatifu Francisko wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” katika ngazi ya maisha ya wananchi wa kawaida. Changamoto hii imetolewa hivi karibuni na Askofu Willybard Kitogho Lagho wa Jimbo Katoliki Malindi, Kenya wakati alipokuwa anachangia mjadala kuhusu Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Huu ni wakati kwa viongozi wa Kanisa na waamini wa dini ya Kiislam kukaa pamoja na kujadiliana. Waraka huu ni dira na mwongozo wa umoja, mshikamano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu ndani na nje ya Bara la Afrika. Hii ni fursa ya kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Bara la Afrika. Hii inatokana na ukweli kwamba, dhana ya familia imekomaa na kuota mizizi Barani Afrika, ikilinganishwa na sehemu nyingine za dunia.

Bara la Afrika ni ushuhuda kamili wa jinsi ambavyo familia ya Mungu Barani Afrika inavyoweza kukoleza na kudumisha umoja na mafungamano ya kifamilia na kijamii. Majadiliano haya ni mchango mkubwa uliotolewa na Chuo Kikuu cha Tangaza kwa kushirikiana na wadau wengine wa Kimataifa kutoka Marekani na Indonesia kuanzia tarehe 19 hadi 21 Agosti 2021 kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii! Kwa upande wake, Monsinyo Lucio Sembrano, Afisa kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika hotuba yake amekazia umuhimu wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kujenga dunia inayosimikwa katika msingi wa haki na mshikamano wa kidugu. Hii ni changamoto ya kusimama kidete kulinda na kudumisha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na ikolojia fungamani ya binadamu. Umefika wakati wa kujifunza kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza kati ya watu wa Mataifa pamoja na kutambua na kuthamini mchango unaoweza kutolewa na kila mmoja katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2015, anawataka watu kutambua na kuheshimu: utu, uhuru na hali ya mtu kujitegemea. Yote haya yanapaswa kuonesha mahusiano kati ya watu kwa kukazia kwa namna ya pekee kabisa katika: heshima, haki na upendo. Udugu unaopata chimbuko lake kwa kumwongokea Kristo ni kifungo muhimu katika maisha ya kifamilia na kijamii, hali inayoonesha umoja katika utofauti ulioko kati ya wanandugu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wakiwa na asili na utu sawa. Dhambi inapoharibu mshikamano huu wa kidugu, hapo utamaduni wa utumwa unajipenyeza na kutoa nafasi kwa mtu kumkataa jirani yake, nyanyaso na hapo madhulumu yanapoanza kuonekana. Utu na heshima ya binadamu vinatoweka na haki msingi za usawa katika taasisi zinamong’onyoka. Kutokana na mapungufu yote haya, Jumuiya ya Kikristo haina budi kuwa ni kielelezo cha umoja kati ya ndugu kwa kuonesha umoja katika utofauti bila kuathiri utu wala kumtenga mtu yoyote kutoka katika Familia ya Mungu. Hii ni kwa sababu wote ni watoto wateule wa Mungu wanaoimarishwa kwa kifungo cha udugu katika Kristo.

Baba Mtakatifu anasema hata leo hii, kuna watu wanalazimika kuishi katika mazingira ya utumwa, kwani kuna mifano hai inayoonesha kwamba, kuna watu wanafanyishwa kazi za kitumwa; wahamiaji wananyimwa haki zao msingi; wanadhulumiwa na kunyanyaswa; wanawekwa kizuizini katika mazingira hatarishi; wananyanyaswa na kudhulumiwa na waajiri kwa kudhibiti mikataba na vibali vya kuishi ugenini. Kuna wanawake, wasichana na watoto ambao wametumbukizwa katika biashara haramu ya ngono; wengine wanauzwa kama biadhaa na kulazimishwa kufunga ndoa za shuruti. Kuna baadhi ya watu wanatumbukizwa katika biashara haramu ya viungo vya binadamu; watoto wanapelekwa mstari wa mbele kama chambo katika mapigano ya kivita; kuna baadhi ya watoto wanaolazimishwa kuuza dawa haramu za kulevya na wengine wanaasiliwa kinyume cha sheria za kimataifa. Kuna baadhi ya watu wametekwa nyara na kufungwa na vikundi vya kigaidi kitaifa na kimataifa.

Baba Mtakatifu anasema, hizi zote ni sura za utumwa mamboleo na kwamba, zina sababu nyingi ambazo zimepelekea kuendelea kuwepo kwa biashara na utumwa mamboleo. Sababu msingi ni dhambi inayoathiri moyo wa binadamu kiasi hata cha kuukataa ubinadamu wa mtu mwingine, hali inayowafanya baadhi ya watu kuwanyanyasa na kuwatumia binadamu wenzao kama bidhaa na njia ya kujinufaisha binafsi. Mambo mengine ni umaskini, ujinga, ukosefu wa fursa za ajira, biashara haramu ya binadamu na matumizi haramu ya mitandao ya kijamii inayowafanya vijana wa kizazi kipya kuwa watumwa pamoja na kuvutiwa kujiunga katika makundi ya kivita, uhalifu, matumizi ya nguvu pamoja na kujihusisha na vitendo vya kigaidi. Baba Mtakatifu anasema sababu nyingine zinazopelekea uwepo wa utumwa mamboleo ni pamoja na rushwa na ufisadi unaojipenyeza katika vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na magenge ya uhalifu wa kitaifa na kimataifa, hapa utu na heshima ya binadamu vinawekwa rehani na badala yake, fedha inapewa kipaumbele cha kwanza.

Taasisi na Mashirika ya kitaifa na kimataifa yajifunge kibwebwe kuhakikisha kwamba, yanavunjilia mbali magenge ya uhalifu wa kimataifa, kwa kuwawajibisha wahusika. Walaji watambue wajibu wao wa kijamii kwani tendo la kununua linafumbata kanuni maadili na mafao ya kiuchumi. Monsinyo Lucio Sembrano, Afisa kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini amehitimisha kwa kusema mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni jukwaa linaonesha uwepo wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya mwanadamu. Changamoto kubwa ni ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu kama njia ya kuzipatia changamoto mamboleo ufumbuzi wa kudumu!

Udugu Afrika
24 August 2021, 15:09